Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaomba nami nitumie fursa hii kwa leo kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na hasa kwa mambo mawili. Jambo la kwanza, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya na jinsi anavyojitoa kwa ajili ya Watanzania na anavyotumia utashi wake kuhakikisha anatufikia wananchi wote na hata wale walioko chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Serikali hasa Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao ni wasikivu, wanatusikiliza na ni wanyenyekevu. Hii ni silaha kubwa ya maendeleo na ninafikiri hata Mheshimiwa Rais alijua kwamba akitumia silaha hii ataweza kufanikiwa na ni kweli amefanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie juu ya huu Mpango, lakini nitajikita kidogo kwenye ukuaji wa pato la Taifa na katika hili ninaomba nisisitize kwamba, ninaomba twende kwa tahadhari na tahadhari hiyo ikae hasa kwenye deni letu la Taifa. Ninaomba sana Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha hebu twende tupunguze GDP to Debit Ratio angalau tufike 3%0, itatusaidia sana, lakini ninaomba nishauri tutafikaje hapo, ili tufike hapo ninaomba kwa unyenyekevu hebu suala la kuongeza National Mineral Reserve litiliwe mkazo. Tukiitunza dhahabu yetu ikawa kwenye benki yetu, Benki Kuu tutakuwa tunaongeza pato na tutaweza kuhakikisha kwamba thamani yetu inakua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mfumo wa EFD umetushinda, hatutaweza kukusanya pesa kwa mfumo wa EFD kupata VAT, ili tuondokane na hilo, ningeomba tutumie mifumo ya kisasa hasa kwa kutumia mfumo wa kwenda kwenye Bohari zetu kule ambako wanatunza mizigo. Tutumie hata kodi zetu kuhakikisha tunapohesabu mzigo, mtu wetu ambaye ni mfanyabiashara anapoleta mzigo kule ndiko tutumie kuhesabu badala ya kuhesabu kwa watu wanaonunua, ninafikiri Mheshimiwa Tarimba alilielezea vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tumeendeleza sana maziwa yetu, lakini ninataka nitoe tahadhari, inawezekana hata maendelezo yaliyopo kwenye Ziwa Nyasa tunayapigia hesabu kwamba yataleta manufaa. Ninaomba nitoe tahadhari ifuatayo; Mheshimiwa Rais ametujengea meli tatu Ziwa Nyasa, meli kubwa ya abiria inaitwa MV-Mbeya Two. MV-Mbeya Two mkiipigia hesabu ninaomba niwahakikishie tutakuwa tunafanya makosa kwa sababu ile meli haifanyi kazi ipasavyo na haina uwezo wa kufanya kazi kwa sababu haijajengwa kukidhi mazingira ya Ziwa Nyasa. Sasa ningeomba tufanye uchunguzi wa kutosha ili tujenge meli ambayo inafanana na mazingira ya Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunajenga bandari kubwa sana pale Mbamba Bay. Ninaomba nitoe tahadhari, Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 81 hii ni investment kubwa sana na katika investment ambayo tumepata Ziwa Nyasa hii ni ya kwanza. Sasa tunapopiga hesabu za mzigo, tunapiga hesabu za kutoa mzigo moja kwa moja Mbamba Bay kwenda Malawi na Zambia kwa kupitia Mbamba Bay kwenda Nkhotakota kwenda Nkata Bay.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe tahadhari, ninaomba utafiti ufanyike na tuangalie njia mbadala. Tayari tuna matatizo ya mpaka wa Malawi na Tanzania kwenye Ziwa Nyasa, bado hatuja-solve hili tatizo. Ni lazima tuwe na tahadhari na hili halijafika popote. Tunapopiga hesabu za kwenda wakati huku tuna matatizo, ningeomba tujihadhari sana, Mpaka wa Malawi na Tanzania bado ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Bandari za Malawi zinaendeshwa na Wareno. Wareno wanaendesha Beira, Beira ni mshindani wetu kwa Bandari ya Mtwara, hawataturuhusu tupeleke mzigo wetu moja kwa moja kwenye bandari zao na bandari zile wanaweza wakatu-charge fedha nyingi na mfano umetokea. Tukitaka kupeleka meli yetu ya abiria tu fedha wanazo-charge ni kubwa. Kwa hiyo, ningeomba tuangalie alternative. Tuimarishe Bandari ya Itungi, tuimarishe Bandari ya Kiwira na sambamba na barabara inayotoka Katumba Songwe kwenda Ileje ili tuweze kupeleka mzigo Malawi na Zambia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni ushauri tu, kwamba kwa sasa hivi Zambia wana crisis ya umeme na nina uhakika na Malawi watapata crisis ya umeme, Je sisi tumejiandaaje kupeleka umeme Zambia? Pale Kiwira Coral Mine kuna makaa ya mawe, naomba sana hebu twende tukafanye investment pale, umeme ule tuwauzie Wazambia Kariba inakauka. Kwa hiyo, ningeomba sana wanapofanya mipango, hebu tufanye hii ni mipango ya Serikali kuimarisha Kiwira Coral Mine ili tuuze umeme Zambia na Malawi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bonde la Mto Songwe; tumezungumza muda mrefu sana kuna Bonde la Mto Songwe na kamisheni iko pale sasa hivi ina umri zaidi wa miaka 20. Ninaomba sana hebu tuimarishe italeta manufaa kwa wananchi wa Kyela na Wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa sababu kutakuwa na skimu za umwagiliaji ambazo ni zaidi ya hekta 3500, ninaomba sana tulifanyie kazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kinachotufanya mpaka sasa hivi tuhangaike na kinachokula fedha ya Taifa ni matumizi ya diesel au mafuta. Ninashangaa mpaka leo tunapozungumza mipango, nilidhani kitu cha kwanza sasa hivi tuelekee kwenye umeme na gesi na ambapo tungeanzia, tuanzie kwenye BRT pale Dar es Salaam. Miundombinu yetu, basi zetu na vifaa vyetu vya usafiri viende kwenye gesi na umeme. Tusisubiri kutumia diesel tena, lakini miundombinu yetu hebu tuiangalie. Kwa nini bado tunaendelea kujenga miundombinu ambayo itaisha thamani sasa hivi? Kwa mfano, pale BRT…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Ally.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)