Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na ninamshukuru Mheshimiwa Rais. Pia, nimpe pole Mheshimiwa Waziri maana amepewa Sekta nyeti na muhimu kwa Taifa letu, lakini ni Sekta ambayo ililaaniwa na Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee Kitabu cha Mwanzo aya ya 17: “Akamwambia Adam, ‘kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nilikuagiza nikisema usiyale, ardhi imelaaniwa kwa ajili yako.” Haya ni maneno matakatifu. Ndiyo maana nikasema ninampa pole na ameanza vizuri. Naomba nijikite kwenye mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo nitaeleza kwa namna gani ardhi ni muhimu katika kujenga uchumi wa Taifa letu. Hapa nieleze na nirejee maneno ya Hayati Baba wa Taifa aliwahi kusema, “Nchi yoyote ili iweze kupiga hatua za maendeleo lazima iwe na ardhi, watu, siasa safi na utawala bora.” Sasa leo nitazungumzia Sekta ya Ardhi namna gani kwa maono yake Baba wa Taifa ardhi ni rasilimali muhimu kwa uchumi wa Taifa letu, lakini bado haitusaidii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dhana ya upangaji, upimaji na umilikishaji. Kinachofanywa na Wizara ya Ardhi haipangi, haipimi mwisho wake inafanya urasimishaji. Nchi yetu haijapimwa, kinachofanyika sasa ni kurasimishwa siyo kupimwa. Naomba nitoe elimu hapa. Dhana ya upimaji inaanza na nyaraka muhimu mbili; ya kwanza inaitwa land use masterplan na ya pili inaitwa infrastructure masterplan. Sasa nikimwuliza Mheshimiwa Waziri ni halmashauri gani zina infrastructure masterplan? Naomba nitafsiri Kiswahili ili Watanzania wanielewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyosema land use masterplan maana yake ni mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi na infrastructure masterplan ni mpango kabambe wa miundombinu kwenye ardhi. Sasa hilo halifanyiki na ukiuliza halmashauri ngapi zina mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi na mpango kabambe wa miundombinu jibu litakuja sintofahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, kazi yako ni ndogo sana. Tengenezeni mpango wa pamoja na Waziri wa TAMISEMI, halmashauri zielekezwe chini kila halmashauri iwe na mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi na mpango kabambe wa miundombinu. Leo hii eneo pekee ambalo limefanikiwa ni Dodoma Jiji. Tuna masterplan 25 zinasemekana na mwaka huu nimeambiwa tano zimeongezeka lakini hizo masterplan ni land use masterplan na siyo infrastructure masterplan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, Dar es Salaam ni squatter city, Mwanza ni squatter city na Arusha ni squatter city. Narejea, jiji pekee ililopangwa japo wengine hawapendi kusikia, Dodoma kwa sababu ndiyo mfano bora, nitasema. Sasa naeleza haya ili Mheshimiwa Waziri uchukue na kwa sababu una nia njema brother utafika mbali sana, nisikilize kwa makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeeleza hapo kwa nini nasema land use masterplan. Land use masterplan yenyewe inaeleza wapi kuna maeneo hatarishi, wapi tujenge nyumba za makazi, wapi tuweke viwanda, wapi tuweke wawekezaji na wapi tuweke mashamba. Haya hayafanyiki, tunachofanya ni urasimishaji nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa Waziri nikushauri, urasimishaji ubaki kwenye miji na majiji kwa sababu tumechelewa. Upangaji na upimaji uende kwenye halmashauri za wilaya bado hatujachelewa. Majiji ni matano tu na Manispaa kadhaa lakini halmashauri ni nyingi sana na nimesikitika kidogo Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako. Unasema unaalika miji ilete mipango ya maeneo yaliyoiva, siyo kweli na siyo sawasawa hapo. Tusisubiri maeneo yaive, yakiiva maana yake ni squatter tunakwenda kufanya upgrading.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba wote nchi nzima walete mipango kabambe kwa Mheshimiwa Waziri, tuipime nchi yetu, nahisi kama kumsukuma mlevi hivi. Mheshimiwa Waziri shirikiana na TAMISEMI utafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye migogoro. Ameeleza vizuri sana Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake kuhusiana na aina ya migogoro nchini. Sasa nimsaidie migogoro miwili. Ipo migogoro inayosababishwa amesema na wataalamu wake wa Sekta ya Ardhi. Hii kudhibitiwa, na ni rahisi sana, na mwarobaini wake ni ILMIS (Integrated Land Management Information System). Huu ni mfumo fungamanishi wa kuhifadhi taarifa za Sekta ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu watumishi hawawezi ku-tamper kwa sababu hakuna hati pandikizi, huwezi kupata huko. Mfano mzuri Kinondoni huko nyuma wana historia, Kinondoni ilikuwa ni hatari sana, lakini wana ILMIS na sasa kidogo imepunguza migogoro kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Sasa Mheshimiwa Waziri ahakikishe ILMIS inakuwa nchi yote, atakuwa amewabana watumishi wake wa Sekta ya Ardhi na hawataweza kufanya double allocations.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu double allocation naomba nitoe elimu hapa Bungeni na ikikupendeza unaweza kuongeza dakika nyingine za mtu mwingine kwa sababu natoa elimu. Hati pandikizi zinapatikaje? Hati pandikizi wataalamu wa ardhi wanafanyaje? Anakuja mtu mwenye fedha na anakuja mtu aliyetangulia mmiliki halali anaanza kuomba umiliki. Sasa yeye katika hatua za umiliki akija mtu mwenye fedha kile kiwanja kwa sababu ni muhimu anamwambia sikiliza bwana mdogo, kabla hatujazungumza kuna shilingi milioni tano mezani halafu jioni tutaonana. Kijana anachanganyikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yule anayekuja na fedha mfukoni nyaraka zile zinakuwa backdated (anapewa nyaraka zinazorudishwa nyuma ukilinganisha na yule mmiliki halali). Matokeo yake anakuwa wa kwanza kupata hati huyu anakuwa wa pili lakini ILMIS ndiyo mwarobaini, huo mchezo haufanyiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda pia nieleze namna utatuzi wa migogoro ya ardhi. Kuna utatuzi wa migogoro ya ardhi kiutawala na utatuzi wa migogoro ya ardhi kimahakama. Mheshimiwa Waziri siyo mamlaka ya mwisho ya utatuzi wa migogoro ya ardhi. Mamlaka ya mwisho ni Mahakama na ndiyo maana mimi Mheshimiwa Kunambi ukisema ardhi siyo yangu ukanitoa, naenda Mahakamani nakushtaki, nasema sijatendewa haki. Mahakama ndiyo mwamuzi wa mwisho wa migogoro ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri tengeneza mfumo. Uzuri nchi yetu ina utawala bora; kuna kijiji, kuna kata na Waziri ni mamlaka ya rufaa. Sasa unakwenda na wewe utamaliza wilaya ngapi Mheshimiwa Waziri? Hotuba yangu ya mwaka 2023 nilisema kaka yangu nimeona ameanza kuwa na mvi. Sasa wasiwasi wangu, shemeji yupo hapa, hebu punguza hiyo. Tengeneza mfumo, yaani wewe ukiwa Wizarani pale ukikohoa, Mwenyekiti wa Kijiji cha pale kwangu Utengule aseme, naam! Simple, wala huhangaiki. Tutamshauri hata nje ya Bunge atafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa alivyonieleza kwamba ana siku 200 za kutatua migogogoro ya ardhi, nikajiuliza maswali, my brother anatumia nini au ni kalumanzila? Kwa kweli migogoro ya ardhi nchi hii ili iishe tupange, tupime, tumilikishe na tuwe na mpango wa Taifa kwenye jambo hili na tuwe serious. Eneo lingine mamlaka zote zinazohusika zitimize wajibu wake. Wewe uwe mamlaka ya rufaa pale, usimamie Sera ya Ardhi, ukifanya hivyo Mheshimiwa Waziri I’m telling you my brother utafika mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni migogoro ya vijiji 975. Nimeona kwenye hotuba yake kwamba ni migogoro 350 tu mpaka sasa. Kasi hiyo siyo sahihi. Mheshimiwa Rais hataki hayo. Dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wake wanaishi bila migogoro ya ardhi. Vijiji 975 sasa ni mwaka wa pili kama siyo wa tatu, tuna vijiji 350; are we serious? Sasa Mheshimiwa Waziri amepokea kijiti, nashauri kasi iongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kule Jimbo langu la Mlimba, mpaka jana wananchi wangu wanachomewa mazao, wanachomewa nyumba zao kwa sababu ya migogoro ya ardhi na hawana amani. Mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na TAWA na mgogoro wa ardhi kati ya wafugaji na wakulima, mwarobaini ni upangaji na matumizi bora ya ardhi. Mheshimiwa Waziri kwa kuwa ana nia njema, all starts well ends well my brother na nimekwambia nitakusaidia kukushauri vyema.
(Hapa kengele ililia kushiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kunambi, naomba hitimisha tafadhali.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe. Ukisoma Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ukurasa wa 119...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, tuna changamoto ya muda na unatambua.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha. Ibara ya 74 unaelekeza Wizara ya Ardhi kusajili vipande vya ardhi 2,500,000 kwenye miji na hatimiliki za kimila 2,600,000...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, naomba hitimisha hoja yako.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vijiji; kasi ni ndogo. Sasa tunakwenda mwakani uchaguzi, tunafikia lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi? Kaka bado una kazi kubwa ya kufanya na Mungu akusaidie, ahsante. (Makofi)