Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia hoja iliyopo Mezani. Awali ya yote naanza kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, natumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyochukulia mambo yote ya kisekta kwa maslahi mapana ya Watanzania. Hata katika hii Wizara kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Waziri, yeye alipewa shilingi bilioni 450 kwa ajili ya kulipa madeni ya kandarasi na miradi. Hiyo inaonesha namna alivyo na dhamira njema ya kuondoa kero na migogoro ya ardhi iliyokuwepo kabla yeye hajaingia ama inayoendelea kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Jerry. Mheshimiwa Halima Mdee wakati anachangia alisema kwamba anatambua Mheshimiwa Jerry ana hekima. Sasa mimi nikawa najiuliza, wale waliokuwa wanasema Mheshimiwa Jerry ni mzee waliangalia nywele zake, lakini wengine wakasema ni kutokana tu kwamba pengine ana matatizo mengi, lakini kumbe ni kutokana na hekima ndiyo maana nywele zake pia zimekuwa ni mzee wa hekima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nampongeza kwa sababu, hata kwa hii kliniki aliyoianza imeonesha manufaa makubwa sana na watu wamekuwa wakiikimbilia na hivyo ina tija na ina matokeo ya papo kwa papo. Hongera sana, hata kama tunakutwisha uzee, natambua kwamba wewe sio Mnyamwezi, lakini mzigo huu Mheshimiwa Rais alikuamini nasi tunakuamini. Endelea kuchapa kazi na wewe ndio Mnyamwezi kwenye eneo la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri maeneo machache. Kwenye kazi alizopanga Mheshimiwa Waziri 2024/2025, mkazo umewekwa kwenye kupanga ardhi. Hapa tunaomba aongeze kasi kweli kweli na hii imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani. Mimi naona katika kupanga ardhi pale atakapofanya upimaji, hiyo ndiyo tutakuwa sasa tumezingatia lile eneo la matumizi bora ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa itapunguza gharama ya miradi kwenye sekta nyingine. Kwa mfano, kuna kipindi nilichangia huku kwamba wakati mwingine tunakuwa kama hatusomani, lakini utaona kabisa kuna wananchi wanaanzisha makazi mbali kabisa tofauti na wananchi wengine waliko. Wale wanahitaji baadaye wapelekewe huduma za msingi kama vile afya, maji, na shule shikizi zinazojengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tungekuwa na matumizi bora ya ardhi na maeneo yaliyopimwa kama ambavyo ameweka kama ni kipaumbele chake cha kwanza, ina maana gharama za kwenye sekta nyingine za kujenga shule shikizi, kujenga miradi ya maji ya kuwafuata wananchi watano ambao wamejitenga kabisa tofauti na makazi ya walio wengi, gharama nyingine za afya, zahanati zile za muda na kadhalika zingepungua kwa sababu, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi, wananchi wengi walioko maeneo fulani wanatakiwa wapelekewe huduma za kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, eneo hili la kupanga ardhi kwa maana ya kupima, sisi kule kusini utakuwa umetusaidia sana. Sasa hivi wananchi kule tunaona kuna migogoro ya wakulima na wafugaji. Kama ardhi yote ingekuwa imepimwa, wale wafugaji hatusemi ni watu wabaya, lakini kwa vile wanaenda kwenye maeneo ambayo hawajatengewa wao kwa ajili ya kufuga na ndiyo migogoro inapoanzia. Kwa hiyo, hilo nalo lingekuwa limepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa suala la matumizi bora ya ardhi ni la msingi kwa sababu, tunaona hata kule kwenye Wizara za kisekta lipo lakini halisimamiwi vizuri. Tumeona hata wale Kamati ya Maafa ambayo tumeitungia sheria hivi karibuni, lile jambo la kudhibiti maafa pia litawezekana kama matumizi bora ya ardhi tutakuwa tumezingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo naomba nishauri ni kuwa na land bank. Ni muhimu sana kuwa na maeneo tunayoyapima na tusiyatumie kwa miaka 50 – 100. Najiuliza leo, ingekuwaje kama hapa Dodoma kusingewekwa akiba ya ardhi kwa ajili ya kujenga majengo ya Serikali? Tunaona yalivyojipanga pale vizuri, ni kwa sababu waliofanya hivyo waliweka hiyo akiba na ndiyo maana Serikali imeweza kuhamia na yale maeneo yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila eneo likiwa linavamiwa tu kiholela, haitafaa. Ni muhimu kuweka land bank na hayo maeneo yasiuzwe kwa ajili ya masuala fulani muhimu ya kimkakati ambayo yatakuja kutusaidia baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, unatambua Idara ya Ardhi imehamishiwa Wizara ya Ardhi, lakini ni tofauti na TARURA na RUWASA ambapo tunaona wao mambo yao yanakwenda vizuri. Idara ya Ardhi, sawa wako kule, lakini wakienda kwa Mkurugenzi kuomba karatasi tunajua hawapati, wakienda kwa Kamishna OC hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tnatambua kazi kubwa anayoifanya, lakini Idara za Ardhi zilizopo kwenye halmashauri kwenye Serikali za Mitaa kule ambapo bado wengine wanaendelea kutumia zile ofisi, OC ni ngumu. Kwa hiyo, nao ni vizuri sasa, ili wale walioko kule wapime, na kushughulika na migogoro ya mipaka ya wilaya na wilaya ama vijiji na vijiji, ni vizuri wajengewe uwezo kwa maana ya kuwa na vifaa, pia hata hizo stationery ili waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwenye hotuba yake amesema ujenzi wa jengo la biashara pale Masasi utaanza kwa bajeti hii ya 2024/2025. Tunamshukuru sana, na pia tunamshukuru pia sana Mheshimiwa Rais wetu. Sasa kuna madai ya fidia Uwanja wa Ndege Masasi. Uthamini ulishafanyika na imeshaenda kwa Mthamini Mkuu wa Serikali na wananchi wanaendelea kuwa na matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sasa, kabla ya Uwanja wa Ndege haujaamua kuchukua kipande kidogo kwa ajili ya kuanza shughuli zake, ni muhimu suala la fidia likawekwa vizuri, wananchi wale wakafidiwa ili shughuli zote ziendelee na wananchi kwa kweli wana matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amekuwa akitibu kwenye maeneo mengine, ni imani yetu pia Masasi atatufikia, na fidia ile wananchi watalipwa, hivyo shughuli ziendelee kama vile tunavyoendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa kazi inaendelea, na iendelee maeneo mengine kote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala dogo sana ambalo nilikuwa naomba na lenyewe ni muhimu pia. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza huku kuhusu migogoro ya mipaka. Maeneo mengine kuna mgogoro wa mpaka kati ya mkoa na mkoa, wilaya na wilaya lakini wakati fulani unakuta migogoro kati ya kijiji na kijiji. Sasa hii kwa kweli siyo ya kumtoa Mheshimiwa Waziri Wizarani aende kule kwa sababu nchi yetu ni kubwa. Ni vizuri tu akatoa mwongozo na wale walioko kule kama ni suala la kwenda kutoa elimu, wakaenda wakaifanya ili wananchi waendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii migogoro wakati mwingine unaiona inatokea kwa msimu. Kwa mfano, katika maeneo ya uzalishaji kama kule kwetu, kipindi cha korosho unakuta sasa ndiyo mgogoro. Kwa sababu gani? Kwa sababu unajua upo ule ushuru ambao ndiyo pengine halmashauri za vijiji zimekuwa zikigombea. Kwa hiyo, ni vizuri hili likawekwa sawa ili kwa kweli kila mwananchi, kila Halmashauri ya Kijiji eneo lilipo, kwa mfano kama ni mgogoro wa kijiji na kijiji, ikatambua maeneo yake na ikaondoa hizo hali za sintofahamu ili kazi za wananchi ziendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi, siyo vyema nikagongewa kengele. Narudia tena kumpongeza Mheshimiwa Jerry na kaka yangu Mheshimiwa Pinda kwa namna walivyo. Kwa kweli wote ni watu wapole, na wamekuwa wakitusikiliza kila tunapowajia. Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki na kamwe msipandishe mabega, Watanzania wana matumaini sana na ninyi, ahsante sana. (Makofi)