Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi jioni ya leo kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye Wizara yetu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Nami nianze kama wenzangu kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anaendelea kuyatekeleza majukumu ya Taifa hili kwa niaba ya Watanzania, lakini kwa jambo lililo Mezani kwetu, tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia Waziri na namna alivyoipanga timu yake ya Wizara ya Ardhi inavyoendelea kushughulika na matatizo ya wananchi na tunaona namna anakopita anavyoweza kufanya mambo mbalimbali na kumaliza changamoto mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi pia kwa Mheshimiwa Waziri na timu yake yote ya Wizara, naamini kwa kweli katika Wizara ile yupo dada yangu pale Lucy kwa kuwa ametokea Pwani najua nguvu na uwezo alionao juu ya kuzungumzia migogoro na naamini katika sehemu ya migogoro nitakayoizungumzia mingine yeye anaielewa vizuri zaidi. Kwa hiyo, namwomba yeye (Naibu Katibu Mkuu) amweleze vizuri Waziri ili aweze kusaidia kumaliza changamoto zilizopo Mkoa wa Pwani ambazo anazifahamu vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo waliochangia wakimwombea Mheshimiwa Waziri Ulinzi. Mimi niseme sisi Wabunge kwa niaba ya wananchi tuendelee kumwombea ulinzi wa Mwenyezi Mungu kwa sababu ulinzi wa mwanadamu siku zote una kikomo. Hata kama atapewa ulinzi wa namna gani, inawezekana mlinzi wake akasinzia na hayo ambayo tunapata mashaka nayo yakamkuta. Kwa niaba ya Watanzania sisi tulio hapa kwenye Bunge hili tuombe kwa kadiri tuwezavyo aweze kupata ulinzi wa Mwenyezi Mungu kwa sababu ukweli kabisa kazi ambayo anaendelea nayo kwenye majimbo yetu bila kumwombea hakika anaweza akapoteza mwelekeo na nguvu ya kupambana na matatizo ambayo anashughulika nayo ikapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo yote hayo ambayo nimeyasema, kwanza nitangulize ombi na ombi hili likiwa na sura ya kumkumbusha. Nakumbuka mimi na yeye tulikutana mara kadhaa, tulipanga ratiba ya kwenda jimboni, ilikuwa tarehe 09 lakini baada ya kukutana na majukumu ilishindikana. Ombi lile Mheshimiwa Waziri bado nalileta kwako nikikuomba sana sana sana ndugu yangu tuiweke vizuri ratiba ya kwenda Pwani na hasa katika Jimbo la Kibaha Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niseme kidogo, pia ndugu yangu wa Chalinze nilipomwambia nitachangia eneo hili akaniambia naomba umkumbushe atakapokuja Pwani asikose kufika Mbala. Ufike na pale Mbala ukamsaidie na lile tatizo ambalo na yeye linampa shida muda mrefu sana. Pia nakuomba, kwa sababu ulipanga siku moja kwenye haya maeneo mawili, ikiwezekana jitahidi sana kila jimbo lipe siku yake. Maana yake mzigo uliokuwa katika Kata ya Kikongo au katika Jimbo la Kibaha Vijijini siyo mzigo mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba Mheshimiwa Waziri atakapotoka kwenda pale kwa ajili ya kushughulikia, akatoa siku moja kwa maana ya majimbo mawili na uzito wa mambo yalivyo, inawezekana akapata rasha rasha. Mimi nataka aende akawasikilize Watanzania wa maeneo yale ya Kikongo kwa sababu kuna migogoro mbalimbali inatoka kwenye kata karibu tano au sita za jimbo langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Mtemvu hapa alipokuwa anachangia nikagundua kumbe na huyu naye ninaye kule. Kwa hiyo, namna alivyochangia ameigusa Kata ya Kikongo na ameeleza hali ambayo anaijua, nafikiri ni vizuri Waziri akaja kutusaidia. Baada ya eneo hili la kwanza ambalo nililitenga kama eneo la shukurani, na kuomba hali ambalo nimeomba, kwanza nitangulize maneno ya kwamba naunga mkono hoja kabla sijaanza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yangu ya kuchangia ambayo leo nimejipanga nayo ni maeneo yafuatayo: Kwanza kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameonesha majukumu ya Wizara katika kushughulikia migogoro, lakini ameanza pia kuzungumzia kwamba wanashughulika na suala zima la upimaji na umilikishaji wa masuala ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili pamoja na Mheshimiwa Waziri, naomba mfahamu kwamba kwa kadiri ambavyo mmeweza kutambua kama hii ni sehemu moja ya jukumu lenu, nafahamu kwamba suala zima la upimaji linakuwa chini ya Mabaraza ya Halmashauri, lakini tunafahamu kabisa tunapopewa hili jukumu la kwamba halmashauri zinatakiwa zipime na zipange ni katika suala zima tu la kutambua maeneo, kuwatumia wataalamu ambao wanatoka Wizara ya Ardhi waliokuwa ndani ya halmashauri husika, lakini pia kwenye utoaji wa maamuzi ya hapa pafanywe nini na hiki kifanywe nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zote za ardhi ni za kitaalamu, zinahitaji watu kutoka kwenye ofisi yako. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na jukumu hili kuwa linafanyika kwenye ngazi zile, ahakikisha analitupia jicho kwa sababu hapo ndipo panapoanza migogoro. Unakuta watu wanatambua maeneo, wanayapanga, lakini kwenye matumizi ya upangaji ambao umekusudiwa unakwenda ndivyo sivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ndilo linalopelekea migogoro mingi ambayo inasababisha sasa Waziri hata sasa ashindwe kuwa na utulivu. Kila jimbo wanamhitaji yeye mtu mmoja; na hii ndugu yangu Waziri ni namna gani Watanzania na Wabunge wana imani na wewe na ofisi yako na siyo mtu mwingine yeyote. Kwa hiyo, jitahidi kutoa maelekezo kwa watu wanaokusaidia wafanane na wewe angalau kwa robo tatu ili waweze kupunguza kasi ya matatizo na wakupe muda wa kuweza kushughulika na masuala mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivi kwa sababu gani? Tuna tatizo au suala zima la urasimishaji. Wananchi wanamiliki ardhi, tumetoa wenye sera ya kuzungumza kutakuwa na masuala ya urasimishaji kwenye maeneo ya miji ambayo haijapangwa. Tumetoa kibali kwa kampuni zifanye hizo kazi za kuwapimia watu na kuwapanga vizuri kwenye maeneo ya miji ambayo hayajarasimishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jimbo langu hasa katika Mji Mdogo wa Mlandizi kuna kampuni zimepewa majukumu ya kufanya jukumu hilo wameingia mitini, kwa lugha ya sasa. Wamewafanyia kazi nusu wananchi, ramani hazijulikani ziko wapi? Hawajui wamefika hatua gani, na wananchi wametoa pesa. Sasa tunaomba mtusaidie kututafutia hawa watu ambao walipewa dhamana ya kuja kufanya zile kazi wakazimalize na kama hawawezi kufanya hivyo, basi ofisi yako Mheshimiwa Waziri ione namna gani inaweza ikafanya jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kwenye suala zima hilo la upimaji na umilikishaji, nashukuru kwenye jimbo langu kuna jiji linaitwa Jiji la Kwala. Baadhi ya vijiji vimetambuliwa ambavyo vinakwenda kulitengeneza hilo Jiji la Kwala, lakini Mheshimiwa Waziri kazi ambayo imefanywa ya upangaji na upimaji kwenye eneo lile ukiangalia kwa haraka haraka tumekwenda kufanya kazi kwenye kipande ambacho wawekezaji wanaenda kuwekeza lakini watu walio jirani na maeneo hayo kazi hiyo haijafanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Jiji la Kwala tunapokwenda kupima maeneo tu ya viwanda lakini eneo la viwanda au eneo la uwekezaji jirani yake wapo wananchi wanaishi ambao nao ni vema wangeweza kupangwa vizuri mapema, kwa sababu tunapopanga kipande kidogo na tunatarajia liwe jiji, tutegemee kuweka mazingira ambayo siyo rafiki sana kwenye eneo ambalo linapakana na maeneo hayo. Nasema hivi kwa sababu gani? Kwenye Eneo la Kwala ambalo tumepanga kama eneo la jiji tumepima maeneo ya wawekezaji lakini bado kuna migogoro mikubwa ya ardhi. Wananchi wanaokabiliana na eneo hilo wapo wanaolalamika kwamba wako ndani ya eneo hilo. Sasa ni vizuri tufanye upimaji na tupange na kuvishirikisha vile vijiji vyote vya jirani vipangwe kwa pamoja ili visiharibike tena kwa sababu tunatarajia uje kuwa mji, na tukifanya hivyo tutakuwa tumemaliza migogoro mingi ambayo tunaizungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala zima la upangaji wa ardhi na matumizi bora ya ardhi. Vijiji vyote kwenye maeneo ya nchi hii, kwa mfano Jimbo langu la Kibaha Vijijini, vijiji vingi vilipangwa; wakapanga matumizi bora ya ardhi. Wakatambua wapi watakaa wafugaji, wapi watu watalima, wapi watu watawekeza viwanda, lakini cha kusikitisha, upangaji huu hausimamiwi na hausimamiwi kwa sababu gani? Anatokea mtu anataka kuwekeza kwenye eneo ambalo siyo lililopangwa kwa shughuli fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi wa Wizara ya Ardhi wanaridhia kazi hiyo ifanywe tofauti na kilichokuwa kimepangwa. Jambo hili linaleta mgogoro mkubwa sana. Limesumbua kwenye Kata ya Ruvu na limepelekea mpaka kuwepo na mgogoro wa mpaka wa kata na kata kwa sababu hawakuheshimu mpango wa kijiji kimojawapo. Kwa hiyo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri haya mambo yakaangaliwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo nataka nichangie ni utatuzi wa migogoro. Hapa nitagusa kidogo eneo ambalo ndugu yangu Mheshimiwa Mtemvu amelizungumza. Eneo hili la migogoro tunajua tuna vyombo vinavyoshughulika na utatuzi wa migogoro ya ardhi. Kwanza, tunayo Mabaraza ya Ardhi lakini pia tuna Makamishna wa Ardhi ambao ndio wanaweza kutusaidia kufanya hizi kazi lakini sasa hivi tunajua kabisa viongozi kwa mamlaka yao ma-DC na Wakuu wa Mikoa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Mwakamo muda wako umeisha.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja nimalizie.
MWENYEKITI: Tafadhali hitimisha.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi pamoja na kusema haya, nimalizie tu kukuomba Mheshimiwa Waziri hii migogoro ambayo ameizungumza ndugu yangu, Mheshimiwa Mtemvu ambayo yote iko kwangu nakuomba unipangie ratiba nzuri twende tukaimalize kwa sababu Kikongo siyo pazuri panatuondolea amani na hali tutakayokwenda nayo mbele ambayo unaifahamu yote, siyo jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, nilishasema naunga mkono hoja na narudia tena naunga mkono hoja, nakushukuru. (Makofi)