Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitakuwa nyumbani zaidi na ninavyozungumza nyumbani maana yake ninazungumza Kawe. Kwanza, nilitaka Mheshimiwa Waziri anisaidie, mwaka 2023 mlisema kazi ambazo mlitarajia zitakamilika 2023/2024, ni pamoja na kukamilika kwa Mradi wa Seven Eleven. Sasa leo unatuambia umefika 35% na mnatarajia kumaliza 2026. Kwa nini mwaka 2023 mlilidanganya Bunge? Ama Serikali hamjui mipango wala hamna mipango, mnafanya kwa kubahatisha!
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mradi wa Seven Eleven ilikuwa na vipengele viwili; kulikuwa kuna Seven Eleven One ambayo hii ni miradi iliyoanza kipindi cha Dkt. Jakaya, ikakwamishwa Kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ikafufuliwa kipindi cha Rais Mheshimiwa Dkt. Samia, ambapo ukwamishaji wake katika kipindi hicho cha Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli Mungu amlaze mahali pema Peponi, nchi ilipata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 199.9 kwa sababu kulikuwa kuna wakandarasi, kuna mikataba imeingia, mikopo na vurugu nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka tu tujue kwamba, Seven Eleven One gharama yake kipindi hicho ilikuwa shilingi bilioni 142, Seven Eleven Two ilikuwa shilingi bilioni 103. Sasa hivi mnatuambia kwamba Seven Eleven thamani yake ni shilingi bilioni 169. Sasa nataka nijue ni one ni two ama combined? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo nadhani nitalizungumza kwa urefu kidogo ni suala la migogoro ya ardhi. Taarifa ya Kamati, ukurasa wa 28 inasema kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi inayotokana na Serikali kushindwa kupima na kupanga maeneo mengi nchini. Kamati inaishauri Serikali iendelee kutoa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa tunasoma Hansard za Bunge kwa Mabunge yaliyopita, hili ni Bunge la Kumi na Mbili, Bunge la Kumi na Moja, na Bunge la Kumi, hii sentensi inaweza ikawa imejirudia kwenye Mabunge mengi zaidi kuliko kipindi chochote. Ndiyo maana mimi nilisema hapa, Bunge lile lililopita kabla ya mwaka jana 2023 wakati wa Bajeti ya Ardhi inawezekana kabisa ama watumishi wana maslahi kwenye migogoro, ama vigogo wa Serikali wana maslahi katika migogoro, ama vigogo wa chama wana maslahi katika migogoro. Ndiyo maana leo pamoja na ngonjera zote tutakazoziimba, Bajeti ya Wizara ya Ardhi imepungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana 2023/2024 matumizi mengineyo ambayo ndiyo Other Charges tunategemea yana-facilitate utendaji wa kazi wa watumishi ilikuwa shilingi bilioni 37.6, mwaka huu ni shilingi bilioni 36.6. Bajeti ya Maendeleo 2023/2024 ilikuwa shilingi bilioni 82, leo ni shilingi bilioni 70, unategemea nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maana yake ni kwamba, kuna mjumuiko wa pamoja wa hujuma, hii migogoro itokee, ili watu wazurure huko mtaani kujifanya wanasuluhisha kumbe wanatengeneza matatizo mengine. Kama tuna dhamira ya kusaidia hii Wizara, lazima tuoneshe kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, mwaka jana 2023 tarehe 03 mwezi wa sita nilizungumza namna ambavyo DDC (Dar es Salaam Development Cooperation) Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam, mimi nimekuwa Mbunge miaka 10 Kawe, sijui hili shirika linafanya nini? Kuna mgogoro mkubwa sana ambao unagusa majimbo mawili; Jimbo la Kibamba na Jimbo la Kawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu unahusu mitaa saba ya Kiserikali. Napongeza tu kwa hatua kidogo ambazo Waziri ameweza kuonesha, kama Waziri, well and good, lakini kwangu mimi naona kama vile ni katone kwenye Bahari ya Hindi iliyojaa mapapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtaa wa Msumi, kwa mfano, kwa ndugu yangu pale Kibamba kwa eneo ambalo DDC wanasema watachukua, linaloingia kwenye mtaa ni 57.3% ya Mtaa wa Kiserikali. Huu mtaa una pori la Serikali ambalo ni reserve, linatengeneza 32%. Maana yake wakichukua eneo, itabaki 10%, ndiyo wananchi wakabanane kule. Mtaa wa Tegeta A, kwa ndugu yangu wa Kibamba ni 26.7%. Mbopo, Jimbo la Kawe, 48% ya eneo la Mtaa wa Mabwepande ni asilimia tano, Madale ni 5.9%, Kilangwa ni asilimia mbili, Makabe ni asilimia 0.38. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu anaitwa DDC, anasema ana hati aliyoipata mwaka 1981. Uzuri ni wananchi tokea mwaka 1980, 1979 wako pale. Kijiji cha Mabwepande kimetangulia, DDC wanasema kweli, walileta maombi, lakini walipewa masharti ambayo hawakuyatimiza wakaenda wakatengeneza hati yao mezani, ndio wanasema tuna hati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo husika, lina shule 17, za msingi 13 na za sekondari nne. Kuna Kituo cha Mafunzo cha Kilimo cha Serikali, kuna zahanati tatu, kuna viwanda vitano, kuna vituo vya mafuta viwili, kuna taasisi za kidini 20. Pia kuna Ofisi za Serikali za Mtaa saba, kuna ofisi za chama chenu, sitaki kutaja hapa, ila mjue ofisi za chama chenu zipo za kumwaga. Yapo maeneo ya maziko matano, kituo cha kulea watoto kimoja na visima vya maji viwili. Hawa watu walipewa hati mezani, ndiyo maana leo unakuta Kijiji cha Mabwepande kimepanuka mpaka Kibamba. Najua Mheshimiwa Waziri ana busara, naomba busara yake imwongoze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hati, hawa jamaa kwanza inasemekana kuna hati tatu; kuna ya mwaka 1981, kuna ya mwaka 1983, kuna Hati ya mwaka 1984. Hati hii ya 1984 ambayo ndiyo waliitoa kwenye Kijiji, kipengele kinasema walitakiwa watumie ardhi kwa kilimo na ufugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakitaka kubadilisha matumizi wa-consult mamlaka. Leo miaka 43 baadaye, nilipokuwa Mbunge wa Kawe hawakuthubutu kuleta pua kwa sababu walijua watakutana na kifaa. Leo nimeondoka wanaenda kupeleka pua kutaka kudhulumu kaya za watu laki mbili hivi, ni haki hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ya nchi hii ni mali ya umma. Bahati mbaya sole fortunate wameandika barua kwa Makamu wa Rais mara mbili, nimezungumza hapa, mwaka 2023 wakati dada yangu Mheshimiwa Angela ni Waziri hapa na Naibu wake wanajua, wakapuuza, hawajachukua hatua. Wanatajwa, Mheshimiwa Waziri, watu wanasema kumekuwa na upotoshaji na udanganyifu unaoendelea kufanyika na Mwenyekiti wa Bodi ya DDC, yuko rafiki yangu hapa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Mbunge wa Kawe Gwajima, Mkuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamemwandikia Makamu wa Rais barua mbili wanalalamika, Dar es Salaam pale ni pua na mdomo na Wizara, Serikali iko wapi? Huwezi ku-ignore watu 200,000. Tu-assume wananchi wana tatizo, hivi kweli wewe umepata kahati kako mwaka 1981 hujaweka hata mbuzi, hujaweka hata kuku, hujaweka hata panya, miaka 43 baadaye unakuja unawaambia tu wananchi walipe pesa, for what? Simply because una-connection ndani ya Serikali! We cannot allow that. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jerry alikwenda kwenye Kliniki ya Ardhi, Bunju. Nikuhakikishie tu wananchi wale wana matumaini makubwa sana naye. Mara ya kwanza alienda alivyoitwa na mwenezi wao, kuna statement akaitoa kuhusiana na ule mgogoro, lakini nashukuru baadaye Waziri ali-revoke akaja akawasikiliza akaona kuna kitu. Naomba Waziri akasikilize hawa watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wamezungumza hapa, Waziri akawasikilize wananchi, asiwasikilize wapambe wanaomzunguka wanampotosha kwa sababu wao ni wanufaika wakuu wa hii dhuluma. Wananchi wamepewa Control Number ya kulipia, eti wanaambiwa viwanja, sijui nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwenye yale maeneo kuna watu pia ni wavamizi. Kwa hiyo, kuna lugha inatumika, ooh, kuna watu DDC wamekubaliana nao kuwalipa, wale ni watu ambao waliingia pale kudhulumu watu wengine ambao wameshinda kesi mahakamani. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Halima Mdee.
MHE HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wana foleni ya makubaliano na majambazi ili kuweza kuwanyima haki wenye haki. Namwomba Mheshimiwa Waziri, namwamini, Wakili, akawasikilize wananchi, kwani ana busara, tutamaliza mgogoro. Nakushukuru sana. (Makofi)