Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ALLY I. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kunijalia uhai na afya njema. Nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi kwa kuniombea dua njema; mamshukuru mke wangu na wanangu kwa ujumla kwa kuniombea dua njema; na pia nawashukuru wananchi wote wema, kwa kuniombea dua njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, mchango wangu nitajikita katika eneo moja tu, hili litakuwa ni eneo la upimaji wa ardhi na mipango miji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliyopimwa inaweka mipango mizuri ya matumizi yake. Ardhi iliyopimwa inatuonesha waziwazi wapi pa kujenga nyumba za kuishi, kulima, kufuga, kujenga viwanda, kuweka miundombinu ya kupumzika na michezo (recreation centers). Pia inaweza kuweka wazi wazi wapi pa kujenga shule, hospitali, ofisi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliyopimwa inaonesha waziwazi wapi ni maeneo ya akiba, na pia inaonesha kila kitu kinachohusiana na ardhi. Ardhi iliyopimwa ndugu zangu ni fedha, na ardhi iliyopimwa ni dhamana. Benki itakukopesha kirahisi ukiwa na ardhi iliyopimwa. Ardhi iliyopimwa ni kinga ya umaskini. Ukishakuwa na njaa utauza ardhi yako kirahisi lakini hali kadhalika unaweza ukaiwekeza kirahisi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliyopimwa ni kinga ya majanga. Kipindi cha mafuriko ardhi iliyopimwa inaonyesha miundombinu wapi pa kwenda kukabialiana na majanga hayo; ardhi iliyopimwa inatuonesha wazi wazi wapi tutapata maji kwa maana ya zimamoto, wanafahamu ni wapi tutaenda kuchukua maji kwa ajili ya kuzima moto, pia vifaa na vitendea kazi vitapita kwenye maeneo gani katika ardhi hiyo ili kufikia janga mahali lilipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliyopimwa ni kinga kwa tetemeko; ardhi hii imekuwa ni bora sana wakati wa matetemeko kwa sababu nyumba zimewekwa kwa mpangilio kiasi kwamba hata itakapoanguka nyumba moja kutakuwa na ugumu kwa nyumba nyingine kuathirika, kama kwa watu walioko kwenye nyumba za karibu karibu kama zile ambazo ardhi hazijapimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ardhi iliyopimwa ni njia na kinga ya kuondokana na magonjwa. Kipindi cha mvua maji hayawezi kutuama na kusababisha magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu, malaria na magonjwa mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ardhi iliyopimwa ni kinga ya migogoro. Kukiwa na ardhi iliyopimwa aghalabu huwa inakuwa na migogoro. Pia ardhi iliyopimwa ni urithi thabiti na kizazi kinachokuja, kwa nini nimeongelea haya? Nimeongelea haya kwa sababu hakuna kitu chochote cha muhimu kama nchi hatujaweka mipango yetu vizuri kwenye ardhi. Ardhi ni urithi mkubwa wa asili kwa dunia ambao tumepewa kuliko maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijikite kwenye Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, inayoonyesha matumizi hafifu ya ardhi. Kwa ripoti ya mwaka 2023 inaonyesha kwamba, Tanzania kiasi cha ardhi kilichopimwa ni 25% pekee. Pia ripoti inaonesha kuwa, kuna makazi holela takribani 70%, kwa maana hiyo wananchi wa Tanzania 70% wanakaa katika makazi holela. Hili siyo jambo dogo hata kidogo. Nafikiri tunajua jinsi gani tunatakiwa tuanze kujielekeza katika eneo la kupima ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utafiti uliofanyika katika halmashauri mbalimbali umeonesha, kumekuwa na uibukaji wa maeneo yasiyokuwa rasmi. Majengo yanayojengwa katika maeneo yasiyopimwa, kwa maana hiyo makazi holela, kwa mfano ripoti ya New Urban Agenda, inaonyesha kabisa kuna takribani nyumbani 1,444,000 kwa makazi holela. Sasa ukichukulia idadi ya nyumba ambazo tumezijenga, unaweza ukaona ni kwa kiasi gani tunaishi katika makazi holela. Hili siyo jambo jema, hususan wakati kunapotokea masuala ya majanga, kama nilivyozungumza hapo mwanzo, na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Ripoti ya Utekelezaji wa Wizara imetuonesha kwamba, kwa miaka tofauti tofauti kumekuwa na nyumba zilizojengwa kwenye makazi holela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2019/2020 takribani nyumba au majengo 348,918; mwaka 2020/2021 kuna takribani nyumba 741,645 holela na mwaka 2022 takribani nyumba 452,806 ambazo ni holela. Kwa hali hii inaonesha wazi wazi kwamba, tatizo hili ni kubwa, kama nilivyoanza kulizungumza hapo mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, makazi holela yameonekana katika halmashauri zote. Halmashauri ya Arusha inaongoza. Ni kitu cha kushangaza sana, lakini ndiyo inayoongoza kwa makazi holela. Takribani 95% ya makazi yaliyopo ni holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kuzungumza hayo niliyoyazungumza, kutokana na ufinyu wa muda, naishauri Wizara kujielekeza moja kwa moja katika kuharakisha upimaji wa maeneo ya nchi, ili kupata uhakika wa ardhi iliyopo kwa vizazi vinavyokuja hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)