Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Nami niungane na waliompongeza Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Waziri Jerry Silaa. Mheshimiwa Jerry Silaa tangu umeteuliwa tumeona kazi yako kubwa. Hizi clinic unazofanya na umekutana na wananchi wanavyolalamika, endelea hivyo hivyo na matarajio ya Mheshimiwa Rais na Watanzania walio wengi wanataka hii migogoro iishe na tuwasikilize wananchi. Endelea hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Waziri Mheshimiwa Pinda naye amekuwa akienda kwenye mikoa na wilaya na alikuja pia Kiteto. Endeleeni hivyo hivyo, mkiwasikiliza Watanzania na migogoro hii ikaisha, ndicho anachotamani Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na ndicho wanachotamani Watanzania wote. Tunataka migogoro ya ardhi iishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakupongeza Katibu Mkuu na timu nzima ya wataalamu, endeleeni hivyo. Ninyi ni Sekta ya Ardhi kwa hiyo mtoke sana mwende field, ndiyo matarajio ya Watanzania. Endeleeni hivyo hivyo. Ombi langu moja tu ni kwamba Kiteto tunamtaka Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya, mtuletee huyo kwa haraka sana. Kiteto ni kubwa na migogoro ni mingi, mkituletea Mwenyekiti wa kututembelea siyo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, leo nitajikita kwenye migogoro ya ardhi. Hii dhana ya migogoro ya ardhi ni kubwa. Ardhi ni uhai, ardhi ni mali, ardhi ni tamaduni za watu na maisha ya watu, hivyo, inahitaji utulivu, umakini, weledi mkubwa sana, utawala wa sheria na sheria itafsiriwe kama ilivyotakiwa na Bunge. Vilevile, inahitaji teknolojia kwa sababu nchi yetu ni kubwa, ili tuweze kupima na kupanga kiteknolojia, tena teknolojia sahihi sana ambayo ina precision nzuri ambayo haitengenezi migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro mingi sasa tuliyonayo, kila ukituma timu iende field inatengeneza ramani yake. Unaweza ukakuta mgogoro mmoja una ramani sita. Fedha zimetumika za Serikali halafu wataalamu wetu hawa wanatuangusha sana. Naamini kwamba utaalamu walionao wataalamu wetu ni wa kusoma GPS, kutumia mashine hizi na kusoma Sera na Sheria ya Ardhi lakini siyo wataalamu wa mapori ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima kushirikisha wananchi. Ni jambo muhimu mno unapokwenda site kutaka kufanya ile GN ifanye kazi, wasikilize wale walio na ardhi yao. Hii imekuwa tofauti, anakuja mtu anajifanya ni mtaalamu. Sasa ni mtaalamu kweli wa mipaka ya mapori yetu? Wewe ni mtaalamu, umesomea wapi mapori yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukifanya hivyo, watunze utaalamu wanaopata shuleni kutumia GPS na hizi teknolojia na namna ya kusoma GN, lakini inapokuja kwenye majina ya maeneo ya watu, msikilize watu. Haiwezekani mnakuja mnatuambia hapa, yaani mnajifanya kwamba ni mafundi mpaka wa vijiji vyetu na majina yetu na vitongoji na milima eti. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri awaambie watu wake wawe na weledi na washirikishe wananchi. Tukifanya hivyo migogoro ya ardhi nchi hii itakuwa imekwisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro inataka weledi kwa sababu inaleta ugomvi. Watu wanachotaka ni tafsiri sahihi za hizi GN. Pia, namna ya kufanya hivi ni kuwa na Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi yenye bajeti kubwa sana. Tunaambiwa hapa na Mheshimiwa Waziri kwamba kati ya vijiji 12,318 ni vijiji 4,126 ndivyo vitakuwa na matumizi bora ya ardhi. Kwa hiyo, kuna vijiji zaidi ya 8,192 visipopata majawabu migogoro haitakaa iishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuamue kama tunataka kumaliza migogoro ni lazima Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi iwe na pesa nyingi sana. Tupime vijiji kwanza, tukishamaliza na vijiji vikawa na hati na matumizi bora ya ardhi tutakwenda kwenye hiyo individual tabling tunayotaka. Huwezi kuwa na individua tabling kama vijiji havifahamiki mipaka yake. Nchi hii ardhi yote tuliyonayo hata naogopa siku hizi kutaja statistics. Ardhi zimegawanyika sehemu tatu; ardhi ya vijiji, ardhi ya hifadhi na ardhi ya jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaambiwa ardhi ya vijiji ni 70% sijui siku hizi imefika ngapi. Ardhi ya hifadhi tulikuwa tunajua ni 28% sijui siku hizi imefika ngapi na general land ilikuwa ni asilimia mbili, lakini siku hizi ni vice versa. Mheshimiwa Waziri ni Mwanasheria na Naibu wake ni Mwanasheria, wanafahamu kuwa ardhi ikishaitwa hii ni ya kijiji ni ya kijiji. Ardhi ya kijiji kwa mujibu wa sheria yeye anafahamu, kuna aina tano ya namna ya kutambua ardhi ya vijiji, kwanza kama kijiji kina hati na imepimwa na hiyo inajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa mujibu wa kifungu 22 ya Sheria ya Serikali za Mitaa, watu wa TAMISEMI, that is known. Ardhi nyingine ni kijiji kilichoanzishwa kwa ile Sheria ya operation vijiji. Nyingine ni ardhi ambayo wananchi wamekuwa wanakaa tu ama ardhi ambayo vijiji vimekubaliana ama ardhi ambayo watu wamekaa wanaishi kwa maisha ya kijijini kwa zaidi ya miaka 12 baada ya Sheria ya Ardhi kuwa imepitishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lugha nyepesi, popote wanakoishi wananchi sasa ni ardhi ya vijiji whether wana hati ama hawana kwa mujibu wa sheria. Wakati mwingine Wizara na Mheshimiwa Waziri anafahamu, Kifungu 185 cha Sheria ya Ardhi, linapokuja suala la ardhi yeye ndio mkubwa kuliko Waziri mwingine yeyote. Sasa sijui wanaogopana ama sijui ni nini? Waziri aweke mguu chini, yeye ndiye mwenye dhamana ya ardhi, yeye ndiye anayetakiwa atutafsirie ardhi ya kijiji ni wapi? Ardhi ya hifadhi ni wapi? General land ni wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiona wale wa maliasili wanakuja kugombana na wanakijiji; amesema Mheshimiwa Kunambi hapa kwamba wanawachomea watu nyumba. Ukiona wale wanafika mpaka kwa wananchi, there is something wrong, hamfuati sheria. Kimsingi watu wa maliasili walitakiwa waende kwa Waziri waseme, tunaomba uje utuambie mipaka ya vijiji inaishia wapi? Halafu wao wapotee, hawarusiwi kwenda kwa watu. Waziri ndiye anatakiwa aje atutafsirie na kama ni fidia, yeye ndiye aje atuambie tunapataje fidia kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukisimamia mipango hii na akasimama vizuri kama Waziri wa Ardhi, hakuna migogoro hapa. Mkiwaacha kila mtu achore ramani yake anavyotaka kama wanavyofanya wale watu wengine, sasa migogoro itaisha lini? Kwa mfano, Kiteto tumekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya Manyara na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Ardhi 2015, juzi tu wamekuja timu kutoka Ofisi ya Takwimu, Wizara hii na Ofisi ya Waziri Mkuu, imetengenezwa ripoti ya kusema ni tathmini na mipaka, mkatuchorea ramani za vijiji na hati mkatupa. Halafu wengine wanakuja miaka mitatu baadaye wanasema wale walikosea. Sasa twende wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro mmoja unakuwa na ramani na ripoti sita au saba, wanawa-confuse wananchi unnecessarily. Hiyo waache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aje Orkiush kwa ajili ya mgogoro wa Orkiush na Mkungunero. Sasa hivi tunachotaka ni tafsiri sahihi ya ramani ya Mkoa wa Manyara na Dodoma, period. Kwa hiyo, tunahitaji equipment ambazo ni precision, ambazo hazitakuwa na error.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ule mgogoro nikikuletea ramani zake utashangaa sana, kuna michoro zaidi ya mitatu na tume tatu, kila mtu ana ramani yake. Hapo mwananchi atakwenda wapi? Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri akisimamia hilo tutatoka vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ipo kwa sababu wananchi hawashiriki. Nilikuwa nasoma hotuba yake hapa, mgogoro wa kwetu na Tanga huko Kilindi; kweli kwa mujibu wa GN inaonekana umemalizika, lakini imagine GN inatengenezwa, na unajua GN inavyosema, kwamba ikiwa mamlaka haijapewa objection yoyote kwa hiyo tunafanya hivi. Sasa wasipotutangazia, na tukiwa na objection tutaleta wapi kama mambo yanaishia kwenye GN na ofisini? Je, yule mwananchi ambaye alitakiwa kuleta objection ataona wapi? Wasimamie na tufuate utawala wa sheria. Tukifuata sheria vizuri migogoro hii itakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Mheshimiwa Waziri wakati mwingine ana mamlaka akiona hizi tume hazileti majawabu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mbunge, tunakushukuru.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, tunakutakia kila la heri Mheshimiwa Waziri. (Makofi)