Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupatia afya na uhai wa kuendelea kuwatumikia wananchi waliotuchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Mheshimiwa Jerry Silaa katika kuwakaribisha viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. nasema hivyo kwa sababu, kama angekuwa amepata nafasi hii kwa miaka minane iliyopita, basi nami ningekuwa miongoni mwa waalikwa maana nilikuwa Katibu wa CCM Dar es Salaam. Pia ukimsifu Mheshimiwa Jerry katika kazi anayoifanya, nipe na mimi sehemu kidogo ya sifa kwa sababu nimechangia malezi yake huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kupata uhuru wa nchi yetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa letu alitangaza maadui watatu wakubwa wa Taifa letu na akatangaza mambo manne makubwa ambayo yanaweza yakafanyika ili tuendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maadui hao watatu alitangaza; ujinga, umasikini na maradhi. Kila Mtanzania akawa anajua kwamba hawa ndiyo maadui wakubwa wa Taifa letu, lakini akasema ili tuendelee tunahitaji mambo manne; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza juu ya ardhi yetu tukitathmini maneno haya ya Baba wa Taifa letu. Yapo mambo ambayo mimi ningependa kutumia nafasi hii kwanza kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Vilevile, kumpongeza Waziri mwenye dhamana, ndugu yangu Mheshimiwa Jerry Silaa, Naibu wake Comrade Askari wa Jeshi Mheshimiwa Pinda pamoja na watendakazi wote wa Wizara. Ukijua kulaumu, ujue na kusifu maana haya mambo yote duniani yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma kabla ya juhudi zilizochukuliwa na Serikali hii chini ya uongozi wa Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoa mzima tulikuwa na watu wanaomiliki ardhi kwa hati zilizo rasmi 5,426, mkoa mzima, lakini ndani ya muda wa kipindi kifupi ambacho maboresho makubwa yamefanyika na hiyo ni Julai, 2020 kuja Mei, 2024 wameongezeka watu 7,301. Kwa hiyo, kuna kazi kubwa. Kazi iliyofanyika tangu uhuru ni 5,426, kazi iliyofanyika kwa miaka mitatu 7,301 nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Uchaguzi ya CCM Ibara ya 74 imeelezea mambo muhimu ambayo Serikali ya CCM itayasimamia katika sekta ya ardhi. Ikasema, kwanza ni upangaji; pili, ni upimaji; na tatu; ni umilikishaji wa ardhi. Kazi hii ni muhimu sana. Ukishapanga ardhi na kupima ardhi unapata mambo mawili ndani ya jambo hilo, moja. Unaondoa migogoro ya matumizi ya ardhi; pili, unaongeza wigo wa kodi na pato la Taifa kupitia ardhi. Kwa hiyo, mimi nimtie moyo sana Mheshimiwa Waziri kwamba, kazi anayoendelea nayo ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi aongeze kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nilitaka achukue changamoto hii. Kulikuwa na utaratibu wa kurasimisha makazi ambapo Halmashauri yangu ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ambayo mimi ndiyo Mbunge, iliingia kwenye utaratibu huu, vikaja vikampuni vingi vingi vya kupima ili watu warasimishiwe makazi. Nashukuru mmechukua hatua maana kulikuwa na matatizo makubwa kwenye Kata ya Machinjioni, Lubuga, Bangwe, Kitongoni na Kibilizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu wa Ofisi ya Ardhi pale wamefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha yale matatizo yaliyokuwepo ambayo yametokana na yale makampuni yaliyokuwa yamepewa kazi, wameyarekebisha na watu wameanza kupata hati kwa kasi kubwa sana. Ahsante sana tunashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado nawaomba mwendelee na juhudi hii katika Kata ya Kibilizi ambayo maeneo ya Bushabani na Kigamboni bado yana tatizo na Kata ya Kitongoni kule Ujiji nayo bado ina tatizo. Mheshimiwa Waziri nataka niseme juhudi mlizozichukua ikiwa ni pamoja na kupunguza ada ya maombi kutoka 20,000 mpaka 5,000, kupunguza ada ya utayarishaji wa hati kutoka 50,000 mpaka 25,000 na kupunguza kiwango cha kulipia deed plan kutoka 20,000 na kuwa free, haya mambo yamechochea sana wananchi wengi kujitokeza kupata hati. Kwa hiyo, endeleeni na jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimalizie jambo moja. Kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 Ibara ya 74(e) kinaeleza hivi, “kuimarisha mfuko wa fidia ya ardhi ili uweze kufidia ardhi itwaliwayo (inayochukuliwa kutoka kwa wananchi) kwa matumizi ya umma na kwa uwekezaji.” Hapa bado kuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mfuko sijui upo au haupo! Sikusikiliza vizuri wakati unaunasoma, ukija hapa utanielezea vizuri kama upo na una kiasi gani cha fedha, maana hapa napo tunakumbana na matatizo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ya wananchi katika maeneo mengi inachukuliwa, na kufidiwa inakuwa shughuli. Wengine wamekaa ardhi yao imechukuliwa miaka mitano na hawajapewa fidia. Hili jambo linasononesha sana. Hivi leo nilivyosimama kuzungumza hapa kuhusu upanuzi wa Uiwanja cha Ndege wa Kigoma tayari kuna wananchi maeneo yao yamepimwa na wameambiwa wasiendeleze chochote wasubiri fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni zaidi ya miezi saba hawajapata fidia, hawawezi kujenga choo, mvua zinanyesha zinaharibu maeneo mbalimbali, wanasubiri fidia na fidia hazipatikani. Mbaya zaidi mnavyochelewesha kulipa fidia kwa mujibu wa sheria na taratibu za evaluation ikishapita miezi sita ni lazima mwongeze tena asilimia kwenye zile fedha. Kwa hiyo, chukueni maeneo ambayo mko tayari kuyalipia kwa sababu mtayalipia kwa kiwango hicho bila kuongeza gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo pale Kigoma la Kigoma Special Economic Zone nalo bado lina kelele kelele. Wapo wananchi wanalalamika, wengine wanasema hawajalipwa fidia, wengine wanasema tumelipwa, wengine wajanja wajanja wakaingia hapo. Mheshimiwa Waziri, hii ni kazi yako yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ni watumishi wa ardhi. Tunaomba Waziri atusaidie, ile ardhi watumishi wake watachochea sana mapato ya kodi ya ardhi kwenye nchi yetu. Kama tulivyotoa priority kwa watumishi wa TRA kuongezwa ili wakusanye kodi, na hawa waongezwe ili wawe wa kutosha na kodi iweze kupatikana nyingi kwenye ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)