Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mafungu yote mawili, Fungu Na. 48 na Fungu Na. 03. Pia, nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi ili nami niweze kusimama kwenye Bunge letu Tukufu ili niweze kutoa mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wa Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, Mheshimiwa Jerry Silaa. Mheshimiwa Rais kama kocha, amechagua mshambuliaji mzuri, mtu mwenye uwezo na mtu ambaye kwa kweli amewa-prove wrong watu wengi ambao walikuwa hawamfahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama namna Wizara imewekwa vizuri kuanzia Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu wake, Katibu Mkuu, Kamishna pamoja na watumishi wengine, utakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Rais anakusudi kubwa la kuhakikisha kwamba ardhi ya nchi yetu siyo tu inapoimwa na kupangwa, bali inakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya Taifa la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi kubwa za Mheshimiwa Waziri, tumeona viongozi wa dini karibu zote ambazo ziko katika Taifa letu wakimwombea dua. Ni ombi langu Mheshimiwa Waziri huyu awekeze ulinzi, ambao utamsaidia kumlinda katika kufanya kazi zake, maana kupambana na majambazi papa ya ardhi siyo kitu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kliniki ya ardhi aliyoianzisha Mheshimiwa Waziri imejibu vilio vingi vya Watanzania. Sasa ni ushauri wangu kwamba kila Mkoa hauwezi kusubiri Mheshimiwa Waziri afike, kila Mkoa hauwezi kusubiri kliniki ya ardhi ifike. Napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri kuweka system maalum ya kushughulikia matatizo ya ardhi, ambayo yeye akisema akiwa ofisini, ile system yote inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake watendaji wake wote kuanzia Mwenyekiti wa Kijiji, Diwani mpaka kufika Taifa kuwe na utaratibu maalum wa kutoa haki kwa wananchi kuliko kusubiri mtu mmoja afike na kliniki kutwa nzima. Kuna kipindi ameendesha kliniki mpaka saa tano ya usiku, hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, jambo lingine ni kuhusu mabaraza ya migogoro, unajua kuna kitu ambacho sielewi, labda leo Mheshimiwa Waziri atanisaidia. Hivi haya mabaraza, ni mabaraza ya kutatua migogoro au ya kuongeza migogoro? Kwa sababu Mabaraza ya Ardhi ya Kata yamekuwa kichocheo kikubwa cha kuongeza migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao, kwa sababu mapato yake hayafahamiki na bajeti ya kuendesha vikao vya baraza haifahamiki. Kwa hiyo, imekuwa mtu mwenye fedha ndiyo mwenye haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote mwenye fedha akienda kushitaki kwenye Baraza la Ardhi la Kata, yeye ndio mshindi kwa sababu yeye ndio atalilisha baraza, atalisafirisha baraza kwenda kuona eneo, yeye ndio atawarudisha na yeye ndio atawagharimia chakula na posho. Sasa hii haiwezekani. Ni lazima kufanya utaratibu maalum, tujue chanzo cha mapato cha haya mabaraza ni kipi na haya mabaraza yanalipwa posho kutoka kwenye fungu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni lazima kuwe na msaada wa uwezeshaji kielimu kutoka Wilaya kushuka kwenye Kata. Maana hawa watu hawajui Sheria za Ardhi, wanachaguliwa tu pale na wakati mwingine wananchi wanalazimisha, “Diwani mtoe huyu au Diwani vunja baraza.” Kwa hiyo, utaratibu wake umekuwa mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema chombo hiki kikawekewa nguvu kubwa ili kiweze kufanya kazi kisheria na mapato yake yafahamike kwamba wakikutana posho wanatoa wapi? Hivi kweli posho ya shilingi 5,000 unalipa Mjumbe wa Baraza la Kata anayeshughulikia mgogoro wa shilingi milioni 100 au anashughulikia mgogoro wa shilingi milioni 10, halafu yeye analipwa posho shilingi 5,000! Ataacha kuchukua mpunga kwa huyu mtu mwenye hela na kumpa haki! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni ushauri wangu, kama kweli tunataka tuone haki inatendeka kwa upande wa ardhi, kwanza haya Mabaraza ya Ardhi ya Kata wawezeshwe msaada wa elimu, wajue taratibu na elimu ya Sheria za Ardhi ili huyu Mwenyekiti wa Baraza la Mgogoro awe ni Mwenyekiti wa Baraza la utatuzi wa mgogoro badala ya kuwa Mwenyekiti wa kuendeleza migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kikosi kazi cha Mheshimiwa Rais kinafanya kazi kwenye vijiji. Mimi nataka kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na ninachukua fursa hii kama Mjumbe wa NEC. Hawa watu wamekuwa wakipima ardhi mpaka vijijini, na Mheshimiwa Samia ameonesha tofauti kubwa. Sasa hivi kuna baadhi ya vijiji vinatembelewa mashamba, yanapimwa na wananchi wa vijijini wanapimiwa makazi yao. Hili ni jambo kubwa ambalo kama likiendelea, nataka niwaambie litatupa urahisi sana kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM inakwenda kuchukua ushindi yaani kwa mtelezo kama vile ilikuwa imeweka, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwakumbuka watu wa vijijini, ila ni rai yangu kwa wananchi kutumia vizuri hizi hati wanazopewa, ni hati za miaka 50, lakini kama wote watakimbilia kuzikopea bila kuwa na utaratibu maalum, wanaweza kujikuta tena mashamba yao yanakuja kufilisiwa na kuuzwa kwa utaratibu ambao utakuwa mbaya sana mbele ya safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nawaomba sana wananchi badala ya kukimbilia kwenda kukopea hizi hati, uwe na uhakika kwamba una biashara na kwamba biashara yako inaweza kulipa huo mkopo unaoenda kuukopa, vinginevyo tutajiingiza kwenye matatizo makubwa sana ambayo hayana sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi ikipima vizuri maeneo ya vijijini, tukajua wapi makazi, wapi mashamba, wapi maeneo ya malisho? Hii ni Wizara mtambuka, hata hayo majani bora kwa mifugo ambayo juzi yalikuwa yanazungumzwa, tutajua tuyapande wapi lakini kama tutakuwa hatujapima na kutenga ardhi yetu vizuri itakuwa ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimesimama kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameipanga hii Wizara ya Ardhi na kwa speed yao ambayo wanafanya kazi kuhakikisha kwamba hati zinapatikana. Pia, utoaji wa haki na kusimamia kuona watu wanyonge nao wakipatiwa haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona taasisi za dini zikirudishiwa viwanja vyao, watu wa dini hawawezi wakaenda Mahakamani wakaanza kusumbuana na watu kutwa nzima, lakini wengine wanaomba dua tu, Mwenyezi Mungu atajalia ardhi yetu itarudi lakini tumeona Mheshimiwa Waziri akisimama na kutoa haki kwa taasisi zetu za dini ambazo zimekuwa zikiombea Taifa hili, Mheshimiwa Rais na amani ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)