Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Namshukuru Mheshimiwa Rais, ameanzisha Haki jinai na bahati mbaya sana hajafika katika Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara, sijui kama maeneo mengine lakini kwangu haijafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Haki jinai ikienda kule Tarime, ikaenda maeneo ya Sirari itakutana na watu ambao wamepigwa na mipini. Ikienda Hifadhi ya Serengeti itakuta kuna wajane kule wana makovu, miguu na macho hawana. Ukienda kule Nyamongo kuna mambo mengi; wajane, yatima na walemavu, wote yaani raia na askari ni kama uwanja wa vita. Kwa hiyo, ningeomba hii Haki Jinai iende kule Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Waziri Mkuu alifanya ziara katika Mkoa wa Mara na Wilaya ya Tarime. Alisimama maeneo ya Nyamwaga ambako ni karibu na Machimbo ya Barrick North Mara, akatoa maelekezo kule na wananchi walijitokeza kuuliza maswali mbalimbali. Kuna fidia mbalimbali zimefanyika katika eneo lile kwa maana ya Nyamwaga yenyewe, Komarera, Nyakunguru, Kewanja na Komarera North. Pia ikaonekana Mthamini Mkuu wa Serikali alifanya tathmini katika maeneo hayo, lakini baadaye ikaonekana gharama ni kubwa, kwa hiyo, watu hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi yeyote wa Serikali akifika katika maeneo hayo, hoja ya kwanza ya wananchi ni fidia ya Komarera North. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi pamoja na wenzake naomba, jambo hili; nilikwenda pale kwenye Kliniki ya Ardhi nikaonana na watu wake. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa yuko tayari, watu wa ardhi wapo tayari, aongee na mtu wa Madini watafute gharama wakasikilize hawa wananchi. Wananchi wanachanganya, kuna watu ambao wana haki na wengine hawana haki. Ukiwasikiliza utatenganisha mwenye haki na yule ambaye hana haki ili mwenye haki yake aweze kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wetu ni mgumu sana, kila akienda kiongozi hata kama una nia njema, ni lazima kwenye kikao chochote hoja ya fidia ya eneo hili iibuke. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeomba jambo hilo ilifanyie kazi na kwa kuwa wapo viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Jerry tunafahamiana sana, tumekuwa Mlimani Faculty of Science, nilikuwa Mbunge wake, Mwenyekiti wake na Rais wake wa Chuo, Mwenyekiti wake wa Mtaa, tumegombea Ubunge.

Mheshimwia Mwenyekiti, sasa Mwenyekiti wa Mkoa yuko hapa, ili nisirudi tena Ukonga, Mzee fanya kazi kule Tarime, rahisisha mambo yaende sawasawa. Mimi nimezoea siasa, hata ukiniacha watu wakaanza kunishughulikia kule kwa fidia, maana yake nitarudi pale Kivule Mwembeni na sitakaa kimya tutasumbuana. Nakutakia kila la heri, chapa kazi, lakini weka nguvu kule Tarime ili watu wangu waweze kupata fidia, inakuhusu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Olelekaita amezungumza hapa, Mheshimiwa Waziri ni kweli katika vijiji 975, Jimbo la Tarime Vijijini nina vijiji saba. Shida kubwa ni watu kusikilizwa, yaani watu wenu wataalamu wakienda kule wana majibu, ramani na wameshachora mipaka. Unamwambiaje mtu kwamba siyo kwake na ameshakaa miaka 70, anakuonesha makaburi, mikahawa na kila kitu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani mwende mkawasikilize watu na mgogoro huu umesimama kidogo baada ya Wakuu wa Mikoa angalau kuelewa hali halisi ya kule kwetu, lakini tunaomba mgogoro huu uishe, wananchi wasikilizwe, mpitie mipaka, kwa sababu hii nchi ni ya kwetu sote. Kama hifadhi wana haki na wananchi wana haki ya kuishi. Kwa hiyo, lazima Wizara iweze kufanya kazi kutusaidia vizuri katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Mheshimiwa Rais, amefanya mabadiliko katika Mkoa wa Mara. Nataka nimwambie Kanali Mtambi na Kanali Surumbu Maulid, mapokeo ilikuwa ni kwamba tumepokea wanajeshi hapa, lakini nataka niseme na nadhani Wabunge wenzangu watanikosoa, lakini Mkuu wa Mkoa pamoja na DC wetu katika Wilaya ya Tarime ameanza vizuri. Amefanya ziara, amesikiliza watu na ni kwa kuwa anafanya kazi kama raia. Kwa hiyo, naomba waendelee kuchapa kazi na wawasikilize. Watu wa Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara wanataka kusikilizwa, hawataki mabavu, ukiwasikiliza mtafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ardhi na mgodi, mimi kama Mbunge wa Tarime Vijijini ambako Barrick ipo kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana. Mambo mengi yamefanyika na huduma za kijamii na watu wa Mgodi wa Barrick na watu wa Ardhi wakikaa vizuri. Kwa mfano, kule kwetu unalichukua eneo la mtu ambalo anajua kwamba chini kuna dhahabu, halafu unamwambia ekari moja ni shilingi 5,000,000/= lakini mtu huyu huyu ukimpeleka eneo la Itiryo, kule Kiyongera ukienda unaambiwa ekari moja ni shilingi milioni 30. Sasa nakuuliza, hivi sina akili kweli!

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lenye dhahabu chini eka moja ni shilingi milioni tano, eneo la kuchimba choo eka moja ni shilingi milioni 30, wapi na wapi hii? Hata hivyo, ukiuliza watu wa Ardhi wanasema sisi tukija kama wawekezaji tukija Tanzania tunafuata sheria zenu. Kwa hiyo, tumegundua wanaoumiza wananchi wetu ni Serikali, Wizara ya Ardhi na wadhamini. Kwa nini msiweke bei kubwa? Mmtu anajua kwamba hapa kuna dhahabu, kwa nini msiweke bei kubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana leo ninaposema hapa, kwa mfano, nimesema nimwombe Mungu labda nizungumze taratibu. Maana yake humu nimeshalia sijasikilizwa, nimerukaruka kichura sijasikilizwa, sasa sijui nifanye nini? Nimevua koti bado imekuwa ngumu. Sasa naongea kwa upole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunapozungumza kuna msiba mkubwa sana pale Nyamongo. Tarehe 22 saa saba mchana vijana wangu waliji-organize kundi wakaenda kuvamia mgodi. Kwa hiyo, wamepambana na Polisi, wamekufa vijana wawili. Ninavyozungumza hapa, kesho wanazika. Kwa hiyo, hali ya kisiasa ni tete pale katika lile eneo zima la Nyamongo. Vile vile tarehe 01 mwezi wa tatu nilikuwa pale, Binti Neema Omari mwenye miaka 16 alipigwa risasi lakini nikaenda pale tukamtoa risasi mbili, tarehe 26 mwezi wa Nne, ameuawa mtu, tarehe 5 mwezi wa Tano ameuawa mtu, tarehe 22 mwezi wa Nne, sasa katika mazingira hayo maana yake vijiji vyote wanazika, na mgogoro ni nini? Mgogoro ni kwamba, katika kutoa yale maeneo ya wachimbaji, mikataba ni kwamba ukimlipa mwananchi mzawa shilingi milioni tano anahama. Hata hivyo, ana watoto, wakikua wakawa wakubwa wanaambiwa eneo letu ni hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu naomba katika eneo hili, kwenye mikataba mipya inayokuja ya kutoa maeneo ya watu tuwe na mikataba ya shareholder. Ni kwamba, kama mtu akichukua eneo la uchimbaji, awe na share katika uchimbaji ule ili wale watu waendelee kuishi kwa kadri ambavyo miaka inaenda. Akipewa fedha akashindwa ku-survive mmetengeneza mazingira magumu sana katika Wilaya ya Tarime, na kwa hiyo, inatusumbua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niseme, nilitaka nizungumzie migogoro ya ardhi. Nimewaambia na watu wa Wizarani pale, kule kwetu ukienda pale Korotambe, miaka nenda miaka rudi wanagombana na watu wa Remagwe kule Pemba, na mgogoro haujawahi kwisha. Ukienda Mrito – Msege wanagombana, nenda Marasibora Rorya na Tarime Nyamberambalu wanagombana. Sasa maeneo hayo ndiyo ambayo Mheshimiwa Waziri anaweza akatufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri wa Madini na mgodi wamekubaliana, nadhani kama sikosei wiki ijayo kwa taarifa ya Mheshimiwa Mavunde ni kwamba mtaongozana kwenda kutoa yale ambayo mgodi hawana uhitaji mkubwa ili yatwaliwe na kupewa vijana wachimbe (wachimbaji wadogo). Vilevile, Mheshimiwa Mama Dkt. Samia ameshapeleka gari la wachimbaji la madini, litawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mgodi wamekubali kuchukua vijana na kuwapeleka kwenye stadi za maisha (VETA) kwa gharama zao na kuwapa vitendea kazi. Hii pia itapunguza tension ya kuja hapa Bungeni kila siku kuwaambia watu wanauana kama kuku katika eneo lile ambapo kwa kweli kama watu Mkoa wa Mara na hasa Wilaya ya Tarime siyo jambo jema sana kwamba kila siku lazime uzike; kuna risasi, kuna mapanga. Siyo sawasawa. Pia kuna namna moja ambayo wanatakiwa wasaidiwe kuweza ku-survive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Jerry kwamba hii Wizara ni kubwa sana na ina shida sana. Hata hivyo, nataka nimwambie, kwa namna ambavyo ulianza na nimekuomba uje kule Tarime na hasa kule kwenye maeneo ya Mgodi na maeneo mengine ufanye kazi ya ziada. Nataka nimwambie, tunataka migogoro ya wafugaji na wakulima iishe, tunataka ugomvi wa wakulima uishe. Ni kwa sababu watu wamemheshimu, ameanza vizuri na tunaomba aendelee vizuri, lakini kimsingi yaani kila ikija hapa Wizara ya Ardhi, Wizara hii haijawahi kuwa rahisi kwa sababu kila Mbunge hapa ana mgogoro katika jimbo lake, kila Mbunge hapa kwenye wilaya yake kuna mgogoro, kila Mkoa kuna mgogoro na bahati mbaya watu wake wanakula rushwa kweli kweli. Wanakula rushwa bila kunawa na wanaonea wananchi. Sasa hili ni lazima Mheshimiwa Waziri atengeneze mfumo kwa wale watu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye halmashauri zetu katika idara ambayo haina nguvu sana ni Idara ya Ardhi. Kuna mtu mmoja tu aidha, mmoja na dereva na hana gari halafu anaamua peke yake. Hata hivyo, ardhi ni maisha. Pia, Baba wa Taifa alisema ukitaka maendeleo ni vitu vinne; uwe na watu, ardhi, uongozi bora na siasa safi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa safi ipo, Mama Dkt. Samia ameweka mambo level, uongozi uko vizuri, ardhi ipo. Sasa ardhi hii isimamiwe, na Waziri ni mwenyeji katika watu ambao wamekuja kuelezea hapo Wizarani. Waziri ni mtu ambaye angalau katika matamko ya Mheshimiwa Baba wa Taifa naye anatajwa, ardhi. Kwa hiyo, naomba atoe heshima hiyo na sisi Wabunge tupate kutoa ushirikiano. Ukienda kwenye eneo la jimbo fulani, ita viongozi wa kisiasa, Wakuu wa Mikoa, Ma-DC na wananchi washirikishwe, migogoro mingine wanaijua mipaka yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, leo nimesema nichangie na hapo nimechangia kwa upole sana. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kile kitimoto kule kwenye jimbo langu mnisaidie kupunguza ili joto lisiwe kali sana, nisirudi Dar es Salaam. Ahsante sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)