Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Wizara ya Ardhi. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alitilia mkazo kwenye masuala ya ardhi nchini Tanzania. Vilevile napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Jerry Silaa na Naibu wake Mheshimiwa Geophrey Pinda na watendaji wote wa Wizara ya Ardhi kwa kliniki ya ardhi waliyoianzisha, kitu ambacho awali hakikuwepo, hongereni sana. Tumeona jinsi ambavyo mnatatua matatizo ya wananchi wa Tanzania, matatizo ambayo mengi yanayohusiana na ardhi; migongano ya ardhi, double allocation na mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kuchangia kama jinsi ripoti ya Kamati yetu ilivyosomwa hapa Bungeni. Mimi nikiwa kama Mjumbe wa Kamati tumekuwa tukiwasiliana na Wizara ya Ardhi, lakini tuna mapendekezo yetu ambayo tuliweka kama Kamati. Mapendekezo na ushauri wa Kamati uliosomwa leo hapa umeonyesha Mradi wa LTIP kwamba unasuasua, ina maana hauna kasi, hautekelezwi kama inavyopaswa kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa LTIP ni mradi wa uboreshaji wa usalama wa milki za ardhi nchini. Mradi huu ni ule ambao una mkopo wa dola bilioni 150, sawa na fedha za Kitanzania shilingi bilioni 345. Fedha hizi ni za mkopo, hivyo Wizara ya Ardhi inatakiwa kwanza izitumie vizuri, lakini zaidi ya kuzitumia vizuri, mipango yake ya matumizi ijulikane, kwamba zimefanya kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri aliyoisoma na kuiwasilisha hapa leo ameongelea Mradi wa LTIP, lakini hakuongelea kwa upana. Amesema unakwenda kuboresha hati za miliki nchini Tanzania, lakini kwenye ripoti yake ukurasa wa 60 ameelezea kuwa amepima vijiji 843.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023 wakati Bajeti ya Ardhi ilipopitishwa hapa tulitoa mapendekezo. Mradi huu ulikuwa unapima vijiji 250 kwa muda wa miaka mitano, Bunge likapendekeza, na kwenye mapendekezo ya Kamati tukapendekeza kuwa vijiji viongezwe. Hii ilikuwa ni mwaka 2023. Sasa kitu ambacho ninajiuliza, tangu mwaka 2023 mpaka sasa hivi, ni kama miezi kumi imepita. Leo kwenye ripoti Mheshimiwa Waziri ameandika kwamba tayari wameshapima vijiji 843.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tukiwa kama Kamati, tumetembelea Wilaya ya Ruangwa katika Kijiji cha Nkatila, na huko tukashuhudia utoaji wa hatimiliki kwa kile Kijiji. Pia tulitembelea Maswa. Hivi vijiji vingine 843 hatujavitembelea. Pia ningependa kujua kama hivi vijiji tayari vimeshapewa hati na Tume ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi, kwa sababu naona inakuwa ni ndoto ya ajabu kwa muda wa mwaka mmoja vijiji 843 viwe vimepimwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi inahitaji kama shilingi bilioni 30 ili iweze kupima vijiji, lakini Tume hii imekuwa ikipewa fedha kidogo kwa ajili ya kupima vijiji hivyo. Matokeo yake ni kuwepo kwa migogoro ya ardhi ambayo haiishi Tanzania. Migogoro hii inatokana na sababu kwamba Watanzania wanakuwa hawajui maeneo wakalime wapi au wakafuge wapi. Vijiji vimepimwa lakini havijapangiwa matumizi ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo namwomba Waziri angaalie utaratibu wa kuweka kasi kwenye mradi huu wa LTIP. Katika hotuba yako umeeleza pia kuna ujenzi wa ofisi 25 za mikoa, lakini kwenye Ripoti ya Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba ndiyo kwanza mchakato unaendelea. Mheshimiwa Waziri, huu mradi ni wa miaka mitano, hizi ofisi utazijenga lini kwenye mikoa kwa muda mfupi? Sasa hivi huu mradi una kama miaka mitatu. Mradi umeanza toka mwaka 2022, hii ni 2024 ofisi hazijajengwa, bado zipo kwenye mchakato, mradi wa miaka mitano. Je, kuna uhakika wa kumaliza hizi Ofisi za Ardhi za Mikoa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachelea kusema kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja, atuambie. Pia Mheshimiwa Waziri kwenye ripoti yake hajaweza hata kueleza huu mradi ambao mpaka sasa una miaka mitatu umetumia fedha kiasi gani? Tunashukuru kwa kliniki, ni za huo mradi, lakini tungependa kupata ufafanuzi, fedha za mradi zimetumika kiasi gani mpaka sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia leo ni suala la wale Wafanyakazi wa Mabaraza ambao wamefanya kazi kwenye Ofisi za Ardhi na walishastaafu, lakini hawalipwi fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wafanyakazi sio wengi, lakini wamekuwa wakidai malipo yao kwa muda mrefu sana. Wizara ya Ardhi haiwalipi na hawa watu walifanya kazi kwenye Ofisi za Ardhi kwenye Mabaraza. Ina maana waliisaidia Wizara ya Ardhi, lakini hawalipwi fedha zao. Wamekuwa wakipigwa danadana, leo wameenda huku, kesho nenda huku, tutawatumia cheque, lakini Wizara ya Ardhi haijawekea umuhimu wa kuwalipa wafanyakazi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu walisaidia na walifanya kazi Wizara ya Ardhi, wangewekewa kipaumbele walipwe fedha zao, kwa sababu inaonekana kwamba watu wamefanya kazi wametumika, lakini kwa kuwa hawapo tena kwenye sekta ya ardhi, wanaonekana hawajafanya kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni zile halmashauri ambazo zilikopeshwa fedha kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Zipo halmashauri mbazo zilipewa hizo fedha, zimesharudisha, tunazipongeza sana. Pia zipo halmashauri nyingine zenyewe zimerudisha fedha nusu, bado zinadaiwa na nyingine hazijarudisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba zile halmashauri ambazo hazijarudisha zile fedha ziweze kurudisha ili halmashauri nyingine ziweze kukopeshwa na ziweze kuendelea na utaratibu wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi inapopangwa inaondoa matatizo mengi, lakini fedha hizi halmashauri zilikuwa zimekopeshwa toka mwaka 2021 mpaka leo halmashauri hizo zinaendelea kukaa na mkopo huo na halmashauri nyingine zinashindwa kukopeswa kwa sababu fedha hazijarudishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumza ni suala la Wizara ya Ardhi kuweka mfumo unaoeleweka kwa ajili ya bili za ardhi. Kama ilivyo kwenye Wizara ya Maji, mtu anapata bili yake mkononiā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa hitimisha, muda umeisha.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)