Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi uliyonipa ili nami niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wetu wa mwaka 2025/2026. Kabla sijaanza mchango wangu niruhusu niwapongeze watu wawili; moja ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuunda Tume ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi na hasa baada ya sisi hapa Bungeni kubishana muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini matokeo ya hii tume yataleta mageuzi makubwa sana katika ukusanyaji wa mapato katika nchi yetu. Hongera sana Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili nami kwa kuchukulia umuhimu wa jambo hilo pamoja na kwamba nilikuwa mapumzikoni kule tayari nimeshaandaa kurasa 50 ambazo nitazipeleka kwenye tume ambazo zimezungumzia maeneo mbalimbali ya namna ambavyo nchi yetu inapoteza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa pili, ninataka nimpongeze ni Mheshimiwa Donald Trump, Rais wa Marekani, ninampongeza kwa ushindi mkubwa na kwa kuaminiwa tena na wananchi wa Marekani hongera zake aendelee kuongoza nchi hiyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Kisesa kwa kuendelea kunivumilia hata wakati wa juakali lakini wameendelea kuwa pamoja nami, hongereni sana wananchi wangu. Nitahakikisha kwamba kwa nguvu zote na kipaji chote nilichopewa na Mwenyezi Mungu tunatekeleza ile azma yetu ya kwamba hakuna kupumzika mpaka maendeleo ya kweli yapatikane Jimbo la Kisesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa nichangie mpango na nianze kwenye utekelezaji, nipitie kidogo eneo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Taarifa ya Mpango hapa inaonyesha kwamba mradi wetu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao utazalisha megawatt 2,115 tayari sasa hivi uzalishaji umefikia megawatt 740 na tumefikia 99.21%, lakini hatuambiwi sasa mpango wetu huu unakamilika lini ili kuzipata zile megawatt zote 2,115. Tuliwaahidi wananchi kwamba umeme huu ni umeme wa bei nafuu, hatujaambiwa katika mpango huu unafuu wa umeme kwa wananchi kutokana mradi wetu huu mkubwa tuliowaahidi kwamba tutashusha bei za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, umeme wetu tutawauzia majirani zetu, leo hii katika mpango huu nchi ngapi ambazo tayari tumeshaingia nazo mkataba wa kuziuzia umeme na umeme wetu unaenda kushuka bei kwa kiasi gani? Ili wananchi wetu wapate umeme kwa bei nafuu, wawekezaji wetu waweze kufaidi uzalishaji ndani ya eneo ambalo lina uzalishaji wa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili la utekelezaji wa Mradi ni LNG, mradi huu tunaambiwa tu kwamba mazungumzo yanaendelea sasa miaka imeenda sana mazungumzo yanaendelea na utaratibu wa kawaida kwa mujibu wa Sheria ya Natural Resource pamoja na alterity zinataka hii mikataba iingie hapa Bungeni. Sasa huko wanapoendelea na mazungumzo wanaendelea kwa muda gani? Kwa sababu miradi hii, kama walivyosema wenzangu inahitajika kutekelezwa kwa haraka ili tuweze kunufaika na miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la mkataba wa usafirishaji mizigo wa kuchangia makasha kwa wasafirishaji wa mizigo tofauti tofauti yaani imported loose cab. Hapa katikati Sheria ya Usafirishaji wa Mizigo hiyo ilibadilika kanuni za usafirishaji wa mizigo hii ilibadilika ikafika mahali kwamba msafirishaji wa mizigo yaani consolidator anasafirisha mizigo majina ya nyaraka zote yanaandikwa kwa jina lake yaani bill of landing, commercial invoices, parking list, declaration form, TPA documents, payment list zote hizi ziliandikwa kwa majina yao kwenye usafirishaji kule anaposafirisha mzigo, lakini tukapata matatizo makubwa sana ya wafanyabishara wengi kukosa nyaraka za ulipaji wa kodi. Kwa sababu majina kule yameandikwa kwa jina la msafirishaji na hapa anakuja kuuza anasafirisha kwa majina yake na anakuja kulipa kodi yeye na ana-declare VAT input tax yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku wananchi wetu wanashindwa kuuza bidhaa kwa kutoa risiti, wananchi wetu wanakuwa hawana nyaraka zozote za kufanya malipo ya kodi na wananchi wetu na wafanyabiashara wetu wakashindwa hata kutumia EFD na wananchi wetu wakawa na matatizo makubwa sana, migomo ilitokea mingi sana kule Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumanne, tarehe 5 Novemba, 2024 hapa Serikali imekuja kusema sasa wafanyabiashara, nyaraka zao zitaandikwa kwa majina yao, lakini hapa tumepotezewa fedha nyingi sana; sasa kwa sababu tumepoteza fedha nyingi hizi fedha zetu tunazi-recover vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nami nashauri kwa sababu ili kampuni la OPPO Agency Company Limited kwa muda wa miaka mitano limefanya hii business na kuna wafanyabiashara wengi ambao wamei-load mizigo, lakini inapofika huku kwenye ku-clear mizigo nyaraka zao za usafirishaji wa mizigo hazionekani, kwa maana ya kwamba mizigo hiyo haikuingizwa ili kukwepa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ufanyike ukaguzi wa kiuchunguzi yaani forensic auditing ya muda wa miaka mitano kulichunguza kampuni la Oppo Agencies Limited katika kipindi hicho cha miaka mitano na kubaini kodi iliyopotea na kama tutabaini kodi iliyopotea, kampuni iilipe Serikali hiyo hasara itakayokuwa imetengenezwa ndani ya miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo lingine hapa ni suala la Mkataba wa DP World, suala la mkataba wa DP World tumeambiwa vizuri hapa, lakini nataka kusema tulikubaliana kwamba Mikataba ya HGAs iletwe hapa Bungeni. Mheshimiwa Waziri hapa anaeleza mwekezaji wa DP World atawekeza dola za Marekani milioni 250 sawasawa na bilioni 687 kama sikosei bilioni kwa miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari mwekezaji huyo ameshaenda anakusanya kodi sasa na huo uwekezaji wake atawekeza kwa muda wa miaka mitano. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikubaliana hapa Bungeni kwamba mikataba hii ya HGAs yote mitatu italetwa kwenye hili Bunge ili tuweze kujua nini kilichokubalika ndani ya mikataba hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi Sheria yetu ya Natural Resources inasema kifungu 12 kwamba mikataba yote ya rasilimali lazima iletwe hapa Bungeni. Ninaendelea kuuliza hivi imeshindikana nini kuletwa mikataba ya Bandari ya Dar es Salaam tuliyoingia mkataba na DP World hapa Bungeni. Nani aliyeenda kukubali kwamba sisi tunakubali uwekezaji wa bilioni 687, nani aliyekubali kwamba sisi tumekubali ratio ya kugawana mapato na DP World kwa ratio ya 40 kwa 60 nani aliyekubali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mkataba....

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina kengele ya pili.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo dakika moja.