Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa maoni yangu kuhusu Bajeti ya Wizara ya Ardhi iliyo mbele yetu. Nami napenda nichukue nafasi hii kuwashuruku Mawaziri, Naibu Waziri na watendaji wao wote kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mfupi nimemwona Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wameonyesha umahiri mkubwa katika kushughulikia migogoro, na hasa mingine ambayo ilikuwa imeshindikana. Kwa hiyo, nina uhakika kwamba hata mawazo yetu tutakayoyatoa siku ya leo kuhusu bajeti ambayo ni tegemeo, fedha zinazoombwa zitajibu matatizo ya waliyonayo wananchi kuhusu mambo ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo machache. La kwanza napenda kuongelea kuhusu gharama za kufanya uhamishaji wa umiliki pale watu wanaponunua nyumba na wakitaka kubadili hati ili ziwe zao, gharama ni kubwa. Gharama hii ambayo inaitwa Capital Gain Tax ambayo inatozwa na TRA pale ambapo evaluation inafanywa ni kodi kubwa ambayo inawazuia wananchi wasiweze kubadili hati hizi na kuamua kukaa na hati za zamani. Hii kodi inakwenda kuanzia asilimia tatu, wengine wanalipa 20%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoomba, Wizara iliangalie jambo hili ili kodi ijulikane, kwamba ni asilimia tatu, nne ama kumi. TRA watoze Capital Gain Tax ambayo inawezesha wananchi ili hata wale ambao hawana uwezo wa kulipa na kuweza kubadili zile hati na umiliki uwe wa kwao badala ya kuendelea kukaa na hati za watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitaongelea zaidi kuhusu umilikishaji pandikizi. Mheshimiwa Waziri ameusoma vizuri katika ukurasa wa 18 aya ya 30 na kuendelea katika kitabu chake. Tunamshuru sana kwa kuleta kliniki hizi, ni nzuri sana. Tunamsifu na tunaendelea kumwombea. Asiogope, sala zinazidi kila kitu. Sisi wanyonge ambao tumeathirika na kuonewa kutokana na hiki kitu ambacho kinaitwa uwakilishaji pandikizi (double allocation) tutazidi kumwombea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno nitakayoyasema leo naomba nisemee watu wote ambao wanapewa viwanja halafu wanadhulumiwa; ambao wanapewa viwanja halafu mtu unalipia mara mbili, na wako wengi. Ukienda pale, hivi inatwaje ile? City Council, Jiji pale, ukitaka kuona dhahma, nenda Kitengo cha Ardhi uone watu wanavyoteseka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena wameweka taratibu, wanakwenda kata kwa kata, lakini dhahma ya watu utakayoikuta pale, utaona namna hiki kitengo cha ardhi katika jiji kinavyokuwa. Mimi nawaita zimwi kabisa la pembe mia. Hata yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri, ataona kwamba watu wana malalamiko mengi, na amesema namna wanavyopewa viwanja na kudhulumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe historia yangu. Mimi ni mwathirika. Sasa kama Mheshimiwa Mbunge anafanyiwa hivi, je, watu wengine wa kawaida ambao wanasota pale inakuwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipewa kiwanja tarehe 16/06/2022. Nililipa tarehe 29/06/2022. Haikuchukua hata wiki mbili, nimelipa kwa control number 992000375444 na hii ni akaunti ya Mkurugenzi wa Jiji. Tunashukuru Jiji la Dodoma. Ni Jiji la Dodoma hapa siyo Arusha, akaunti ya Mkurugenzi wa Jiji Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka ilipokuja kliniki ya kwanza iliyoletwa hapa na Mheshimiwa Mabula nikaona hapa ni bora nikimbilie huko ili nami niende kutafuta haki yangu. Nilichokikuta kiwanja hiki kilishapewa hati mwaka 2021, nami nimelipa na yule amelipa. Sasa nasema haya mambo ni criminal. Unawezaje ukanipatia control number mimi halafu ukampa mtu mwingine control number halafu Mkurugenzi anakaa pale ofisini anaangalia watu wake wanavyofanya uchafu wa namna hii? Hii ni criminal case, siyo kama ile aliyokuwa anasema Mheshimiwa Kunambi leo asubuhi. Wote tumepewa control number, mwenzangu analipa nami ninalipa. Yeye amepewa kiwanja, ana hati, lakini mimi sina hati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu sana, nilipokwenda kuomba hati kuna mtu mmoja anaitwa Mwakasitu pale halmashauri, nimepeleka documents halafu picha zimepotea. Miongoni mwa issues ambazo ziko pale ni kwamba wanapoteza documents za watu kwa makusudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo mwingine anaitwa Mwakajuja amekwenda na documents, nimepeleka document mara sita. Nenda wapige photocopy, na pale kwenu halmashauri ni ghorofa, unatembea panda teremka, panda teremka, nenda chumba hiki. Ndivyo wanavyowafanyia watu. Mimi nimetembea mpaka viatu vinaisha visigino. Amekimbia mpaka wamemhamishia Kigoma na documents zangu. Sasa nimeanza kwenye kliniki hii ya leo, hii ambayo ameileta, mpaka barua kwa Mkurugenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiseme mengi, kuna mtu ninamtaja, yuko hapa, nami nimesema nitawataja, anaitwa Loveness. Wamalize mgogoro, anipatie kiwanja changu kabla sijakwida mtu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kumwonyesha ni namna gani hii masijala inafanya. Hii masijala ambayo imejaa zimwi la mapembe inabakia ya nini? Kwa nini wasiindoe hii masijala? Zamani Mheshimiwa Lukuvi alishataka kuvunja masijala ya Dar es salaam kule, ninyi mnashindwa nini? Haina maana yoyote pale, wanatesa watu. Sio wote, sijasema kwamba ni wote, sio wote, lakini kusema ukweli mambo ninayoyasema nayasema kwa jazba kabisa nikitetea na watu wengine ambao wanasota namna hiyo. Kwa hiyo, naomba hizi taratibu ziangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu wana dharau. Mtu ukienda wanakutazama, kwa sababu wameshakula fedha, ili ukate tamaa, uache kiwanja chako na fedha yako ife. Nimesema yangu haifi na naomba na wengine wanaonisikiliza tusote, tutembee. Nimeshakwenda kwa Mheshimiwa Jerry na nimeshamwambia. Amenishika mkono amenipeleka, lakini hakuna chochote. Hata yeye inawezekana wanaona labda eeeh! Yaani vitu vidogo hivi twende kwa Mheshimiwa Waziri jamani! Kila mtu akiibiwa kiwanja aende kwa Waziri! Mapapa wa viwanja, kwa Waziri? Atakonda na wengine watasema ni mvi, hapana tutamkukondesha sisi wenyewe.
Mheshimwia Mwenyekiti, kupitia Bunge hili na maneno atakayoyasema, naomba kiwanja changu. Wako pale, wanasikia na nimewaambia kwamba ninakwenda kuyasema leo hii hii kwa kuwataja majina kwa sababu wamechosha. Wamenichosha na wanachosha wengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwakagenda pale amepigwa. Siku nyingine nilimkuta Mheshimiwa Mabula, tulikutana kule, naye alishapigwa. Waheshimiwa Wabunge humu wananyamaza tu, lakini wameshapigwa na wale watoto. Unanunua, wanauza, wanatoa hati, that is criminal. Kwa nini wasiwachukuliwe hatua? Kwa nini wasipeleke mambo haya kwenye Mahakama? Wawashitaki watu hawa ambao wanafanya hivi? Huu ni wizi, ni wizi mkubwa. Kama ofisini nilikuwa na control number kwamba unalipa barabarani sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia juzi kuna mfanyabiashara mmoja alikuwa anaongea na RC Makonda, amemwambia kitu cha namna hii. Tunalipa fedha zinaingia kwenye control numbers za mifuko mingine. Serikali wana mikono mirefu, kwa hiyo, naomba wafanye uchunguzi ili walione hili. Wafanye uchunguzi na waondoe haya mambo ambayo wanafanyiwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wananyanyaswa na wanaibiwa na hao watoto halafu ukienda wanakutazama tu? Mimi jana aliniona, nilikuwa nimekasirika, nilitaka kukwida mtu kusudi waandishi wa habari waje, halafu watangaze kwamba kuna Mheshimiwa Mbunge Mzee mmoja amemkwida. Yaani aliponea chupu chupu, nilitaka kumkamata kabisa shati. Hatuwezi kwenda namna hii, lazima tuonyeshe reaction, wasitunyanyase namna hii. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo sisemi mengi, nilikuja nimelibeba hili purposely kabisa, kwamba niseme kwa niaba ya wengine ambao hawana uwezo wa kuja hapa iliā¦
MBUNGE FULANI: Na faili lako la malipo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatembea na faili kila mahali ninapokwenda, utadhani naomba kazi. Mimi na faili langu kila mahali, kiwanja namba 653 kila mahali, kiwanja jamani nimelipa. Yaani kila mtu anakupiga teke. Huyu anakupiga teke huku na mwingine huku, haiwezekani. Tena nawaambia leo hii hii kiwanja changu nikipate, au kesho nikienda kwa Mkurugenzi nitapiga yowe kuanzia pale ghorofa ya kwanza. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)