Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipatia fursa hii ya kuweza kusimama kutoa mchango wangu pamoja na maoni, kufuatia taarifa tatu zilizowasilishwa hapa Bungeni. Taarifa ya Kamati ambayo inashughulika na Masuala ya Bajeti, taarifa ambayo imewasilishwa na Waziri wa Nchi, Mipango na Uwekezaji pamoja Taarifa ya Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nikupongeze sana. Niwapongeze sana Mawaziri na pia, nimpongeze sana Rais, mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuweza kuisogeza mbele nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijikite zaidi kwenye maeneo makuu matatu; eneo la kwanza, nitajikita kwenye masuala ya mazingira ambayo yapo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Eneo la pili, nitajikita zaidi kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii na eneo la tatu, nitajikita zaidi kwenye eneo la Wizara ya Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais, nikiri kwamba, kweli Mheshimiwa Waziri amezungumzia wazi kabisa miradi yote ya mazingira, hususani ile ya tabia ya nchi, mbali na changamoto ambayo tunaipata kwa sababu, mifuko hii tunategemea fedha nyingi kutoka kwa wadau wetu wahisani kutoka nje. Wizara imetamka wazi kabisa, kwenye mpango wetu huu ambao tayari tunaenda nao itajikita zaidi kukusanya fedha ndani ya nchi kwa ajili ya kutekeleza ile miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa kama Mjumbe wa Kamati, tumekuwa tukilalamika sana kwenye Kamati yetu kuhusiana na miradi yetu mikubwa, ni mizuri, lakini mwisho wa siku inakosa fedha, kwa ajili kuiendeleza. Sasa, Mheshimiwa Waziri, ameyazungumza hapa leo kwamba, miradi hiyo sasa hivi itatengewa fedha kupitia Wizara zetu. Kwa hiyo, ni jambo kubwa na ni la kupongezwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tukiangalia kwenye miradi kama hii ya mazingira ni miradi ambayo inakuwa sura ya kimuungano na fedha ambazo zinapatikana zinakuwa zinagawiwa, nusu zinabakia huku Tanzania bara na nusu zinaenda Zanzibar. Ukweli usiopingika ni mabadiliko ya tabianchi, hususani kwa upande wa Zanzibar, ndiyo inayaumiza zaidi. Kwa hiyo, niombe sana Wizara, kwenye mgawanyo wa fedha ambazo tayari tutakuwa tunazipata tuhakikishe kwamba, upande wa Zanzibar nao tunaelekezea fedha nyingi, kwa ajili ya kunusuru Kisiwa chetu cha Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mengi yamelalamikiwa hapa na Wabunge mbalimbali. Kwa mfano, kuna maeneo ya kule Pemba, nayo sasahivi yanaathirika na ujio mkubwa wa maji, pia, maeneo ya Nungwi, maeneo ya Mjini pale Stone Town, yote hayo kutokana na mabadiliko ya tabianchi maji sasa hivi yanaingia kwenye mitaa ya watu. Fedha tunazozitegemea tayari ni za Muungano kwa hiyo, niiombe sana Wizara kwenye hili ni lazima tuliangalie, lakini pia, tuiangalie Zanzibar kiupekee zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni, Maliasili na Utalii. Kwenye eneo hili Mheshimiwa Rais ni lazima tumpongeze sana kwa asilimia mia moja. Kwa kweli, Mheshimiwa Rais amejivua Urais akasema lazima niingie mtaani, niingie msituni, niingie baharini, kuhakikisha Tanzania naitangaza. Kwa hiyo, lazima Mheshimiwa Rais kwenye eneo hili tumpongeze sana kusema ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameutangaza utalii na sasa hivi ukiingia maeneo yote duniani kote Royal Tour ndiyo inazungumzwa zaidi. Kwenye eneo hili Mheshimiwa, kama Wizara, lazima tujipange pia, tumhakikishie Mheshimiwa Rais ile target ya kusema kwamba, tunataka tuingize watalii wasiopungua 5,000,000 basi tuifikie. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Mipango amezungumzia kwamba, mpaka sasa hivi tumeshaingiza watalii wasiopungua 3,000,000 na points, lakini target hii tutaifikiaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima Wizara iweke mipango mikakati ili kuhakikisha kwamba, utalii utaongezeka zaidi na target yetu ya 5,000,000 inafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni utalii wa fukwe tumeuacha na tumejikita zaidi kwenye utalii wa wanyama pori, milima pamoja na misitu, lakini kwenye utalii wa fukwe bado hatujaweka mikakati. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, angalia zaidi kwenye eneo la fukwe, tunayo maeneo mengi bado hatujawekeza. Tukiwekeza zaidi kwenye fukwe naamini kwa 100% ile target ya Mheshimiwa Rais kufikia watalii 5,000,000 tutaifikia na tunaweza tukaongeza zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri tuangalie nchi ya Morocco, wao hawana wanyama na milima, lakini wana fukwe za Sahara na wanaingiza watalii zaidi ya milioni 10 kwa mwaka. Kwa nini Tanzania ambao tumebarikiwa na vivutio vingi vya kiutalii tusifikie kwenye target hiyo ya milioni tano? Ninaamini kabisa kwenye eneo hili tunaenda kuongeza watalii mara dufu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hilohilo la utaalii pia tuangalie zaidi utalii wa vyakula, bado huko hatujawekeza zaidi kwenye eneo la vyakula. Sasa hivi ukiangalia ukienda kwenye hoteli nyingi za kitalii, vyakula vingi vinavyoagizwa utasikia south Afrika au Nchini Kenya, lakini nchini kwetu vyakula vingi ambavyo tunazalisha ni vyakula vilevile traditional crops, ni vyakula vya kikawaida tu ambavyo vyote tumevizoea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watalii wenzetu hawa wanapotoka duniani kuna vyakula vyao wamevizoea na wanapokuja kwenye nchi zetu hizi mara nyingi sana wanapendelea vyakula ambavyo wametoka navyo nyumbani kwao huku pia wavikute. Kwa hiyo, tuangalie namna gani tunaweka mkakati kutafuta mbegu kabisa za Ulaya, zikaja hapa nchini kwetu tukapata fursa na wakulima wetu wakaweza kulima mazao hayo baadaye wakapata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kwenye Wizara ya Uvuvi, bado nitaendelea kuzungumza zaidi na Mheshimiwa Ulega kwenye zao la mwani. Niipongeze sana Wizara yako, imejitahidi sana kutoa elimu kwenye zao la mwani. Kwa sasa hivi elimu imewafikia Watanzania kwa 100% kwa hiyo niwapongeze sana kwenye hilo, nimeona mikakati yako mizuri kabisa ya kuisaidia nchi hii hususan kwenye blue economy lakini zaidi kwenye zao hili la mwani, bado hatujaweka mikakati zaidi ya mwani kuwa na thamani zaidi. Wakulima wengi wanalalamika, mwani unanunuliwa, lakini thamani ya mwani ni ndogo sana kwa wakulima wetu. Kwa hiyo niiombe sana Wizara kwa sasa hivi tuweke mikakati zao letu la mwani liweze kuwa na thamani ili mkulima aweze kufurahia kama mazao mengine ya korosho, ufuta na mazao mengine mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, niwashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)