Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kabla sijachangia Mpango, ninaomba niweze kuomba mambo matano. Moja ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, walipe wakandarasi. Watu ambao wamehudumia Serikali wengi wanapata taabu na wanafilisika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba sana waanze kufikiria sasa kuanza kujenga treni ya mwendokasi kuelekea Kilimanjaro. Itoke Dar es Salaam kwenda Moshi – Arusha. Pia, naomba sasa Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, wanafahamu kwamba tumetengewa shilingi bilioni 11.6 kwa ajili ya Ujenzi wa Soko la Kwa Sadala. Tafadhalini sana, tunaomba hii fedha ili soko lianze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia hili suala la Liganga na Mchuchuma, tangu nasoma shule ya msingi ninalisikia linazungumzwa. Ifike mahali liishe na sisi watu wa Hai tuliomba na wakasema wataweka kwenye mpango kwamba kile kiwanda cha mashine tools kiwe kinapata material kutoka huko. Kwa hiyo, jambo hili lifike mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwenye maombi yangu, wapokee utaratibu ambao tumewashauri hapa kwenda kwenye cashless. Haya mambo ya kutumia pesa kwa maana ya makaratasi, yanatuchelewesha. Tukubali na tupokee ushauri huo. Baada ya kusema hayo, sasa nichangie mpango ulioko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vipaumbele ambavyo wameviweka ni kwamba wamesema, ukurasa ule wa 13, “kuimarika kwa upatikanaji wa usalama wa chakula.” Ndiyo ninataka nichangie hapa. Wenzangu wengi wamezungumza, tunaposema upatikanaji wa usalama wa chakula ni nini? Tumeona mipango ambayo Serikali wameweka mbele yetu na tumeona maoni ya Watanzania wengi wakati wanachangia mawazo yao kwenye Maono ya Mpango ya Miaka 50 ijayo. Wengi, takribani watu 1,170,000 walioshiriki wamesema kipaumbele cha nchi hii kiwe ni kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ifike mahali tutoke kwenye maneno, twende kwenye vitendo. Tunaposema kilimo, tuone output ya kilimo, tuone tunazalisha na tunauza. Tusiongee sana, tumeshaongea na muda umefika sasa wa kulima kilimo ambacho kitakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri, tungeweza kuigawa nchi yetu katika kanda mbalimbali kulingana na aina ya ardhi na upatikanaji wa maji. Kwa mfano, tukasema Kanda ya Ziwa tulime zao hili, kwenye mkoa huu tulime aina ya zao moja lakini kwenye kilimo hicho, tuongezee thamani mazao. Kama tunasema tunalima nanasi, basi tuweke mashamba ya nanasi, tuweke umwagiliaji wa kutosha na tuweke viwanda vya kutengeneza juisi ya nanasi ili mtu alime afikishe bidhaa mwisho. Tuhangaike kutafuta masoko huko duniani. Kuliko hivi tunavyolima kidogo kidogo halafu hatuna umahiri kwenye zao fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tukisema Ukanda huu wa Kaskazini walime mahindi na maharage. Ni vizuri ifike mahali viongozi wetu walioko kwenye mikoa na wilaya ukimwambia Mkoa wa Kilimanjaro, wewe tunakupa target ya tani bilioni kadhaa za mahindi. Usipofikia hicho ndiyo kipimo chako. Ukifanya vizuri maana yake umefanikiwa na ukishindwa umeshindwa, ndiyo kipimo kiwe hivyo. Kwa hiyo, kwa kufanya hivi tutajikuta nchi yetu ina chakula cha kujitosheleza na tutaweza kuuza nje ya nchi kwa kuongezea thamani mazao tuliyonayo na ni sambamba na kujenga viwanda na hili linawezekana. Tukubaliane kwamba, kama tunaweka zao hili, kila zao ambalo tutapanga kulilima liwe na kiwanda chake cha kuongeza thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo wamezungumza kwenye mpango kama kipaumbele cha tatu, wamesema kuongezeka kwa ushiriki wa Sekta Binafsi katika shughuli za uwekezaji wa biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema Sekta Binafsi iingie, tunaiandalia mazingira gani hii Sekta Binafsi? Leo ukiangalia sheria zetu za kodi, siyo rafiki hata kidogo. Ninasema bado zina hangover ya kikoloni, kwa sababu wale walioko TRA wanamwona mfanyabiashara ni adui. Sasa hili siyo sawa. Tufike mahali tu-regulate sheria zetu za kodi, ziwe rafiki. Yule anayeenda ku-charge kodi pale aone kwamba kuna mtu kawekeza fedha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunapofanya auditing, mtu anapeleka ripoti yake TRA inawekwa mezani, mtu anazikusanya zaidi ya miaka minne hazijafanyiwa kazi, lakini angeenda mwaka huo akapewa ripoti yake akaambiwa ulikosea hapa, inamsaidia mwakani kubadilika. Pia wale watumishi walioko TRA wakumbushwe kwamba wana wajibu wa kulea wafanyabiashara. Siyo hivyo wanavyoishi, wanataka kukamua ng’ombe, lakini kumlisha ng’ombe hawataki, siyo shughuli yao na inafika mahali wanaona ni fahari kufunga biashara za wafanyabiashara. Ni fahari kwao kufilisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali hiyo attitude ibadilike, kwamba ikifika meneja wa mkoa kuna mfanyabiashara amefilisika, wewe meneja tuku-charge kwamba kwa nini huyu amefilisika? Hukumshauri vizuri. Kwa hiyo, hilo na lenyewe lionekane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema uwekezaji, pia naomba nizungumze jambo moja. Tulinde wawekezaji na wafanyabiashara wetu wa ndani. Pamoja na kwamba mimi ni muumini sana wa diplomasia; hivi jamani kinachoendelea pale Kariakoo mnakiona? Wale wageni waliojaa pale, anazalisha kule kwao China, anakuja na kontena, anaenda analiweka ndani halafu anachukua yeye mwenyewe anaenda kupanga pale anauza. Mnategemea ushindani wa biashara sisi Watanzania tutaweza kushindana nao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, tunatakiwa kuendelea na mahusiano mazuri na wenzetu, lakini ni lazima tulinde watu wetu. Ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wafanye research kinachoendelea pale Kariakoo. Vinginevyo wale watu watakimbia pale; watashindwa kufanya biashara na wafanyabiashara wetu watafilisika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kusema na niliuliza swali juzi hapa kuhusiana na CSR kwenye Mlima Kilimanjaro. Sikatai Mlima Kilimanjaro ni wa kwetu wote, lakini maeneo mengine kwa mfano wanaofanya biashara ya dhahabu utakuta wako ndani ya maeneo yetu lakini wanapata CSR. Pia, sisi Mkoa wa Kilimanjaro siyo mbaya wakafikiria namna ya kutengeneza sheria ili na sisi tupate CSR kutokana na maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwa Mkoa kama Kilimanjaro na wilaya ambazo maeneo yao ni madogo sana, sisi Wilaya ya Hai ardhi ni kama imekwisha. Maeneo mengi yako kwenye vyama vya ushirika. Hebu niombe, tunafahamu kipaumbele kwenye vyama vya ushirika ni kulima zao la kahawa, lakini bado mashamba yale ni rafiki kwenye utalii. Naomba sana Mheshimiwa wa Mipango atembelee Wilaya ya Hai, aone yale mashamba; yanafaa sana kwenye uwekezaji wa hoteli za kitalii ili tubadilishe mfumo wa uchumi wetu kwa sababu hatuna sehemu nyingine ya kwenda kulima. Lazima tutafute alternative ya kufanya biashara ambayo itaongeza pato la watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo wameliweka hapa zuri kabisa ni kwamba, kuwa na nidhamu katika utekelezaji wa mipango. Nimefurahia sana jambo hili. Nidhamu ni nini? Ni pamoja na ile taarifa ya mashirika mlisikia kilichotokea pale, wakuu wa taasisi wale. Ninaomba, ifike mahali hizi kazi tupeane kulingana na uwezo mtu anavyoweza kufanya kazi. Kama wamekiweka hapa kipaumbele hiki, maana yake ndiyo kinaenda kusimamia mipango mingine, tupate watu wenye uwezo mzuri, washindanishwe wasipewe tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai ziko nafasi za uteuzi, lakini zile za utendaji mtu aombe, washindanishwe, tupime uwezo wake na awe anafanyiwa review kila mwaka kulingana na uwezo wa kazi yake, ndipo mipango hii itaweza kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya katika nchi yetu na wananchi wa Hai wameniambia niseme ahsante sana kwa Mheshimiwa Rais kwa miradi kedekede aliyoleta ndani ya Jimbo la Hai. (Makofi)