Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa kuchangia katika mada hizi mbili ambazo zimeletwa na Waheshimiwa Mawaziri hapa. Nitaongelea zaidi kwenye suala zima la Mpango wa Maendeleo pamoja na vipaumbele vyake ambavyo wameweka. Naomba kuvinukuu, wameongelea suala la kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji na utoaji wa huduma, kukuza uwekezaji na biashara kuchochea maendeleo ya watu na mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi katika suala zima la kukuza uwekezaji na biashara. Nilikuwa naangalia katika taarifa ya Mheshimiwa Profesa, pale ukurasa wa tisa, anazungumzia suala la uchangiaji katika ukuaji wa uchumi na sekta ambazo zinaongoza amezitaja pale; ametaja kilimo kina 15.9%, ujenzi 15.5%, madini 11%, viwanda na mtiririko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nitarudia kulisema na nimekuwa nikilirudia mara kwa mara. Kuna sekta moja ambayo tunaisahau sana katika suala zima la kuchangia ukuaji uchumi, lingeweza kuchukua nafasi kubwa sana kwa sababu, masuala ya viwanda pamoja na kwamba, viwanda ina asilimia tisa hapa, pengine ingekuwa na asilimia nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote nazungumzia suala la uendelezaji miliki. Sekta ya miliki tunaisahau, lakini tujue kabisa sensa ya watu na makazi iliyopita imezungumza suala zima la ongezeko la watu, tumetoka milioni 48 sasa tupo milioni 61. Ukiangalia population density ambayo tulikuwa nayo mwaka 2012 mtu mmoja alikuwa anaweza ku-occupy hekta 2.5. Sasa hivi tuna hekta 1.4 kwa sensa ya mwaka 2022 tujue wazi kwamba, ardhi inazidi kwisha, watu wanaongezeka. Kwisha kwake kunatokana pia na mpangilio mbaya ambao pengine hatujaweza kuusimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukienda kwenye sekta ya miliki, uwekezaji wake ni rahisi na ni mzuri na unachangia katika sekta nyingi, watu wa viwanda watauza, watu wa chakula watauza, watu wengi wa kutosha watapa ajira. Ukiangalia hitaji la makazi kwa watu na tunahitaji makazi, si yale tu ya kusambaa ya kwenda horizontal, tunataka yale ya vertical. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mahitaji, nilisema hata juzi, ni nyumba 390,981 zijengwe kwa mwaka, lakini taasisi zetu zote ukiangalia National Housing, nenda sijui Watumishi Housing na nenda hizi Real Estate zilizopo za private, uwezo wao wa kujenga nyumba kwa mwaka ni nyumba 1,153. Sasa ni lini watafikisha hizo nyumba 300,000 kwa mwaka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo tukasema suala zima la kufungua wigo kwa wawekezaji. Tukazungumzia suala la Diasporas ambao wanapata hadhi maalum, waweze kuwekeza kwenye nyumba. Tukazungumzia suala la mtu wa nje, ambaye atakuja ajenge nyumba na kuuza, ataondoka, akijenga hapa anaiacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia masuala ya Mheshimiwa Mtemvu, kule kwake Magomeni Kota ambako tunasema unafanya land pulling. Unakusanya vijumba vyote vile ambavyo havina ile hadhi pengine, halafu wale watu wote wanapata nyumba katika yale maeneo, lakini unajenga kwa kwenda juu; uta-save ardhi yako, lakini accommodation ya watu wengi itakuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili hatulioni kama ni suala linalochangia kwenye ukuaji. Hizi sekta zilizowekwa nadhani sekta ya miliki ingeweza kushika hata nafasi ya tatu au ya nne katika uchangiaji wa uchumi. Ningeomba sana Serikali, tumelisema sana hili, tuone namna bora ya kuona ni jinsi gani tutakwenda kushirikisha sekta hii ili iweze kuingia kwenye ukuaji wa uchumi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie madini, wanafanya vizuri sana, hasa hawa wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, tungeomba sasa ule umiliki wa ardhi kwa hawa wachimbaji, waweze kumilikishwa maeneo yao yale, lakini pia, watatumia ardhi ile katika kujiongezea mitaji. Wanapoongeza mitaji tayari pia, kunakuwa na wigo wa kuongeza uchumi katika suala zima la ongezeko la fedha. Bila kuwawezesha kwa kuwa na miliki ya ardhi bado itakuwa ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala zima la wafugaji, sasa hivi ni wachungaji, wanaofuga ni wachache sana. Nako pia, tukaangalia wale wenye maeneo wakapewa elimu ya kuweza kufuga wa ufugaji wa kisasa, wakazalisha nyasi wao wenyewe kwa chakula, itakuwa imesaidia sana hata ile migogoro iliyopo. Tukaacha yale maeneo ya vijiji ambayo wametenga, kwa ajili ya wafugaji, kuna wale ambao ni ma-settler wana maeneo yao, lakini bado wanataka kuingia kwenye maeneo mengine. Wale wawezeshwe namna ya kuweza kulima nyasi, waweze kuzalisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye Sekta ya Uvuvi inakwenda vizuri na inafanya vizuri, lakini tuone namna bora sasa ya kuwa na utunzaji wa mazalia ya samaki, ili yaweze kutunzwa pale tunapotaka kuvua samaki, maana yake ni yaende kwa msimu. Maeneo mengine yaachwe yaendelee kama yalivyo, lakini tuwe na maeneo specific ambayo tunajua kwamba, tunaenda kuvuna samaki pale na ongezeko lake limekuwa ni kubwa. Kwa hiyo, ni vizuri pia, tukaangalia sekta hizi katika suala zima la kuwawezesha wanaosimamia na kuweza kuona ni jinsi gani watakwenda katika kutunza mazingira, lakini pia na kuweza kufanya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana Serikali kwenye Sekta ya Uchukuzi na usafirishaji wamefanya vizuri kabisa katika miundombinu yote SGR, bandari na mambo mengine. Kuna miradi tunayoianza haiishi kwa wakati, viwanja vya ndege, Uwanja wa Ndege wa Mwanza uko pale kila leo na hata kwenye maandiko hapa sikuona wapi upo? Labda mtu atanisaidia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, umekaa pale, kuna changamoto ya watu wanadai fidia na uwanja umesimama hauwezi kuendelezwa. Ningeomba sana miradi ikianza ikamilike ili tuweze kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji. Jana wamempongeza Mheshimiwa Aweso na mimi nampongeza sana kwa miundombinu ya kawaida ameweka. Changamoto iliyopo ni usambazaji wa maji yale, miundombinu iliyopo ni chakavu, mingine toka watu wapo 100,000 na sasa watu wapo 500,000 haiwezekani miundombinu ileile iweze kusambaza maji. Utaweka matenki makubwa, utaongeza vyanzo vya maji, lakini kama hatufumui mfumo mzima wa usambazaji bado changamoto itakuwepo. Kwa mfano, watu wa Mwanza hawaelewi maji yanatoka Mwanza, Shinyanga, sasa yanakuja Dodoma halafu Mwanza wana changamoto ya maji na maji yapo Ziwa Victoria, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, miundombinu yetu ya usambazaji maji ndio inayotakiwa kuboreshwa kwa sababu, matenki ya reserve yapo mengi, chanzo kipo kimewekwa, changamoto tu ni namna ya kuweka miundombinu itakayofuatilia usambazaji katika maeneo haya. Tukilifanya hili itakuwa imetusaidia sana katika suala zima la kuondoa changamoto iliyopo na kuweza kuendelea kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa namna ambavyo amepongezwa na kuweza kupewa degree kutoka kwenye kile Chuo Kikuu kule India, wametambua mchango wake. Kwa hiyo, sisi kama Tanzania hatuna budi kuendelea kumuunga mkono pale ambapo yeye kasimamia zile R4, zipo vizuri. Kwa hiyo na sisi tuendelee kuhakikisha kwamba, Mheshimiwa Rais…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Kengele ya pili.

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.