Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi nami kuweza kutoa mchango wangu kwenye majadiliano yanayoendelea. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote. Pili kwa kuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ninaunga mkono maoni yetu yote ambayo yaliwasilishwa na kwa umahiri na Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Bajeti Mheshimiwa Oran Njeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Waziri Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Mipango Profesa Mkumbo, kwa kazi nzuri pamoja na watendaji wao wote na namna ambavyo alitupa ushirikiano wa karibu sana kwenye Kamati yetu ya Bajeti wakati tunafanya majadiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Profesa Mkumbo katika Taarifa yake amewasilisha Mpango wa Maendeleo 2025/2026, lakini ninataka niungane naye kwa namna ambavyo ameelezea kwa ufasaha mafanikio yaliyopatikana ndani ya miezi sita baada ya Serikali kukabidhi shughuli za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa Kampuni ya DP World Dar es Salaam. Kwa nini ninaungana naye ni kwa namna ambavyo kama yeye mwenyewe anavyosema, ni namna Mheshimiwa Rais wetu alivyokuwa shupavu, jasiri, mstaamilivu na sote ni mashuhuda wa namna hata Bunge hili lilidharauliwa baada ya kupitisha ule mkataba hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeze Mheshimiwa Spika wetu Mheshimiwa Dkt. Tulia, ninakupongeza na wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa namna ambavyo mmetuongoza katika mjadala ule lakini nadhani katika yale maneno yanayosemwa kwamba wanaokutukana siku moja watakusalimia kwa heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaamini wale ambao walikuwa wamempinga tena kwa lugha ya kebehi watamsalimia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wa heshima kubwa, baada ya kuona mafanikio haya tu ya muda mfupi na tuna imani yale ambayo faida zote zilizoelezwa za mkataba huu wa DP World na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya uendeshaji wa Bandari Dar es Salaam na siyo bandari zote, siyo mkataba wa milele yote hayo yamejidhihirisha, ni kweli kwenye ukweli uongo hujitenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda kuipongeza Serikali chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya namna ambavyo imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati, lakini kwenye mradi huu wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa kuwa natoka kwenye Mkoa wa Pwani ambapo mradi huu unajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze kwa dhati Serikali kwa kuingiza megawatt 750, lakini nina shukrani za maeneo ya visiwa ambayo hatukuwahi kudhani kama utapelekwa umeme wa gridi ya Taifa, nina shukrani za kutoka visiwa vya Wilaya ya Kibiti, Mbuchi, Maparoni, Kiongoroni na Visiwa vya Wilaya ya Mafia umefika umeme wa Grid ya Taifa kwa mara ya kwanza jambo ambalo limekuwa historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme umepitishwa kwenye majaruba ya maji, kwenye bahari, kwenye maingiliano ya delta na Bahari ya Hindi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa historia hii, lakini pia na kwa miundombinu. Sasa hivi visiwa hivyo vinafikika na miundombinu ya barabara yamejengwa madaraja ambayo hayakuwahi kufikiriwa ndani ya miaka 60 ya uhuru. Ni wazi kwamba kazi nzuri imefanywa, lakini kwa kuwa kazi hizo zinafanyika kutokana na makusanyo ya mapato, tunajadili mapendekezo hapa ambayo natarajiwa kukusanya trilioni 55. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati pia tumefanya tathmini ya utekelezaji wa robo ya kwanza ya bajeti ya mwaka huu 2024/2025. Hapa ninataka niipongeze kwa dhati TRA kwa kazi nzuri inayoendelea kufanywa, nimpongeze Kamishna mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Yusuph Mwenda, ninampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, lakini pia ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo tumeona kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha robo ya kwanza wamekusanya zaidi ya trilioni 7.7 na 105%, lakini hatua zinazochukuliwa na Mamlaka ya Mapato sasa hivi tumemwona Kamishna akifanya ziara mikoa mbalimbali, akikutana na wafanyabiashara, wafanyakazi na wadau mbalimbali. Amefanya ziara kwenye maeneo ya mipaka yetu, amefanya ziara kwenye maeneo ya bandari zetu, amefanya kikao na TIC pamoja na wawekezaji wa nje waliokuwepo hapa nchini. Hatua zote zinaonekana lengo lake ni kuongeza ukusanyaji wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu katika hili ni kuomba Serikali kwenye bajeti inayokuja 2025/2026 kuona namna ya kuwezesha Mamlaka ya Mapato. Wanajenga mifumo ya ukusanyaji mapato mfano mfumo wa IGAS, mfumo wa TANSIS na mifumo mbalimbali, lakini changamoto kubwa ni namna ya uwezeshaji ili kukamilisha mifumo hii. Niombe Serikali ile bajeti ya bilioni 400 ambayo wamekuwa wakitoa kidogo kidogo kwa ajili ya mamlaka hii ya mapato ikamilishe ile mifumo kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia iwezeshe vitendea kazi magari ya kupambana na wakwepa kodi zile scanner katika maeneo ya mipaka yetu kwa mfano Kamati ya Bajeti tulitembelea Namanga, tumewahi kutembelea sisi mabalozi wa kwetu tumetembelea Holili, tumetembelea Tarakea, lakini pia kupitia ziara ya Kamati ya Bajeti imetembelea Buhigwe tumeona Mkoa wa Kigoma kule mipakani. Kwa hiyo, Serikali ina uwezo kukusanya mapato mengi zaidi kama itaiwezesha TRA. Ombi langu katika hili kwa kuwa kila kitu trilioni 55 tunatarajia, trilioni 38 zitokane na mapato ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya trilioni 38 hizo ambazo ni zaidi ya 70% zaidi ya trilioni 31 zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameonyesha ushujaa na ushupavu na matarajio ya kuwezesha TRA, ameongeza wafanyakazi kwa mara ya kwanza zaidi ya 1,200 mwaka wa fedha 2023/2024 uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuwa akiwezesha hatua ya kuunda kikosi kazi cha kupitia mifumo ya kodi, ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wanakusanya kodi kwa haki bila upendeleo na wote tunalipa kodi, lakini na wale ambao wana vitendo vya kukwepa kodi wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia uimarishaji wa Taasisi za TRAB na TRAT ili kuwezesha wanasikiliza masuala mbalimbali ya kodi lakini pia hata Ofisi ya Msuluhishi wa Kodi iwezeshwe ili kwa pamoja jitihada zote zichangie upatikanaji wa trilioni 55 zinazotarajiwa, lakini hata sasa trilioni hizi 49. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii lakini kiukweli Awamu hii ya Sita, ameupiga mwingi kwenye kukusanya mapato.