Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Serikali kwa ujumla, hususan Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, timu yote ya Wizara pamoja na Kamati husika kwa jinsi ambavyo wamechambua haya mambo mpaka wamefika leo kutoa hotuba nzuri hivi. Namushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa umahiri wake. Nampongeza sana kwa umahiri wake na ninawapongeza viongozi wote waliohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zile 4R za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zinatuhusu Watanznaia wote, lakini Sekta hii ya Ardhi hasa hasa inahusika zaidi na R ya tatu na R ya nne. Katika R ya nne, Kulijenga Taifa, hatuwezi kulijenga vizuri upya Taifa kwa maana ya miradi ya miundombinu, majengo ya biashara na makazi, majengo ya huduma za jamii na huduma za jamii kwa ujumla na ujenzi kwa ujumla bila kufanya maboresho makubwa kwenye Sekta ya Ardhi au Land Reforms. Hatuwezi kupata maendeleo endelevu katika nchi (Sustainable Development) bila kufanya land reforms. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaalamu mmoja wa maboresho ya Sekta ya Ardhi duniani aitwaye Raleigh Barlowe katika andiko lake lililochapishwa mwaka 1953 katika Journal of Farm Economics, Volume ya 75, Na. 2, Uk. 173 – 187 katika mada iitwayo, Land Reform and Economic Development, amesema, ninanukuu: “Land reform is often treated as a necessary or highly desirable condition for economic development, although it might also be viewed as a partial consequence of the development process.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba maboresho ya Sekta ya Ardhi ni sharti muhimu la maendeleo ya kiuchumi, ingawa vilevile wakati mwingine maboresho ya Sekta ya Ardhi yanaweza kufanyika kupitia matokeo ya mchakato wa maendeleo. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo analolishauri mtaalamu huyu ni kwamba, ili tupate maendeleo ya haraka ni lazima maendeleo hayo yawe guided na maboresho ya Sekta ya Ardhi. Siyo maendeleo yapatikane kwanza halafu ndiyo tuje tuboreshe Sekta ya Ardhi. Hayo ndiyo makosa ambayo tumeyafanya miaka yote ambapo Sekta ya Ardhi imekuwa nyuma ya maendeleo ambayo wanayafanya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tumepata matatizo mengi ya kuwa na ujenzi holela katika miji mingi, makazi duni, holela, nyumba zisizo na viwango ambazo zimekuwa zikisababisha ajali mara nyingi, makazi yasiyo na huduma za miundombinu, migogoro mingi ya ardhi, watu wetu kukosa dhamana kwa ajili ya kukopa kwenye benki, watu wa vijijini kukosa dhamana hata kama wana Hati za Kimila na hizi Hati za Kimila hazitambuliki na benki. Haya ni matatizo ambayo yamesababishwa na kutokuwa na land reforms ambazo zina-guide maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi chache ambazo ni muhimu sana kwa Wizara hii. Juzi katika semina wametupitisha kwenye Sera ya Ardhi ambayo imefanyiwa mapitio na wametuahidi kwamba, baada ya sera sasa watakuja na Mkakati wa Taifa wa kutekeleza Sera ya Ardhi. Hii ni tofauti na walivyofanya mwaka 1995, baada ya kuwa tumepata Sera ile ya Ardhi ya mwaka 1995 walikuja wakatengeneza Sheria za Ardhi, mwaka 1999.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sera ilifuatiwa na Sheria badala ya mkakati. Kwa hiyo, baada ya Sheria ya Mwaka 1999 ndiyo wakaja wakatengeneza kitu kinaitwa Mkakati wa Kutekeleza Sheria. Mimi nilikuwepo katika Timu ya Wataalamu ya MKUKUTA wakati ule na tulikuwa tunabishana na Wataalamu wa Sekta ya Ardhi, tunawaambia mmefanya makosa, utekelezaji kwenye Sekta ya Ardhi utakuwa na matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana utekelezaji wa Sekta ya Ardhi kuanzia mwaka 1999 mpaka sasa mwaka 2024 bado hawajapata mafanikio makubwa kwa sababu walikosea. Kwa sasa hivi kama unakuja na ile plan continuing kwamba, unatoka kwenye sera, halafu unakuja kwenye mkakati, halafu baadaye unakwenda kwenye sheria, halafu ndiyo uje kwenye mpango, hapo kitakuwa ni kitu kizuri. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, ninaamini sasa mambo haya yatakuja kuwa mazuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi ya pili naitoa kwenye Wilaya ya Sikonge. Nimearifiwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Mkoa wa Tabora kwamba tayari mpango umeshakamilika. Ifikapo mwaka 2026 vijiji vyote vya Wilaya ya Sikonge vitakuwa vimepimwa, mipango ya matumizi bora ya ardhi na kwa kweli, hatua hiyo ni kubwa sana. Haijafanyika kwa muda mrefu, hii ni pongezi kubwa sana kwa Wizara ya Ardhi. Nampongeza Kamishna Msaidizi wa Ardhi, aendelee na Mpango huo ausimamie ili uweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwneyekiti, nina ushauri katika maeneo machache. Ninaishauri Wizara ya Ardhi, iandae mkakati wa kutekeleza hii sera mpya ambayo imewasilishwa juzi. Mkakati wa sera uandaliwe kwa umakini mkubwa kugusa maeneo yote ili sera itekelezeke vizuri zaidi, halafu baada ya hapo wafanye mapitio makubwa ya kuja na sheria mpya za ardhi. Baada ya sheria waje na mpango wa mwaka mmoja, mipango ya miaka mitano na mipango ya muda mrefu, miaka 20 na kuendelea, ambayo itai-transform sekta ya ardhi iweze kusaidia maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna sababu kwa nini mtu wa mjini apate Hati ya Ardhi ambayo inatolewa na Wizara ya Ardhi, halafu mtu wa kijijini apate Hati ya Kimila. Katika mabadiliko ya sheria mtakayoyaleta ni muhimu sana itolewe Hati ya Ardhi Mjini na Vijijini, ili mtu wa mjini awe na uwezo wa kukopa benki na mtu wa kijijini awe na uwezo wa kukopa benki. Huu utaratibu wa Hati za Kimila hautambuliwi na benki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima mwatendee haki Watanzania wote wanaoishi mijini na vijijini. Ardhi yote inayomilikiwa na wananchi ipimwe ili kila kipande ambacho anamiliki mwananchi kijulikane ili kuondoa migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali ije na mpango wa ujenzi wa nyumba bora. Haiwezekani tangu uhuru hatujaweka ultimatum ya ujenzi wa nyumba bora. Zamani kulikuwa na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanasimamia mipango ya ujenzi wa nyumba bora, lakini Serikali kwa ujumla haijaja na mpango mahususi wa kuwasaidia wananchi wawe na ujenzi wa nyumba bora, tofali za kuchoma na mabati. Mnaweza mkawa na mpango wa ruzuku kwa ajili ya vifaa vya ujenzi ili Watanzania wa-transform waje kuwa na nyumba bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, tuna mgogoro wa mpaka kati ya Tabora na Singida. Mgogoro ule ni kama vile umeisha, kilichobaki ni kuweka beacon na wawekaji wa beacon ni Wizara ya Ardhi. Naomba mje kwenye mpaka wa Tabora na Singida mweke beacon hata kesho ili kuondoa mgogoro wa mpaka kati ya Tabora na Singida ambao umekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, nilikuwa na maeneo haya ya ushauri ili kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri kwa 100%. Ahsante sana. (Makofi)