Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa mafungu yake mawili; Fungu Na. 48 na Fungu Na. 3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia nami nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya kwenye nchi yetu. Ni dhahiri kila Mtanzania anajua kazi inayofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa haraka nitumie nafasi hii kuipongeza sana Wizara kwa ujumla; kamisaa wetu Mheshimiwa Jerry William Silaa na kaka yangu Mheshimiwa Mizengo Pinda Geophrey, pia nisiache kwa watendaji wakiongozwa na Mhandisi Sanga, Katibu Mkuu; Naibu Katibu Mkuu pamoja na wataalam wao wote. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri ambayo na sisi Waheshimiwa Wabunge tunaithamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nijielekeze kwenye maeneo mawili tu. Eneo la kwanza ni eneo la urasimishaji likienda sambamba na migogoro ya wawekezaji dhidi ya wananchi wetu au ya maeneo. La pili, ni eneo hili ambalo wengi wamelizungumzia. Kuhusu Fungu Na.3 la Tume yetu ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la urasimishaji ni sehemu ambayo katika kipindi changu cha miaka mitatu, na huu wa nne, nimekuwa nikilisema kila tukiwa tunachangia bajeti. Naipongeza sana Serikali, imefikia pazuri, tofauti na tulipoanzia; na hapa mlipofika mpaka leo mmepata mkopo wa Benki ya Dunia wa shilingi bilioni 345 na mmejielekeza nazo kwenye maeneo ya Dar es Salaam huko ili kuondoa migogoro kupitia dawati au Kliniki ya Ardhi. Pamoja na maeneo mengine, huko kwenye nchi yetu, mimi napongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye hili eneo, Waziri akiwa ni mdau wetu wa Dar es Salaam, pia naomba sana waongeze kasi. Kamati imesema ina shaka juu ya huu mradi wetu wa LTIP kama unaweza kwenda sawa kama tulivyokusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aongeze kasi kwenye madawati hayo ili mpaka tunafikia uchaguzi wetu Dar es Salaam, nami nishukuru sana viongozi wangu wa Mkoa wa Dar es Salaam wako hapa, wametambulishwa, nashukuru, lakini watambue wazi sasa hivi hii ndiyo agenda yetu Dar es Salaam. Urasimishaji kama hatutoboi na kule nje patakuwa ni balaa. Hili ni jambo jema, nimemwambia tukiwa ndani na tukiwa wawili; na hapa nalisema wazi kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwa ujumla wake ni hili jambo la usimamizi wa ardhi na wawekezaji. Nchi yetu imefanya sensa kwa zaidi ya mara tano hivi; mwaka 1967, tumefanya tena mwaka 1978. Mwaka 1967 ilikuwa na watu milioni 12, mwaka 1978 milioni 17, mwaka 1988 tukafanya tena tukawa na watu milioni 23, mwaka 2002 tukafanya tena sensa tukawa na watu milioni 34, mwaka 2012 na mwaka 2022 tukawa na watu milioni 61. Kwa sensa ya mwaka 2022 Bara ina watu milioni 59.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka kusema kwamba nimeona hoja ya wawekezaji, nami naipongeza sana Wizara, wamekuwa wanayo nia ya kuingiza wawekezaji 151 kutoka nje na wawekezaji 65 kutoka ndani, jumla yake ni takribani maombi 216, amesema Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana. Amezungumza kuwa hawa wa nje wana matarajio ya kumwingizia mtaji wa zaidi ya dola milioni 58.95 au bilioni 152. Hili ni jambo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo kwenye hao wa ndani ambao kwa sasa kwa mwaka huu wamewafikiria maombi yao kama 65 hivi. Kwenye historia ya nchi yetu kuanzia miaka ya 1980 tumekuwa na wawekezaji uchwara. Hizi lugha ngumu sana, nitakuwa najitahidi kujifunza Kiswahili. Nataka nimpe mfano mmoja, tunaye mwekezaji wa tangu mwaka 1984 mpaka 1987 alifika ndani ya kijiji Jimbo la Kibaha Vijijini kwa ndugu yangu Mheshimiwa Mwakamo hapa, sisi wengine ni Wazaramo, wakati huo huo ni Waluguru; ndiyo humo humo kwetu kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwekezaji huyu ameingia akapewa ekari 200 vizuri tu. Alipopewa ekari 200 amekaa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15, anatoka anawaambia wananchi pale kwamba mimi nina ekari 2,500. Ekari 2500 ni kama vijiji viwili vya Lupunga na Kikongo, hatari sana. Vilevile wapo watu pale ndani ambao walikuwa ni sehemu ya ajira kwenye kulima mchicha kwenye ekari 200, na kesho yake wanakuja kuambiwa kuwa hata wewe tulikununua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ni kwamba mwekezaji wa aina hii anafika anaulizwa, onyesha hati, hati haionyeshwi, anawaambia tu kwamba kuna hati. Sasa hebu onyesha pale nilipokuuzia mimi, anasema nilinunua mikorosho, kwangu hakuna mikorosho, nilipewa tu zawadi hata maeneo ambayo hakuna mikorosho, lakini kuna viongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata juzi nilikuwa nasema hapa, kuwa nyie viongozi wakubwa, Katibu Mkuu na Waziri ni wa kuteuliwa, kila siku mnabadilishwa, lakini kuna wataalam wetu huku chini ambao ni changamoto. Sasa eneo kama hili nilitegemea RC wangu awe anafika ndani kwenye mashamba ili ajionee. Wanayetaka kumtoa leo ana mti wenye unene wangu, wanayetaka kumwingiza hajawahi kulima hata mchicha, wamempa leo ana miaka 40 ilhali sheria na sera inazungumza miaka 12. Wanasimamia sheria ya wapi? Kwa nini wananchi wanaonewa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiacha hoja hii, nilizungumzia sensa ili uweze kuona kwamba kama mwaka 1978 au 1988 ambapo kulikuwa na watu 23,000, leo watu 59,000 kwa mujibu wa mambo ya ardhi; watu 59,000 ambao ni vijiji viwili anawapeleka wapi hawa? Mheshimiwa Waziri hili analijua vizuri, atarajie kwenda kule akamwokoe Mheshimiwa Mwakamo na akakiokoe Chama Cha Mapinduzi ndani ya Wilaya yetu ya Kibaha Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nilizungumza kuhusu Fungu Na. 3 – Tume ya Taifa ya Mipango. Wengi wamesema lakini mimi nitapenda kusema kwa takwimu. Mimi nimekuwa nikishangaa sana, na hapa nizungumze tu kwamba napongeza ule mradi wa LTIP wa dola milioni 150, takribani shilingi bilioni 345. Pamoja na mambo mengi, mwaka jana tulimwambia Waziri mwenye dhamana aliyekuwepo wakati huo, Mheshimiwa Dkt. Angellina Mabula, tukasema hizi ni fedha nyingi, wameweka mipango mingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie, wamekusudia kuingiza takribani vijiji visivyozidi 1,667 kwenye upimaji huu, tena baada ya maboresho, na vijiji hivi kwa thamani ya kupima kijiji kwa shilingi milioni 15, maana yake anatarajia kuweka shilingi bilioni 25, hazizidi hapo. Kwa hiyo, ndani ya hizo fedha zote za mkopo atatuambia hapa hajachukua zaidi ya shilingi bilioni 23, ndizo alizoziingiza kwenye kupima ardhi za vijiji, tutapima kweli!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Olelekeita amemaliza kusema hapa, na Mheshimiwa mwingine ndugu yangu wa Dodoma amezungumzia kuhusu nia njema ya kupima. Kama tungepima, tungetambua wazi kwamba kuna maeneo ya malisho yangehitajika na tungejua ya kilimo, makazi, uwekezaji, miundombinu ya barabara, huduma za jamii na hifadhi za misitu. Mheshimiwa Olelekeita ameuliza ni asilimia ngapi hii? Hatujui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kaka yangu Mheshimiwa Bashe, katika miaka yake miwili ametafuta shilingi bilioni 700 humu ndani. Ameanza na shilingi bilioni 249, mwaka wake wa kwanza tukamwekea shilingi bilioni 700, wa pili shilingi bilioni 900 na huu wa tatu shilingi trilioni 1.1, over seven hundred billion.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jerry Silaa, miaka miwili anahitaji shilingi bilioni 120 kupima vijiji 8,400 alivyobakiza 120. Kwa nini yeye akose ndani ya Bunge hili? Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, capacity yake ya kufanya katika kipindi cha mwaka mmoja ni capacity ambayo inaweza ikampa takribani vijiji 1400; na ukimpa kwa shilingi milioni 15 maana yake anahitaji shilingi bilioni kama 20. Sasa katika shilingi bilioni 20 leo wanampa shilingi bilioni tano! Kwa shilingi bilioni tano aliishia kupima vijiji 300. Sasa si ataishia vijiji 400! Tunakwenda wapi? Anahitaji miaka 19.6 au miaka 20 kupima vijiji vyote 8,400 vilivyobakia. Haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge humu ndani kwa nia njema tumsaidie Mheshimiwa Rais, maana siasa ya Chama cha Mapinduzi zipo ndani ya upimaji wa vijiji kutokana na faida ya upimaji wa vijiji hivyo. Tukipima vijiji ndipo tutaona vizuri, hata lile jambo zuri la kilimo la Mheshimiwa Bashe lingeenda vizuri. Tutajua anaishia hapa, wafugaji wanaishia hapa, wawekezaji wanaishia pale, huduma za jamii wanaishia kule, eneo la misitu linaishia pale, malisho yanaishia huku. Tunaanzia juu tunashuka chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi kwenye vijiji. Kwa mwaka huu apewa shilingi bilioni tano kwa ajili ya maendeleo ili kupima vijiji 400, haimtoshi. Capacity yake ni vijiji 1,100 au 1,400. Tukimpatia shilingi bilioni 20 angalau atatumia miaka mitano kupima vijiji vyote 8,000 vilivyobakia. Hili ni jambo la msingi na jambo la muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nitumie tena nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kumwona yeye kama kamisaa anayetufaa kwenye Wizara hii. Anaendelea kuwa na macho makubwa ya kuona dira ya Taifa inakotaka kwenda. Tunaendelea kumwombea dua Mheshimiwa Rais ili Mwenyezi Mungu ampe karama kubwa, aliyonayo iongezeke mara dufu na Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia hija na haja ya kuendelea kutuhudumia katika kipindi kinachokuja 2025/2030,…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: …tupo kwa ajili yake na tutahakikisha kura zote zinakwenda kwake. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi, naunga mkono hoja kwa asilimia zote. (Makofi)