Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii nami niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Ardhi. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kuendelea kuhudumia nchi yetu kikamilifu. Nawapongeza pia Wizara chini ya Mheshimiwa Jerry Silaa kwa kazi ambazo tunaona zinaendelea. Kwa kweli Wizara inaendelea kuonyesha mabadiliko makubwa, kwa hiyo, tuendelee kumpa moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kazi anazozifanya Mheshimiwa Jerry Silaa pamoja na watendaji wa Wizara hii na wote wanaomsaidia kwa ujumla. Kikubwa tuendelee kumpa moyo kwamba hiyo ndiyo kazi aliyopewa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wewe utajiombea peke yako lakini yale machozi ya Watanzania ambayo unakwenda kuyatoa kwa furaha baada ya kudhulumiwa maeneo yao kwa miaka mingi yatakuwa ni maombi tosha kwako na wenzako wanaokusaidia. Endelea kufanya hivyo kwa sababu dhamira ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona migogoro na dhuluma zote za wananchi wake zinaondolewa. Wewe na Wizara yako ndiyo umepewa dhamana ya kuweza kupanga vizuri matumizi ya ardhi katika nchi hii. Kwa hiyo, wewe endelea kufanya hivyo, sisi pamoja na Watanzania wengine tutaendelea kushuhudia yale ambayo unayafanya, lakini Mungu atakubariki kwa yale ambayo unayafanya kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauri mwaka 2023 juu ya upimaji wa ardhi katika nchi yetu, na unakumbuka tuliongea maneneo mengi ya kushauri. Tumeona namna ushauri unachukuliwa. Nimeangalia hapa Tume ya Mipango ya Ardhi ya Taifa, Serikali imewapa fedha kwa 100% nao wamefanya kazi kwa zaidi ya 100%. Hii inaonyesha kwamba tunao watendaji wazuri, wakipewa rasilimali za kutosha watatufikisha pale tunapotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023 walipangiwa kupanga vijiji 210. Mpaka kufikia Juni, wamepima vijiji 339. Hii inaonyesha hata ukimpa fedha anazozihitaji shilingi bilioni 22 ili aweze kutupimia vijiji ambavyo kwa mwaka wana uwezo wa kupima vijiji zaidi ya 1,000, tukimpatia fedha hizo, maana yake atakuwa na uwezo wa kupima vijiji 1,640. Atachukua muda wa miaka mitano na miezi sita kukamilisha vijiji vyote 8,000 na zaidi vilivyobaki. Gharama ya vijiji vyote kama atapewa fedha kuvipima vyote, anahitaji shilingi bilioni 22 kila mwaka kwa miaka mitano, kutukamilishia upimaji wa vijiji 8,194. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona mambo haya siyo magumu kiasi hicho? Serikali imefanya mambo makubwa ya fedha nyingi. Suala la kupanga nchi ni suala la kuondoa migogoro, jambo litakalowafanya wananchi kujipanga vizuri katika nchi yao, kufanya shughuli zao za kiuchumi bila bugudha na mwingiliano wa idara nyingine na wananchi. Tusipofanya hivi Mheshimiwa Jerry Silaa ataota mvi mpaka kwenye nyusi za kwenye macho. Migogoro itaendelea kuwepo na kuwepo bila mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iwape Tume ya Mipango, hiyo shilingi bilioni 22 wapime vijiji 1,460 kwa mwaka ambapo baada ya miaka mitano na miezi sita suala upimaji na upangaji wa ardhi tutakuwa hatuliongei tena katika Bunge hili. Kwa hiyo, tunaomba tena Serikali ifanye hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongelea ule mkopo wa shilingi bilioni 300, tukasema, katika fedha hizo ukiwapa hawa watu wa ardhi shilingi bilioni 100 na zaidi wanamaliza kesi yote. Kwa hiyo, ajenda hii ya kuongelea Bungeni muda wote masulala ya kupanga nchi itakuwa imeisha na itakuwa ni sifa kubwa kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na itakuwa ni sifa kwa nchi na itakuwa ni sifa kwa Bunge letu, pia tutakuwa tumetekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa uhalisia wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali ifanye hivyo, kwa sababu tazama katika ule mradi wa LTIP mpaka leo umeweza kupima vijiji 843. Kwa hiyo, kumbe tukiwapa nguvu Tume na hiyo miradi ya pembeni, hata hiyo miaka mitano haiwezi kufika. Haifiki. Kwa hiyo, tusaidie jambo hili liweze kwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu kule kwangu kuna mgogoro ule wa Mongoroma ambao kidogo juzi ulileta taharuki hapa. Mgogoro ule ni mdogo sana, Wizara ya Ardhi inatakiwa itupe elimu watumiaji wa ardhi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sekunde kadhaa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara nyingine zote na wananchi ni watumiaji wa ardhi, kwa maana hiyo, mtu ambaye atasimama na kuweza kusababisha tukapatana ni Wizara ya Ardhi. Sisi hatuwezi kuwa tuna mgogoro, wananchi wana mgogoro na Wizara ya Maliasili halafu Maliasili ndiyo wakautatua ule mgogoro. Ni jambo ambalo haliwezekani. Wote ni waathirika, anayeweza kutatua mgogoro ule ni Wizara ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanasema wamepeleka vigingi, wameshaweka vigingi kwenye maeneo ambayo wananchi wana kesi nao zaidi ya miaka 30. Maana yake kaamua tu yeye mwenyewe bila kushirikisha wananchi. Sasa hapa suluhisho litapatikana kwa wewe Mheshimiwa Jerry Silaa kufika Mongoroma haraka iwezekanavyo ili tumalize ile issue, na kikubwa zaidi ni agizo la Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba ufanye jambo hilo, ufike mpaka Mongoroma. Kondoa hapa ni saa moja tu umefika, mkutano wa saa moja, saa tatu uko zako Dodoma unaendelea na shughuli zako. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jerry Silaa utakapokuja kuhitimisha uniambie ni lini tunafuatana kwenda kuwasikiliza wananchi wangu wa Mongoroma? Wana hamu sana na wewe ili waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wale wanashindwa kufanya kazi zao, wanashindwa kujenga majengo mazuri, wamecheleweshewa shughuli zao za kiuchumi miaka mingi, walishakuwa na kesi mahakamani, wakaona wanapoteza gharama, wakaachana na kesi hizo, leo tunasubiri maelekezo ya Rais ili wananchi wangu waweze kuwa na maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule ni mji siyo vijiji, ile ni mitaa, sasa kama ni mitaa sisi hatuhitaji mtuongezee eneo, tunahitaji mtoe vigingi vyenu mlivyoviweka kwenye maeneo ya wananchi, mpeleke kwenye hifadhi, sisi wananchi tutawasaidia kulinda hifadhi yetu baada ya kukubaliana kutoa vile vigingi vyenu kuweka kwenye eneo lenu ambalo tunaliheshimu na tunalifahamu na wananchi wanaliheshimu na wanalifahamu. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeisaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, Mheshimiwa Waziri mwende mkamalize ule mgogoro wa mpaka uliopo kati ya Dodoma na Manyara kule Kondoa. Ule mgogoro msipoangalia vizuri unaweza ukaleta maafa baadaye. Kwa hiyo, jitahidini kwa sababu tayari mmeshafanya kazi kubwa, kazi iliyobaki ni ndogo. TAMISEMI walishawaandikia namna ya kufanya kwenda kupima vile vijiji vitatu ambavyo viliingia Dodoma, mkamalize, mkaainishe ili wale watu waishi kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wahifadhi wa Mkungunero leo wana maeneo wanaogopa kwenda kulinda rasilimali za nchi kwa sababu wananchi wanawatisha na silaha za jadi. Ili kuondoa hilo, wananchi waonyeshwe kwao na wanyama waonyeshwe kwao mpaka uchorwe, ueleweshwe, mtangaze kesi iishe. Wote ni Watanzania, atakayeishi Dodoma aishi Dodoma, atakayeishi Manyara wote ni Watanzania wale wale, kwa maana hiyo, tunataka hilo mlifanye na Mungu awatie nguvu, awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)