Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuweza kuniona. Awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anavyoiendesha nchi yetu na namna anavyojenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mipango kwa namna ambavyo nao wanavyofanya kazi zao vizuri sana za kuweza kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika upande wa mchakato wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa na kuangalia malengo yake. Nitajikita kuhusiana na Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2025/2026 na hasa kuangalia dhima yake inayozungumzia suala la kujenga uchumi shindani na viwanda pamoja na maendeleo ya watu. Katika dhima hii ya uchumi, hasa kwenye uchumi wa maendeleo ya watu pamoja na mchakato wake, nitaangalia mambo matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, nitaangalia suala la elimu. Maendeleo ya watu ni lazima kwanza kitu cha kwanza tuangalie suala la elimu. Bila ya elimu maana yake hayo maendeleo juu ya watu maana yake itakuwa bado, hatutaweza kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la elimu ya watu, maana yake ni kuwaondosha katika mindset zao na kuzileta katika mindset za kimaendeleo. Suala la pili, nitaangalia suala la matarajio ya namna ya watu kuweza kuishi ambalo nalo limo katika mpango ambao upo na jambo la tatu ni pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija na mpango uliowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Mipango, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, ni mpango ambao nitasema kwamba umeakisi haja kubwa sana na nitasema kwamba ni mpango ambao umejitosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, nije katika ile Falsafa ya Mwalimu Nyerere ambayo alizungumza maneno hasa katika masuala ya maendeleo ya watu. Alizungumza hivi, “Maendeleo ni watu lakini siyo kitu.” Maendeleo ni watu siyo vitu. Ili watu waweze kupata maendeleo, lazima watu waweze kujitegemea. Ili watu waweze kupata maendeleo ni lazima watu kupambana na umaskini. Ili watu waweze kupata maendeleo ni lazima kuondosha ujinga pamoja na maradhi.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo Falsafa ya Mwalimu Nyerere ambayo alizungumza na alikuwa na mantiki kubwa sana alivyokuwa anazungumza maneno hayo, kwamba, maendeleo ni watu, hasa katika kupunguza umaskini, kuondosha ujinga, maradhi na masuala mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo, katika huu mpango tulionao, maana yake ni dhahiri kwamba tunajadili suala la kujitegemea. Tunajadili suala la kupambana na umasikini na tunajadili suala la kuondoa ujinga pamoja na maradhi. Hayo ndiyo mambo tunayojadili katika huu mpango. Pamoja na dhima tuliyokuwa nayo ya uchumi shindani pamoja na viwanda, hayo yote yanaakisi maneno ya Mheshimiwa Marehemu Mzee wetu, Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la kujitegemea. Suala la kujitegemea, ukiliangalia hasa ni suala ambalo ni mtambuka sana na ni suala pana, ambapo tukiangalia katika suala la kujitegemea, maana yake tuangalie suala la rasilimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kama Tanzania, kama ni nchi maana yake tunazo rasilimali za kutosha katika kujenga uchumi wa nchi yetu. Ukiangalia ardhi tunayo na ndani ya ardhi huko kunapatikana maji, madini na ndani ya ardhi humo tunafanya shughuli zetu zote ambazo hizo kama ni utajiri kama ni nchi maana yake tunayo rasilimali ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija katika suala la rasilimali watu, maana yake watu ndiyo sisi. Maana yake ni kujaribu tu kuwapa elimu watu wote kuondokana na ujinga na kupata elimu yenye tija kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweza kufika katika hatua ya malengo tunayoyakusudia na maendeleo yenye kuleta tija, kuna mambo ambayo ni lazima tuyaangalie katika hali ya upana mkubwa sana. Suala kubwa la kuweza kuliangalia ni suala la elimu. Bila kuangalia elimu, maana yake mipango yetu yote tutakuwa hatuwezi tukafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala kubwa sana katika maisha yetu na katika mazingira yetu, bila kuwajengea watu mazingira ya elimu na elimu yenyewe, maana yake iwe ni elimu yenye tija, ya ujuzi na ya kujenga maarifa. Tukiwa na elimu ya kujenga ujuzi, tukiwa na elimu yenye kujenga maarifa maana yake hapo tunaweza tukatengeneza mfumo wetu mzuri wa maendeleo yetu ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo limezungumzwa na watu wengi sana, ili mpango wetu uweze kukamilika tuangalie suala la kilimo, kilimo maana yake ukitizama katika hali ya nchi yetu asilimia kubwa ya watu ambao wanaishi katika nchi ya Tanzania maana yake wanategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika mipango yetu maana yake tuangalie sana suala la kilimo, lakini kilimo chenyewe maana yake kilimo kilichokuwa bora, kilimo ambacho chenye kuleta tija. Ili kuweza kuwa na kilimo kilichokuwa bora na kilimo chenye kuleta tija maana yake ni lazima kwamba tuwe na miundombinu ambayo ni mizuri, tuwe na wataalam ambao watakaoweza kuimarisha kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee walikuwa wanatuambia kwamba kilimo ni uti wa mgongo tukiangalia kweli kwamba kilimo ni uti wa mgongo bila kuangalia suala la kilimo kama nchi yetu maana yake watu tutaweza kuwaacha na njaa. Ila tukiweza kulima maana yake tutakuwa tuna uwezo wa kuweza kuondosha njaa, tutaweza kuondosha, tutakuwa tuna uwezo wa kuweza kupata kipato cha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala lingine katika kuondosha maradhi, maana yake ni lazima kwamba tujenge hospitali ambazo zimeshajengwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kila mahali, lakini tatizo letu ni moja. Maana yake tatizo letu ni kwamba tunahitaji kuwa na wataalam ambao watakuwa ni wataalam bobezi, ambao wataweza kutibu maradhi ambayo yataweza kuwaondosha maradhi watu wetu kama kuondosha umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nije katika suala la tatu hasa lililopo katika mpango wa maendeleo; nije kwenye suala la ufuatiliaji...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, kengele ya pili.

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)