Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu. Pia ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2025/2026. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, vilevile ninampongeza Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Mpango. Vilevile niungane na wote waliopongeza kwa kuanzisha Wizara hii ya Mipango na kuwaweka watu makini ambao kwa kweli tumeona mipango yetu mingi imeanza kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na sekta ya maji. Maji ni uhai, kila mtu anahitaji maji, viumbe vinahitaji maji, kilimo kinahitaji maji. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sera yake ya kumtua mwanamke ndoo kichwani, kwa kweli tunampongeza sana, tunajua kwamba toka akiwa Makamu wa Rais hii ilikuwa ni ndoto yake kwamba wanawake sasa tutuliwe ndoo kichwani na hii ni heshima kwa sisi wanawake wote nchi nzima kwamba, Mama amekwenda kugusa vitu ambavyo vinamjengea heshima mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yamefanya hata ndoa zetu zimeanza kuimarika kwa kiasi kikubwa, pia maji yamefanya mwanamke sasa hata kuweza kufanya kazi za uzalishaji kwa sababu muda mwingi sana alikuwa akitumia kutafuta maji. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, wetu na apewe maua yake mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze sana Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso ambaye ametimiza ndoto ya mama yetu na tumeona kwa kweli akifanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba mwanamke anatuliwa ndoo kichwani kwa miradi mingi ambayo ipo katika Majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mpango maalum kuhakikisha kwamba wananchi wanapatiwa maji safi na salama na lengo la dira ya miaka mitano inasema kwamba upatikanaji wa maji unatakiwa 85% vijijini na 90% mijini lakini taarifa ya mwaka 2023/2024 inaonesha kwamba mpaka sasa hivi upatikanaji wa maji umefikia 70% vijijini na 90% mijini. Lengo hili nafikiri inatakiwa sasa miaka mitano ni mwakani mwaka 2025 tunatakiwa tufikie hilo lengo lakini zipo changamoto nyingi sana ambazo zinasababisha lengo hili pengine ikawa shida lakini tunaomba kwa sababu uhalisia ukiangalia hizi asilimia unakuta bado akinamama wanahangaika na maji hasa huko vijijini, kwa hiyo ninaomba sasa, hizi changamoto angalau zifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, ni fedha za Mfuko wa Maji, kutowasilishwa katika Mfuko huo kwa sheria inayofuata. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, nakumbuka kwamba tulimwita kwenye Kamati yetu na ninaipongeza Kamati yetu ya Maji na Mazingira. Kwa kweli mara nyingi sana imekuwa ikihakikisha kwamba suala hili linafanyika vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, alikuja na tukaweka mkakati kuhakikisha sasa huu mfuko unafanya vizuri zaidi ili pesa zipatikane nyingi katika hii Wizara ili miradi iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kumekuwepo na changamoto kubwa ya madeni ya wazabuni na wakandarasi kutolipwa kwa wakati na kusababisha hiyo miradi kucheleweshwa. Sasa gharama inaongezeka kwa sababu miradi inakuwa inachelewa kukamilika kwa wakati. Pia, kunakuwa na riba kubwa sana ya madeni. Kwa hiyo, naomba hili pia lichukuliwe kwa uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumekuwa na mitambo. Tunaishukuru sana Serikali yetu, wametuletea mitambo karibu kila mkoa. Hii mitambo ya maji ipo, lakini tatizo kubwa sasa ni ukosefu wa fedha, ili hii mitambo iweze kusaidia uchimbaji wa visima sehemu ambapo hakuna miradi ya maji. Kwa hiyo, naomba sana hizi changamoto ziangaliwe kwa umakini mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna changamoto kubwa ambapo kumekuwa na madeni ya huduma za taasisi za Serikali. Tumeona ripoti ya 2023/2024, wanadaiwa karibu shilingi bilioni 45. Hili jambo kwa kweli tumelizungumzia sana kama Kamati na kama Waheshimiwa Wabunge kwamba, kwa nini taasisi za Serikali zinadaiwa wakati zinatakiwa ziilipe Wizara ya Maji? Sasa mpango mkakati ni nini? Je, sasa wanazilipaje ili hizi pesa ziende kusaidia miradi ya maji ili sasa mwanamke kweli atuliwe ndoo ya maji kichwani na Mheshimiwa Rais wetu aweze kuifikia ndoto yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona pia kuna gharama kubwa sana ya umeme kwa ajili ya kuendesha huduma ya mamlaka zetu nchini. Sasa tulikuwa tunaomba, kwa sababu tulivyozitembelea mamlaka nyingine zinalipa umeme karibu shilingi bilioni mbili kwa mwezi. Inasababisha unit ya maji inapanda sana kiasi kwamba gharama ya maji inakuwa kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu. Huu Mpango wa Taifa wa Maendeleo ushughulikie changamoto zifuatazo: kwanza, kulipa madeni kwa wakandarasi na kuwasilisha fedha za Mfuko wa Maji zinazokusanywa kwenye chanzo. Pia, matumizi ya mitambo basi yatengewe fedha maalum ili visima vingi viweze kuchimbwa na mabwawa mengi yaweze kuchimbwa. Kuwe na mpango mkakati ili taasisi za Serikali zilipe madeni yake. Pia, Serikali ione uwezekano wa kupunguza gharama za umeme ili kuwezesha uendeshaji kuwa rahisi zaidi. Kwa sababu tulienda kwenye vijiji, tumekuta units za vijijini ni kubwa kuliko mijini. Kwa hiyo watu wanashindwa kuunganisha maji vijijini kwa sababu bei ya gharama ya uendeshaji wa miradi ni kubwa sana. Kwa hiyo, ninaomba hili liangaliwe ili watu wengi huko vijijini waweze kuunganisha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifanyike pia tathmini ya upatikanaji wa maji nchini kuanzia ngazi ya vijiji, kata, tarafa, wilaya na mkoa ili kupata hali halisi, kwa sababu tumeona uhalisia hauoneshi jinsi ambavyo tunapata hizo tathmini, lakini ukienda huko chini unakuta kwamba, bado kuna changamoto kubwa sana ya maji pamoja na tunapata asilimia inakuwa kubwa. Ili tathmini itoe majibu sahihi itakayosema, kuandaa mpango ili miundombinu ya maji iwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi huwa naangalia REA, unaona kwamba sasa hivi tuko kwenye vijiji halafu baadaye tunaenda sasa kwenye vitongoji. Sasa hata kwenye maji iwepo tathmini kama hiyo, kwamba, je, vijiji vingapi vimeshapata maji? Sasa bado vitongoji vingapi kila eneo? Hii itatusaidia na sisi kuwa na tathmini kwamba sehemu ambapo hakuna maji sasa ni kitongoji fulani ambacho tunapambana miundombinu iende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hivi visima vinachimbwa, lakini hamna usambazaji lakini miundombinu haiwekwi miundombinu ili watu wapate maji. Pia, tumeona vile vituo vya maji vinakuwa mbali sana kiasi kwamba wanawake bado wanabeba ndoo kichwani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Maji, tunaomba sana hilo liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni kuhusiana na Liganga na Mchuchuma... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)