Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye Wingi wa Rehema, alienijalia afya ya kusimama katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza naomba niunge mkono hoja. Baada ya kuunga mkono hoja naomba nichukue nafasi hii nami niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Jerry kwa kazi nzuri anayoifanya. Tumeshuhudia maeneo mengi amekuwa akifanya kazi nzuri ya kuwasaidia Watanzania, kuwatetea wanyonge na kurudisha haki za watu walioporwa haki zao. Hongera sana Mheshimiwa Jerry kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuwatumikia Watanzania. Pia naomba nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaongoza na kuwatumikia Watanzania. Hakika mama huyu amekuwa ni mkombozi wa Watanzania. Kwa hiyo, tunaomba tuendelee kumwombea Mwenyezi Mungu amjaalie afya aendelee kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajielekeza katika hoja moja tu, hoja ya migogoro ya mipaka katika maeneo mbalimbali. Migogoro ya mipaka imekuwa ni kilio kikubwa kwa Watanzania na hata ukiangalia kwenye jamii zetu watu wengi na hata wengine wanapelekea kuuana kutokana na mipaka ya ardhi. Kwa hiyo, ni namna gani unaweza kuona mipaka inavyoweza kuondoa amani kwa watu mbalimbali na hata kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika, ardhi haiongezeki kabisa kabisa na kwa hivi sasa badala ya kuongezeka ardhi inapungua. Ukiangalia mafuriko ya mwaka huu yameweza kumega ardhi kubwa kwenye mito, mito imemega ardhi, maziwa yamemega ardhi lakini vilevile bahari imemega ardhi kwa maana hiyo ni ukweli kabisa ardhi haiongezeki lakini watu wanaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Watu wanaongezeka na mahitaji yanaongezeka. Kwa mfano, kwa sasa hivi ukiangalia wanafunzi wanamaliza vyuo wanaelekea mitaani, vijana wanaotoka jeshini wakimaliza vyuo wanaelekea mitaani. Huku kwingine ajira inapungua, ajira pekee iliyobaki ni kwenye kilimo na huko huko kwenye kilimo ndiyo huko sasa ardhi haitoishelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimekuja na kilio cha kuiomba Serikali iongeze kasi ya kupima ardhi na kuweka mipaka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Jerry kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kabisa naomba kazi ya kuwatumikia Watanzania kwa kupima ardhi na kuweka mipaka iweze kufanyika ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yetu ya Kasulu upo mgogoro wa muda mrefu katika eneo la Kasulu DC, Kijiji cha Kagera Nkanda, Mvinza na Katoto. Huko kuna migogoro ya muda mrefu sana na mara ya mwisho nilitembelea vijiji hivyo mwezi wa Tisa. Wananchi wale waliniomba Waziri uweze kufika. Hivyo Mheshimiwa Waziri katika ratiba yako nakuomba sana na ninakusihi upange ratiba uweze kufika Kagera Nkanda Mvinza na huko kwingine ili uje ufanye mikutano. Tena naomba uitishe mikutano uwasikilize wananchi, ukishawasikiliza naamini utasema neno moja tu watapona, kwa sababu kilio chao ni kutaka kuwekewa mipaka ili waendelee kufanya shughuli zao za uzalishaji wa kilimo wakiwa na amani kuliko ilivyo hivi sasa unakuta ni migogoro ya ardhi na wakati mwingine wakilima mazao yao yanachomwa na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mheshimiwa Waziri nirudie tena, naomba ufike Wilaya ya Kasulu, utakapokuja uje Kagera Nkanda, Mvinza na Katoto. Nafahamu ni mbali sana kufika katika vijiji hivyo na wakati mwingine unapita wilaya nyingine na watu wanaweza wasikupeleke kule wakakwambia Mheshimiwa kule hakufikiki, wewe bado ni kijana, fanya linalowezekana ufike kwenye maeneo hayo ambayo hayafikiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)