Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye katujaalia uhai na kutufanya tuweze kutoa mchango wetu kwenye Wizara hii ya Ardhi. Mchango wangu utakuwa kwenye maeneo kama matatu. Kabla sijatoa mchango wangu, naipongeza Wizara kwa maana ya Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wote. Nawahakikishia wako kwenye njia sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jerry kwa namna alivyoanza na namna anavyoendelea, nakumbuka Mwenyekiti mwenzangu wa halmashauri, anaenda vizuri. Namtia moyo na Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda. Kwa namna mnavyoenda, nina kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu kama kocha, amejua namna gani anaweza akapanga timu yake ili malengo anayoyatarajia na sisi Watanzania, matazamio yetu yaweze kufikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa kwenye maeneo matatu. Eneo la kwanza ni juu ya Mabaraza ya Ardhi. Kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 25 anaongelea Mabaraza ya Ardhi ambayo yameundwa kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Sura Na. 216. Nawapongeza kwamba mpaka sasa kuna mabaraza takribani 139 yameundwa na katika hayo, mengi yanafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mabaraza ya Ardhi kwa ngazi ya wilaya kufanya kazi, bado kuna changamoto. Naomba Wizara ione namna gani pamoja na kufanya kazi, iwasaidie ili wafanye kazi kwa ufanisi kwa sababu kufanya kazi ni jambo moja lakini kufanya kazi kwa ufanisi kufikia malengo ya wananchi ni jambo la pili ambalo ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, mabaraza haya hayana vifaa. Kukosekana kwa baadhi ya vifaa kwa mfano wanahitaji photocopier. Wanapohitaji kutoa photocopy kwa mfano, kuna maeneo wanaomba wateja watoe photocopy au wawachangishe ili wakatoe photocopy. Sasa tafsiri ya mwananchi, anaona kama vile ameombwa rushwa, jambo ambalo halitoi tafsiri nzuri kwa Serikali. Kwa hiyo, pamoja na kuunda mabaraza haya, basi naomba Wizara ijitahidi kuhakikishe kwamba yanakuwa na vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwapa vifaa, Wenyeviti wa Mabaraza haya bado maslahi yao yana changamoto kubwa na muundo wao wa ajira una changamoto vilevile. Kwa hiyo, yajengwe mazingira ya kuwafanya Wenyeviti hawa wa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya wawe comfortable na wa-feel proud kufanya kazi wanazozifanya kutoa haki kwa wananchi wetu na kuondoa manung’uniko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la Mabaraza ya Ardhi, shida kubwa ipo kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Kata. Kuna shida kubwa kwenye muundo wake, kuna shida kubwa kwa namna yanavyowezeshwa kuweza kufanya kazi jambo ambalo linasababisha migogoro mingi sana ya ardhi kwenye maeneo yetu. Nikitolea mfano Ukerewe, sisi ni eneo dogo la visiwa. Kilometa za mraba ambazo ni ardhi, tuna kilometa za mraba 640 na watu karibu 400,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona katika kilometa ya mraba moja, inakaliwa na watu takribani 600, hivyo migogoro inakuwa mingi sana. Migogoro inakuwa mingi kwa sababu gani? Kwa sababu ufanisi wa mabaraza yetu ya ardhi ya kata ni mdogo sana. Hii ni kutokana na muundo wa mabaraza haya ama ni watu gani wanatengeneza mabaraza haya, wana mwongozo gani na wana utaalamu gani? Ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumekuwa na mapendekezo mengi ama mabaraza haya yasimamiwe au haki kwenye mabaraza haya ipitie Mahakama zetu au namna nyingine yoyote ile. Mmekuwa na kigugumizi kufanya maamuzi kwenye eneo hili. Nashauri, kama haiwezekani kupitia Mahakama mabaraza haya kutoa haki, basi kiundwe chombo ambacho ni huru kama ilivyo taasisi nyingine ili iweze kujisimamia chini ya Wizara ya Ardhi ili mabaraza yetu ya ardhi ya kata yawe na ufanisi yaweze kutoa haki kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko na manung’uniko mengi sana ya wananchi huko chini kutokana na migogoro inayosababishwa na mabaraza yetu ya ardhi ya kata. Hima hima tafadhali Mheshimiwa Waziri, chukueni hatua haraka, fanyeni maamuzi ili kuweka mfumo mzuri kwenye mabaraza yetu ya ardhi ya kata ili wananchi wetu kule chini waweze kupata haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo natamani kuchangia ni juu ya mabadiliko ya Sera ya Ardhi. Natambua na kwenye hotuba umegusia, mko kwenye mchakato wa kufanya mabadiliko ya Sera ya Ardhi na hasa kwenye maeneo ya fukwe ili kuona namna gani sasa umiliki kwenye maeneo ya fukwe unaweza kuwezesha watu kuwekeza kwenye maeneo yale kama ni wafanyabiashara au namna nyingine yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri, wakati wakiendelea na mchakato huu na watakapofikia maamuzi kwenye mchakato huu wa mabadiliko ya Sera ya Ardhi wasiweke uniformity kwenye maeneo yote, wazingatie maeneo tofauti kulingana na mazingira. Maeneo kama Ukerewe ambayo ni visiwa ni sehemu ya makazi vilevile, kuna watu wanaishi pale, wamezaliwa pale, vizazi vyao vyote wanaishi pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haiwezi kuwa rahisi sana kwamba anakuja mwekezaji apewe tu au maamuzi yakafanyika akapewa eneo ama kisiwa. Jambo hili litaathiri sehemu kubwa ya jamii inayoishi kwenye maeneo yale. Kwa hiyo, wakati sera hii inafanyiwa mabadiliko izingatie maeneo tofauti kulingana na mazingira ili kwenye maeneo ya visiwa kama Ukerewe ambako pamoja na kwamba ni visiwa, lakini vilevile ni makazi ya wananchi, jamii husika ishiriki kwenye mchakato wote ili haki yao ya msingi isipotee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo nilitamani kuchangia ni juu ya upimaji, upangaji na usajili wa ardhi. Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia na kuonyesha umuhimu wa maeneo yote ya nchi yetu kupimwa. Hili ni jambo la msingi sana kwa kuwa litatuondolea migogoro, kwa sababu kila eneo litajulikana kwamba eneo hili ni eneo kwa ajili ya shughuli gani? Jambo ambalo litatoa urahisi, na kama mtu mwingine yeyote atakwenda tofauti na misingi ya maelekezo ya eneo husika, basi hatua zitachukuliwa. Hii itatuondolea migogoro mingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa kutoa mkopo kwenye halmashauri ili ziweze kupima ardhi kwenye maeneo husika. Ukerewe ni miongoni mwa maeneo tuliyopata mkopo huo. Nimemfuata Mheshimiwa Jerry mara kadhaa ili aweze kutusaidia fedha nyingine, ingawa nimesikitika kwenye taarifa yake hakuitaja Ukerewe kama ni miongoni mwa halmashauri ambazo zimeshamaliza mikopo yake. Naomba nimhakikishie kwamba tumemaliza mkopo huo, na kwa sababu ametoa utaratibu mpya, basi tutaomba tufikiriwe kupata mkopo mwingine ili tuweze kupima maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukerewe kama ilivyo Zanzibar, ni Zanzibar nyingine ya Tanzania. Kama tutaipima tukatoa mwongozo mzuri, ikatumika vizuri, ni eneo zuri sana la utalii, na shughuli nyingi za kiutalii zinaweza kufanyika na kuliingizia Taifa hili kipato. Kwa hiyo, bado tunahitaji fedha nyingine ili tuweze kupima eneo letu lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kliniki yake anayoendelea nayo. Ushauri wangu kwenye eneo hili, hawezi kwenda kila mahali. Naomba sana, kama anaweza kutengeneza mfumo kwenye maeneo yetu kule wilayani na kwenye kata kuwe na kliniki za namna hiyo, ili watalamu kutoka wilayani pale, na kama italazimika labda mtalamu mmoja kutoka mkoani na kadhalika wakashiriki, basi maeneo yaliyoko chini kule vilevile kuwe na kliniki za namna hiyo ili kuweza kushughulikia migogoro mingine mbalimbali iliyoko kwenye maeneo yetu. Jambo hili litafanya jamii yetu iweze kuwa salama. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru. Nimalizie kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu, natambua kuwa una Katibu Mkuu bora sana…
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: …ninaamini watafanya mambo makubwa na Mwenyezi Mungu awajalie sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)