Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hoja ya mpango iliyopo mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Kitila Mkumbo, Waziri wa Uwekezaji, lakini bila kuwa na umuhimu sana ninampongeza Mheshimiwa Waziri William Wanging’ombe Lukuvi, kwa kweli nasema Mwenyezi Mungu azidi kuwalinda na azidi kuwabariki na niliku-miss sana Mheshimiwa Lukuvi, lakini leo kwa uwepo wako hapo nimefarijika sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu nitazungumzia maeneo matatu. Eneo la kwanza ni maendeleo katika mikoa kimkakati lakini nitauzungumzia kwanza Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi katika Majimbo Nane ya ukoloni ilikuwa ni Jimbo mojawapo, walilolitambua kama ni Jimbo la maendeleo. Hivyo katika Majimbo Nane - Lindi ilikuwa ni Makao Makuu ya Southern Province ikiwemo Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Mtwara. Leo tunapoizungumzia Lindi ni Mkoa maskini kwa vile haikutengenezewa miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mikoa 13 ambayo tulikuwa tunasema ni Mikoa maskini Tanzania ikiwemo Dodoma, miundombinu iliyopelekwa Dodoma imeifanya Dodoma kuonekana ni mkoa tajiri, sasa niulize kwa nini Lindi wameiacha? Imeachwa kwa makusudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi tulikuwa na airport, ile airport ilikuwa ni ya pili katika Afrika. Ilikuwa ndege British Airways, ikitoka London inatua Alexandria, ikitoka Alexandria inatua Lindi chini ya KAR halafu inakwenda South Afrika, Johannesburg. Jiulize je, airport ya Lindi unaiongeleaje katika mfumo wa dunia, haimo. Mkoa wa Lindi katika bandari ambazo zilikuwa zinafanyakazi mojawapo ni Bandari ya Lindi, lakini jiulize leo unaiona wapi Bandari ya Lindi? Haipo, haionekani! Viwanda vyote havionekani, vimeingia katika uwekezaji wamevifunga. Lakini inasikitisha kuona ni Manispaa maskini, lakini ina uwezo mkubwa wa kuzalisha. Hivyo, naomba Waziri wa Fedha ambaye ni balozi wa watu wenye ulemavu iangalie Lindi kwa umakini, isiwe mikoa mingine inakimbia mingine inakuwa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 14 Septemba, Mheshimiwa Rais alikuwa Lindi, kwa kweli alihuzunika. Alifarijika kwa sababu mbili. Moja, alikutana na watu wa Lindi ambao walimpokea kwa umahiri sana. Katika mikoa ambayo Mheshimiwa Rais katika utembezi wake na kuzunguka kwake, Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Lindi ulivunja rekodi kwa watu kumkubali. Alitoa kauli moja, nina deni na Mkoa wa Lindi. Katika msafara ule Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitembea na Mawaziri, niliwaona Mheshimiwa Waziri Bashungwa, Waziri wa Kilimo na Waziri wa Uchukuzi na hizi hoja wakati zinaletwa pale walikuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpongeze Waziri Bashungwa. Baada ya kuingia mafuriko alikaa site na alihakikisha barabara zile zinapitika, Mwenyezi Mungu akulinde zaidi, hii ni mara ya pili nampongeza Mheshimiwa Bashungwa. Alitoa ahadi kwa wanawake wale waliowalisha chakula pale Somanga kwamba utawaletea majiko ya gesi, mimi nipo tayari kuyapokea majiko ya gesi nikawagawie Liwale na Somanga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa nendeni mkaiangalie Bandari ya Lindi, naomba Kamati kama Mungu atawajalia waende Lindi katika kikao kinachofuatia. Waone bandari ile, haina miundombinu ya aina yoyote. Leo Nchi ya Comoro imeamua kuja kuwekeza katika Bandari ya Lindi kwa kutumia wharfage, majahazi na kila kitu, wanaweka wapi mizigo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tulikuwa tunasikia hela zinatengwa, zinaenda wapi? Nikitoka katika Bunge hili, kwa kumuunga Mheshimiwa Rais, mimi nipo tayari kwenda Lindi, lakini naomba niende Lindi na Waziri wa Uchukuzi na timu yake yote kuanzia Katibu Mkuu, Meneja wa Bandari, Mkurugenzi Mkuu wa Bandari tukakae Lindi tuhakikishe Lindi ile yenye maendeleo inawezekana. Inafikia mahali unajiuliza kwa nini Lindi imesimama, lakini imesimamishwa mikoa mingine imepelekwa mbele na imepewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Bashungwa, umepambana na kwa kweli Serikali imepeleka bilioni 140 kwa ajili ya kuhakikisha zile barabara ambazo zilikufa zinafufuka, lakini leo mvua ikinyesha kuanzia mwezi ujao Liwale haipitiki, Nachingwea haipitiki, inasikitisha sana. Haiwezekani mikoa ambayo inazalisha mazao ya fedha za kigeni ikiwemo korosho na ufuta inaongoza ufuta katika Afrika lakini leo kajiulize, mtu kutoka Liwale anautoaje ufuta wake kuuleta Lindi, inakuwa ni tatizo. Hivyo tukae kwa pamoja, hii nchi ni ya sungura wa wote, tuweze kuisimamia Lindi na iweze kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inatia aibu kuiona Lindi ambayo ina uchumi katika upande wa madini leo imekuwa ya pili kwa madini Tanzania, nenda kajiulize madini yale yanafanya nini? Hakuna barabara, hakuna miundombinu, kitu ambacho ni aibu. Leo ukimwambia Waziri aende Liwale atakwambia kwa mwaka mmoja naenda mara moja kwa vile hakupitiki, lakini jiulize Liwale ambayo inadhalilishwa leo alitoka Waziri Mkuu wa kwanza Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa, hajaenziwa mpaka leo! Sitakubali, kama mwezi huu hawatakwenda watu hawa kwenda kuisimamia.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango mzuri sana. Hongera sana na Lindi itafanikiwa usiwe na hofu.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja, lakini nikiondoka na Mawaziri wa Uchukuzi na timu yake ya Bandari tuhakikishe Bandari ya Lindi na airport ya Lindi inafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana. (Makofi)