Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Waheshimiwa Mawaziri waliokaa pale, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, kwenye Mpango wa Serikali na mipango yetu mingi wala hatuhitaji kutumia elimu kubwa sana hapa. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, inatakiwa awaambie Watanzania na Wabunge wenzake kwamba hivi Wizara ya Fedha inakwama wapi kuchukua kodi kwa Watanzania ambao wanapaswa kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni fedha ambazo zipo walipakodi wa nchi hii hawafiki 20%, ni fedha ambazo zipo watu wanafanya biashara kiholela, mapato yanapotea ya Serikali, walipeleka zile mashine za EFD lakini wakaweka gharama kubwa sana, wangeweza kuzinunua wakawapa wafanyabiashara bure halafu kila fedha isilipwe cash ili watu ambao wanapaswa kulipa kodi walipe kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango katika jambo la kuanza nalo achana na vyanzo vipya, nenda kwa watu ambao wanafanya biashara, wenzetu mbona wameweza na wanafanya maeneo mbalimbali wanaweza kufanya kazi tupate fedha. La pili, kwenye matumizi ya fedha ya Serikali, ili Watanzania walipe kodi vizuri ni lazima wakilipa kodi wawe na uhakika fedha inayolipwa inaenda kufanya kazi za maendeleo kwa wananchi. Kama watakuwa wanalipa kodi halafu wanaona kwenye Ripoti ya CAG kila mwaka kuna madudu mengi maana yake watu wanakata tamaa. Kwa hiyo lazima tusimamie watu walipe kodi lakini pia tusimamie fedha zifanye kazi ambayo imekusudiwa kama ambavyo kila Mbunge anasema amepeleka fedha nyingi majimboni na huduma zinapatikana, wasimamie fedha ya Serikali zisipotee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango ya Serikali kuna miradi mingi sasa hivi imekwama, maana yake lazima tushone koti kulingana na ukubwa wa kitambaa, tuwe na miradi michache ya kimkakati lakini mradi ukianzwa umalizike. Hivi kwa mfano leo barabara kama ile ya kutoka Tarime mpaka Mugumu (Serengeti) ambayo ukanda ule wote wa kwangu wanaitegemea, mkandarasi ameenda site, ameenda amechimba chimba ameondoka mvua zinanyesha watu wanakwama kutwa nzima, kwa hiyo unakuwa huna maelezo. Kwa hiyo katika mipango yao miradi ile ambayo imekwama ni vizuri wakatenga fedha wakaimalizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kulikuwa kuna malalamiko mengi, unatoka pale Ziwa Victoria uende mpaka Rorya, uende mpaka Tarime, wanajenga tenki pale Sirari, mkandarasi amehama kaondoka na vifaa pale site. Kwa hiyo, miradi ile viporo, barabara mbalimbali nchi nzima, miradi ya maji, Miradi ya REA ya kupeleka umeme kwenye vitongoji, hii ndio mipango ya Serikali ifanyike kumalizia miradi ambayo imekamilika pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukienda Musoma. Bandari ya Musoma leo haifanyi kazi, kwa hiyo, ina maana bidhaa inakuja mpaka Mwanza halafu wanapeleka kwa malori mpaka pale Musoma. Bandari ya Musoma ni sehemu ya uchumi, ikikamilika ile wataenda mpaka Kisumu, wataenda mpaka Jinja, kule Kampala, Bukoba na Kanda ya Ziwa yote ikachangamka, tupate huduma pale ni sehemu ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Musoma umesimama, hamjamalizia, tumepata misiba tunatumia gharama kubwa sana. Watu wanaumia migongo, lakini wangeweza kupanda ndege kutoka hapa, Dar es Salaam, wakaenda Musoma na ni sehemu ya Baba wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Liganga na Mchuchuma imezungumzwa miaka yote hawahitaji elimu mradi upo, chuma kipo, makaa ya mawe yapo ni Mpango wa Serikali. Iwalazimishe kazi ile iweze kukamilika tupate huduma pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ya kujenga masoko. Hivi kwa mfano, eneo la Sirari kuna eneo lipo potential kabisa kwa mazao yote ya Tarime na Rorya. Siku hizi Wakenya wanachukulia mazao mashambani hata yakiwa mabichi ambayo hayajaiva. Ukijenga pale soko la kimataifa maana yake mazao yote ya Kanda ya Ziwa utayauza pale Sirari, watu watachangamkie masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kule Tarakea, nenda Horohoro, Tanga, nenda Tunduma, mkiwekeza maeneo hayo mtapa fedha nyingi sana na uchumi wetu utakuwa na maeneo haya wananchi watapata huduma nzuri zaidi, ndiyo maana nasema katika mipango ya Serikali wala huhitaji kutumia nguvu kubwa, ni elimu ya kawaida kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninataka nisema ni watumishi wa umma; kweli tumejenga shule, sekondari, lakini walimu kwenye shule hawapo. Katika sekondari zetu mnazungumza habari ya sayansi, kuna watoto wetu wanafanya mitihani ya form four, hawajasoma practical, wanasoma kwa kuangalia vitu kwa macho, sasa sayansi anaelewa namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima mkaweke mpango kwamba, shule zote za sekondari mpeleke vifaa vya maabara, watoto wasome sayansi tupate madaktari, tupate ma-engineer, tupate manesi na ni jambo ambalo linawezekana, kama ambavyo tumejenga madarasa. Sasa tuelekeze kuajiri walimu wenye sifa, lakini pia na vifaa ambavyo vitasaidia katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ni, mipango ya Serikali. Ukifuatilia miradi mingi ya Serikali kwanza inabidi utafute fedha ya kupeleka mradi halafu unakwenda kulipa fidia kwa sababu, maeneo hayajapangwa. Mpaka leo tunapanga hapa mipango, lakini kuna ugomvi mkubwa kati ya wakulima na wafugaji, hayajatengwa maeneo ya kulima hatukutenga maeneo ya wafugaji, hatukutenga maeneo ya viwanda na maeneo ya miji. Kwa hiyo, ukipeleka fedha ya mradi fulani ni lazima utenge fedha ya kwenda kulipa fidia na wananchi wetu hawajalipwa, wanalalamika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ni lazima tupange, kwamba, tuondoe ugomvi wa wakulima na wafugaji, tuondoe ugomvi wa wananchi waliokaa karibu na Hifadhi ya Serengeti na maeneo mengine kwa mipango. Tujadili kwamba, wanyama wapo kweli, lakini watu wameongezeka sasa, kipi kifanyike?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua, haya yakifanyika maana yake ni nchi yetu itaenda kasi. Mipango hii ambayo inapangwa hapa tumeshaijadili mara kadhaa, tunamwelekeza Waziri wa Mipango, Mheshimiwa Profesa Kitila na mwenzako wa Fedha. Miradi yetu ile viporo na ujue huko tunakoenda mwakani, unajua kuna nini mwakani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii viporo naomba mkaikamilishe, ili Wabunge, mimi nina mpango wa kurudi Bungeni sina mpango wa kuachia Jimbo. Sasa siwezi kurudi Bungeni kama Barabara yangu ya Tarime – Serengeti haijakamilika, maji ya Ziwa Victoria hayajaenda kule kwangu, kama vifaa vya maabara haujapeleka, kama hujaondoa ugomvi kati ya wakulima na wafugaji, kama hujaondoa mgogoro uliopo kati ya watu wa Hifadhi ya Serengeti, wananchi wangu na kule Serengeti kwenyewe. Haya mambo yanawezekana, huhitaji kuwa Profesa wala Daktari, ni willingness. Profesa jambo la ushauri la mwisho ni, wewe ni mtaalam, nendeni mkaangalie shida ipo wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, placement; kama wanaweka mtu mahali, waweke mwenye uwezo. Tumewashauri mara kadhaa, angalieni Makatibu Tawala wa Mikoa ambao wanasimamia watumishi wote katika mikoa yetu. Waangalie Wakurugenzi wetu, wawachuje wale ambao wanaweza kufanya vizuri kazi ya mipango, kusimamia fedha na mapato yetu wabaki, wale ambao hawana sifa waondoeni, kuna shida gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa ni kweli kwamba tuna shida ya placement katika nchi hii. Kuna watu hawana uwezo, lakini ni Mkurugenzi pale, kwa hiyo, mapato yanapotea. Leo watu wanakula fedha mbichi, hata kwenye masoko fedha zinapotea, kwenye minada fedha zinapotea, watu wetu hawalipi kodi, ukichunguza wale watumishi wenyewe ndio wanazipitisha katika mlango wa nyuma. Kwa hiyo, kupata fedha, nchi hii zimejaa tele ni mipango na commitment, inawezekana huhitaji kuwa msomi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)