Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii iliyoko mbele yetu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anaendelea kuwapigania wananchi wake wa Tanzania kuhakikisha kwamba wanamiliki ardhi na migogoro inapungua au inaisha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wenzangu walivyosema, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya, wote tumeona, Naibu Waziri na viongozi wote ambao wanakusaidia kazi ikiwemo Katibu Mkuu, Injinia Sanga na Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote, kwa sababu bila ushirikiano madhubuti haya yote mazuri ambayo leo tunayasema na kuyapongeza, basi yasingetokea. Nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Muhambwe, naishukuru Serikali na wewe mwenyewe Waziri na Kamishna wa Ardhi kwa jinsi ambavyo na mimi nimefaidika na urasimishaji ulioboreshwa kwa kutengenezewa hati katika vijiji vyangu vya Kisogwe na Busunzu. Kwa kweli kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Busunzu tunakushukuru sana. Kwa vile umetuonjesha vijiji viwili tu ilhali tuna vijiji 50, basi naiomba Serikali iliangalie jimbo hili la Muhambwe ili nasi tuweze kufaidika na kupangiwa ardhi yetu ili nasi wananchi wetu waweze kupata hati na kuweza kufaidika na hii keki ya Serikali ya kufanya ardhi yao iwe na thamani baada ya kupatiwa hati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, pamoja na mazuri yote yaliyoongelewa nina machache ya kuchangia kwenye hotuba hii. Ukurasa wa tisa wa hotuba yako umeongelea ukusanyaji wa maduhuli. Ni ukweli usiopingika kwamba ukusanyaji wa maduhuli umeshuka, mlijipangia kukusanya shilingi bilioni 300 lakini mmekusanya shilingi bilioni 136 sawa na 45% ya makusanyo. Mwaka huu nimeona mmejipangia kukusanya shilingi bilioni 250. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sababu iliyochangia kushuka kwa ukusanyaji wa maduhuli ni tamko la Wizara ya Fedha kusema makusanyo hayo yahamie TAMISEMI. Hii imeleta taharuki na imeleta kutokufahamu na imekuwa iko kwenye dilemma kwa sababu sasa pesa haikuweza kukusanywa vizuri. Naomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha, waliangalie hili tamko na kulibadilisha ili Wizara ya Ardhi iendelee kukusanya haya maduhuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu kwanza ni jukumu lao la kisheria kuweza kukusanya haya maduhuli, pia, Wizara ya Ardhi ndiyo ina watumishi ambao wamesomea ardhi, wanafahamu taratibu za makusanyo hayo ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe, Serikali imeshaweka pesa nyingi sana kutengeneza mifumo kwenye Wizara yetu ya Ardhi. Tunao mfumo wetu wa ILMIS ambao umeunganishwa pamoja na mfumo wa ukusanyaji wa pesa ambao unaandaa taratibu zote za upangaji, upimaji, uthamini na umilikaji wa ardhi. Kwa hiyo, mfumo huu uko kwa pamoja ukifanya kazi zote za ardhi ikiwemo kukusanya kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Ardhi ndiyo ina ile kanzidata ya nani anamiliki nini? Nani anamiliki wapi? Nani anapaswa kulipa nini? Kwa hiyo, kwa sababu zote hizi muhimu ambazo Wizara ya Ardhi inazo, naomba niishauri Serikali iliachie jukumu hili Wizara ya Ardhi, iendelee kukusanya hayo maduhuli ili hata hili lengo walilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 250 liweze kutimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tumempongeza Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo anaendelea kuziweka vizuri Kliniki za Ardhi. Tumetembelea kliniki mbalimbali anazokwenda, zile kliniki ziko katika ukweli na uwazi. Ni kweli kabisa imekuwa faraja kwa Watanzania ambao wamedhulumiwa kwa muda mrefu, Mheshimiwa Waziri amekwenda kurudisha furaha, amekwenda kurudisha mali zao zilizopotea. Takwimu hazisemi uongo, amesema ameshughulikia migogoro zaidi ya 7,000 na katika hiyo 4,500 ameweza kuimaliza na hii 2,000 inaendelea kufanyiwa kazi. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hiyo migogoro aliyoitatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri leo yupo kesho hayupo, iko sababu ya makusudi kabisa ya kuweka mfumo wa kitaasisi ambao whether Jerry yupo au hayupo, mtu yeyote atakayekuja pale basi kuwe na mfumo maalum wa kuweza kufanya hii migogoro iweze kutatulika badala ya kusimama mmoja au kusimama watu wenye nia njema au nzuri, wachache wakabaki hawafanyi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba pamoja na kuwa wanafanya kazi vizuri sana, bado wako watendaji wachache ambao hawajaelewa nini Mheshimiwa Rais akiongelea kuhusu 4R. Bado wanafikiria tuko wapi sijui, kwa maana bado wanadhulumu wananchi na bado wanakula rushwa. Kwa hiyo, kama Serikali itaweka mfumo wa kitaasisi ambao utashughulikia hii migogoro ya ardhi, basi tunaamini kabisa shida ya Watanzania na migogoro itaisha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongezea kwenye suala hili la migogoro, wote tunafahamu jinsi gani wananchi ambao wana migogoro ya ardhi wanapata shida sana kwenye taasisi zetu za kisheria. Kipo kivuli cha kusema migogoro ya ardhi ni kosa la madai, kwa hiyo, linachukuliwa kama kosa light sana. Ndiyo maana tunaona wako matajiri ambao wao wamekuwa sasa maarufu na umewaonesha hadharani jinsi gani wao ndio miamba wa ku-forge documents na hati kwa sababu wanajua hata wakienda Mahakamani, hilo ni kosa la madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kosa hili basi hizi taasisi iangalie jinsi gani inaweza ikaliweka ikawa ni kesi kali na likachukuliwa kama ni kesi za jinai ili hawa watu wanaofanya haya matatizo, basi waogope kufanya uvamizi wa hizi mali za wananchi. Wajue kwamba wakienda kwenye hizi taasisi, basi sheria kubwa itachukuliwa ili waweze kuacha kabisa hayo matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala ambalo limekuwa ni changamoto sana katika Bunge hili na Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakiendelea kulalamika, nalo ni juu ya fidia. Wizara ya Ardhi imepewa dhamana ya kufanya uthamini wa maeneo mbalimbali ambayo Serikali au taasisi inataka kufanya uwekezaji. Wizara imetimiza jukumu lake vizuri sana chini ya dada yetu Evelyne kuwasaidia hawa ambao wanataka kuwekeza au kufanya mradi pale kuweza kupata uthamini ambao ni halali ili Serikali na wananchi waweze kufaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko changamoto moja ya kucheleweshwa kulipa fidia ilihali mradi unaendelea kutekelezeka. Wengi wamesema hapa, kule kwetu Kigoma uwanja wetu wananchi wameshaambiwa wasiendeleze, lakini hawajalipwa fidia. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hili na kuamua kuja na Waraka Na.1 wa 2024 kwa ajili ya uthamini ambao utasimamia taratibu nzima za uthamini wa hizi mali kabla ya uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuja na waraka ni jambo moja, lakini kuutekeleza waraka ni jambo la pili. Pia kuja na waraka ni jambo moja lakini kuusimamia waraka huu ni jambo la pili. Naiomba Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Waraka huu usimamiwe vizuri sana. Hamna sababu ya Wizara ya Ardhi kuhangaika na kufanya uthamini ilhali Serikali au taasisi inayotaka kuwekeza au inayotaka kujenga mradi haina pesa ya kuwalipa wananchi. Mwananchi anaambiwa baada ya miezi sita tuta-review lakini hilo jambo halitekelezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanalia na wanalalamika kwani wameshapisha miradi lakini hawajalipwa pesa. Mheshimiwa Waziri nakuomba, huu Waraka umeutengeneza ili uweze kuleta tija kwa wananchi wetu wa Tanzania, basi usimamiwe kimadhubuti kuhakikisha kwamba kabla ya uthamini, taasisi au Serikali ijiridhishe na kuthibitisha kwamba inazo pesa za kuwalipa hawa wananchi ili baada ya uthamini, basi wananchi hawa waweze kupata pesa yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wenzangu wote waliosema kwamba mwarobaini wa hii migogoro ni kutengeneza matumizi bora ya ardhi ya nchi yetu na kuipanga nchi yetu ili kuhakikisha kila mtu anamiliki kipande chake. Wote wameonesha ukubwa wa hili tatizo kwa sababu wote tuna migogoro katika majimbo yetu. Migogoro ya wakulima na wafugaji ni matatizo ambayo yako karibu kila jimbo na yote yanatokea kwa sababu nchi yetu hatujaipima kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa katika taarifa zao, ni 33% ya nchi hii tu ndiyo imetengenezewa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Hii ni kama vijiji 4,000 hivi tu. Kwa hiyo, naiomba Serikali, kama Mheshimiwa Waziri ambavyo amekuwa akisema kila siku, tunahitaji shilingi bilioni 120 kuweza kuipima nchi yetu. Basi Serikali iweke nia ya dhati kabisa ya kuipatia Wizara hii shilingi bilioni 121 ili tuweze kuipima nchi yetu ili kuweza kupunguza migogoro ya ardhi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)