Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kunipa nafasi nami ya kutoa mchango wangu katika kujadili suala la mpango. Kabla ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupa afya na uhai na zaidi ya yote nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kulitumikia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wawili, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Mipango kwa kutuonyesha njia ya sisi kutoa michango yetu mizuri kutokana na wasilisho zuri walilofanya pamoja na Wenyeviti wa Kamati walioweka michango mzuri katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuanza na maneno yanayosema kujitawala ni kujitegemea. Taifa lolote ambalo ni tegemezi Taifa hilo linapunguza hadhi na heshima ya uhuru wake. Kwa hiyo, nataka pamoja na yote tunayozungumza tumerudisha Tume ya Mipango kwa sababu tumeona ipo haja ya kufanya hivyo. Kwanza kwa ajili ya kuweka mipango kwa maslahi ya Taifa, lakini pili kuweka vipaumbele vya utekelezaji wa mipango hiyo. Pamoja na kuyafanya yote hayo lazima tuwekee ringfence hili jambo lenyewe la Tume ya Mipango kwamba mipango yetu tukishaipanga tuiheshimu tusiwe na tabia ya kwenda mbele rudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mwingine ukiulizwa unasema hapa tunahitaji political will, mpango ndiyo political will yenyewe tulishaweka mpango tuuheshimu tuufuate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi nyingine mipango mikubwa inakuwa ni sehemu ya Dira ya Taifa na inakaa kwenye Katiba ya Nchi ili mtu yeyote anayekuja, kiongozi yeyote wa nchi anayekuja anaiheshimu, anaifuata kwa sababu haya ni masuala ya kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo la kusema mipango yetu iheshimiwe, jambo lingine ambalo ninataka niliseme ni kwamba, katika kujitawala ni kujitegemea. Mipango yetu ijielekeze katika kupunguza utegemezi wa Taifa letu na ili kufikia dhamira hiyo ya kupunguza utegemezi, yapo mambo ya msingi ya kuyasukuma na kuyapa kipaumbele katika mipango yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, nimepata bahati ya kujifunza sana mambo mengi kwenye Sekta ya Nishati, lakini leo hii tunapozungumza mipango yetu ningezungumza kwa nchi yetu, Mpango wa kwanza ambao ungekuwa kipaumbele kwa Taifa letu, ni kuzalisha gesi asilia kwa wingi na kuisambaza katika nchi yetu yote, ili gesi hii itusaidie kupunguza gharama za kuhitaji mafuta ya nishati kutoka nje ambayo yana msalaba wa kutafuta kitu kinaitwa dola kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo yapo magari yanatumia gesi, yanapanga foleni kutwa nzima kutafuta gesi ambayo inazalishwa nchini haihitaji dola. Kwa hiyo, tukiongeza uzalishaji, na tena sasa hivi nimetembelea kule Madimba wala siyo suala la kuongeza uzalishaji maana wamepunguza uzalishaji kwa 60% kwa sababu mteja wao mkubwa alikuwa ni TANESCO na TANESCO wamepunguza kuchukua gesi baada ya Bwawa la Mwalimu Nyerere kuanza kufanya kazi. Kwa hiyo, kuna gesi nyingi ambayo bado haijatumika imezuiliwa kuzalishwa kwa sababu haina mtumiaji. Tuongeze matumizi ya gesi haya yatatutoa kwenye utegemezi, utumwa wa kutafuta dola, utumwa wa kupatana na wenye kampuni za mafuta kuwanyenyekea utapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni chuma, tuvune chuma ili miradi yote ambayo inahitaji chuma tupate chuma kutoka nchini. Hadithi ya Liganga imekuwa ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi; lakini siyo tu kuongeza maana hata viwanda ambavyo tulitaka vitusaidie katika kukuza uchumi, tumechukua viwanda vingi ambavyo sivyo vinavyo-add value ya mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji, yaani viwanda tulivyovihitaji ni viwanda ambavyo vinaongeza thamani ya mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo hii kuna mzalendo mmoja pale SIDO Kigoma ameweka Kiwanda cha Kukamua Mafuta ya Mawese na kuya-refine kutoa hiyo Korie. Kiwanda kiko pale lakini uzalishaji wa michikichi umekuwa ni mdogo mpaka analazimika kuchukua mafuta kutoka Malaysia ili aje hapo ayasafishe ndiyo auze, kwa hiyo, lazima tuongeze kasi. Mpango wetu lazima useme, tunataka kuondokana na suala la kuagiza mafuta kutoka nje ni nguvu gani tutaiweka kwenye kilimo cha michikichi ili kuondokana na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, alifanya kazi kubwa kweli ya kusukuma michikichi lakini siioni nguvu kubwa ya Serikali kuweka pesa kwenye kilimo cha michikichi, kuwawezesha wananchi walime vizuri, walime ya kutosha ili tuweze kuzalisha mafuta kwa wingi. Kwa hiyo, niwaombe sana lazima tujielekeze katika jambo hili kwa nguvu kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ninasema Serikali yetu inafanya kazi kubwa na nzuri na hakuna habari ya kurudi nyuma katika mambo tuliyofanikiwa. Mambo tuliyofanikiwa ni pamoja na kuboresha bandari zetu, tumeshawapa kazi DP World waendelee kufanya kazi na sisi tunategemea mavuno makubwa kuliko hata huko nyuma tulikokua. Ahsanteni sana. (Makofi)