Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana kwa sababu, hakuna jambo lolote linafanyika bila ardhi. Chochote kile tunachokifanya katika nchi hii au duniani, kinafanyika juu ya uso wa ardhi. Kwa hiyo, ni sekta au ni Wizara ambayo inabeba maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza tu kwa kumpongeza ndugu yangu Mheshimiwa Jerry. Pongezi alizozipata ni nyingi, lakini anastahili. Kwa hiyo, naomba tu kama walivyopongeza, hasa Mheshimiwa Tauhida, nami ni hivyo kama Mheshimiwa Tauhida alivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita zaidi kwenye jimbo langu. Yako mambo mengi ya kusema, lakini kubwa nataka tu niseme juu ya migogoro midogo midogo na mikubwa ya mipaka na mashamba. Naanza na shamba moja kubwa lililopo Kata ya Kinyangiri, linaitwa Shamba la Makometi. Shamba hili ni mali ya Wizara ya Mifugo, lina hati, lakini limekuwa shamba pori kwa muda mrefu na mnafahamu madhara ya mashamba pori. Mashamba pori wananchi huwa wanaingia huko. Sasa, pale wananchi wa kutosha wameshaingia, wengine wamejenga humo, wengine wanalima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, japo bado kuna eneo kubwa limebaki, lakini mimi nakuomba Mheshimiwa Waziri, shamba hili sasa uende ukatambue upya mipaka, lakini kubwa zaidi uwatambue wale wananchi ambao wako mle kwa sababu, wameachwa muda mrefu. Maeneo yao mengine yameshakuwa makubwa kama kitongoji sasa, kwa hiyo, angalau hayo maeneo yarasimishwe na eneo kubwa la shamba pori lililobaki Wizara ifanye jambo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara imeshindwa, basi ituachie sisi Halmashauri ya Mkalama ili tulipangie matumizi ya maendeleo kwa sababu, tumekuwa tukililinda kwa muda mrefu, maana sasa Wizara haifanyi chochote. Matokeo ni wananchi wetu wanaingia halafu baadaye watakuja kutolewa, watakuja kupata shida sana, watakosa mahali pa kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sasa kuna wengine wamezaliwa humo wanaamini hayo ndiyo maeneo yao. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje Mkalama atambue mipaka ya shamba hili la Makometi, shamba pori, ambalo lilikuwa ni kituo cha mifugo. Wananchi ambao wameingia humo watambuliwe wafanye mambo yao kwa uhuru, lakini eneo lililobaki basi Wizara ifanye kitu ama itukabidhi Halmashauri tuendelee nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu migogoro ya mipaka kati ya Wilaya ya Mkalama na Wilaya za jirani. Upo mgogoro wa mpaka kati ya Singida DC kwa ndugu yangu Mheshimiwa Ighondo pale katika Kijiji cha Ntondo. Kuna mgogoro pale unasumbua sana wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mgogoro kati ya Wilaya ya Iramba na Mkalama, katika Kijiji cha Kisana, Kata ya Gumanga. Kijiji kizima wameingia, karibu kitongoji kimeingia kwetu, lakini wao kwa sababu asili yao ni kule Iramba, wanataka waendelee kutii mambo ya kule wakati tayari wako kwetu. Kwa hiyo, naomba migogoro hii ifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mgogoro kati ya Kijiji cha Milade na Wilaya ya Ikungi katika Kijiji cha Munyu; upo mgogoro kati ya Kijiji cha Milade na Kijiji cha Mgungia; pia upo mgogoro kati ya Kijiji cha Maruga, Iramba, na Tumuli. Hii yote ni migogoro kati ya Wilaya ya Mkalama na Wilaya nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Wilaya ya Mkalama inapakana na mikoa miwili; inapakana na Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Arusha. Huu mpaka wa Mkoa wa Manyara na Arusha na Wilaya yangu ya Mkalama imekuwa ni tatizo kubwa na la muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza swali hapa Bungeni na nikajibiwa kwamba, watakwenda wataalamu kule, lakini mpaka hivi ninavyoongea mgogoro huu haujaisha. Mgogoro huu una madhara makubwa. Wako Wahadzabe wanaishi kule katika Kata yangu ya Mwangeza, hawa watu bado wanakula asali, nyama na mizizi, na kwa kuwasaidia imepatikana miradi, tukaamua tuwawekee mizinga kule ili tuwapatie asali, maana zamani asali ilikuwa inapatikana kwenye vichuguu. Siku hizi hakuna asali ya kwenye vichuguu, kwa hiyo, tukawapatia mizinga, lakini wenzetu wa Mkoa wa jirani wakaja wakateka, wakavunja ile mizinga wakisema kwamba eneo lile ni lao wakati siyo lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje Mkalama, aje Mkoa wa Singida, atuite. Aite Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, na sisi Wabunge wote twende kwenye mpaka tutambue. GN ipo, mipaka huwezi kuhamisha, ile GPS huwezi kuihamisha, tusomeeni pale mpakani ili kila kitu kieleweke. Sisi tumeshajiandaa maana unaweza ukawakosa wapigakura au ukaongezewa wapigakura. Sasa ukweli ukishasimama pale mambo yote yataeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili alichukulie maanani, limeanza muda mrefu sana mpaka tumenyang’anywa mnada pale Kijiji cha Endaragati na wenzetu wa Manyara wakauchukua ule mnada, tuna uhakika ni wa kwetu, tukisoma ninajua kabisa ule unarudi. Kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Flatei ajiandae tu pale, yale mapato atayakosa iwapo Waziri atakuja kusoma vizuri ule mpaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba niongelee suala la Baraza la Ardhi, Mabaraza ya Ardhi ya Kata. Nchi yetu ni kubwa sana. Baraza la Ardhi la Wilaya kushughulikia migogoro ya Wilaya ni mzigo mkubwa sana. Nakuomba Mheshimiwa Waziri arudishe ile system ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata kutoa hukumu, lakini ayaboreshe, yapelekewe Wenyeviti ambao ni professional kama yalivyo Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu hatuna upungufu wa human resource. Wako vijana wengi mtaani wamesoma sheria, wamesomea uhakimu, wanasubiri ajira. Haya Mabaraza ya Ardhi ya Kata yakiimarishwa haki itatendeka kule chini. Kitendo cha mwananchi mnyonge kwenda kwenye Baraza la Ardhi la Wilaya ni mgogoro mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeshuhudia, mwenyewe niliuziwa ardhi na jamaa, halafu kumbe katuuzia wawili akataka anidhumulu kwa sababu mimi ni Mbunge, nitaogopa wapigakura. Nikaona hebu ngoja niende kwenye Baraza la Ardhi la Wilaya nikapate haki yangu. Mwaka mzima na siyo makusudi, wale Wenyeviti wameelemewa na kesi. Maana uende ukasajili, utoke hapo uwaite mashahidi, wewe usikilizwe, asikilizwe mwenzako, alete mashahidi wake, sijui yaani mpaka ule mlolongo wa kesi uje uishe ni mwaka na yote hiyo ni gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanyonge wengi wameamua kuacha hizi kesi, wamedhulumiwa. Amekosa nauli yake mwenyewe, lakini leo anatakiwa abebe mashahidi, abebe sijui watu gani wakasikilize kesi. Inafika mahali wanaamua kuacha. Kama mimi Mbunge nimetoka jasho, mwaka mzima, kila siku ninachoma mafuta na siyo makusudi, siyo kwamba wale Wenyeviti wanafanya makusudi, ana mlolongo wa kesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anakaa kuanzia saa nne mpaka saa 12 jioni kusikiliza kesi za ardhi. Sasa nakuomba Mheshimiwa Waziri arudishe Mabaraza ya Ardhi ya Kata yatoe hukumu, ila yaboreshwe, yapelekewe Mahakimu professional ili watoe hukumu. Haya Mabaraza ya Wilaya yawe Mabaraza ya Rufaa, yatakayoshindikana kule kwenye Kata ndiyo yaende kwenye Wilaya. Hapo tutakuwa tumemsaidia mnyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanyonge wanateseka sana, wengi wameacha ardhi zao na watu wenye fedha wanafanya makusudi kabisa. Anachukua ardhi, anajua huyu atashindwa tu njiani kwenye kesi. Wale Wenyeviti hata rushwa hawachukui, wale ni kwamba, tu ile nenda rudi, nenda rudi, wananchi wanaamua kuacha, lakini ukweli ni kwamba, wameelemewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wale Wenyeviti wanafanya kazi kubwa. Naomba niwapongeze, nimeshuhudia mwenyewe wanafanya kazi kubwa sana, kwani migogoro ni mingi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, arudishe Mabaraza ya Ardhi ya Kata yatoe hukumu. Maana sasa hivi yanafanya usuluhishi tu, hayatoi hukumu. Kwa hiyo, kwanza hayaheshimiki, lakini wapelekewe Mahakimu Professional ili watu wetu wapate haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata haya Mabaraza yatalinda hata hiki ambacho Wabunge wamekisema kila kona kwamba, tupime ardhi. Tukishaipima haioneshi kwamba wahalifu watakosekana. Wako watu watataka kuvamia eneo limepangwa la malisho wao wanataka walime, wengine eneo la viwanda, wao wanataka wajenge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya Mabaraza ya Ardhi ya Kata kama yatakuwa yamewezeshwa vizuri, ndiyo yatakayotatua hii migogoro huko chini. Hata hiyo ardhi ukiipima itabaki kuwa salama kwa muda mrefu na itakuwa imewasaidia Watanzania. Kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Waziri naomba sana kwa hili, aje Mkalama, atupimie mipaka na sehemu nyingine nchi itulie. Apime ardhi kama alivyosema, lakini awezeshe haya mabaraza ili wanyonge wa nchi hii wapate haki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kumpongeza, hongera sana. Unajua kijana anapofanya vizuri, anasababisha mama aendelee kutuona vijana kwamba, tunaweza. Kwa hiyo, anatuwakilisha vizuri na ninampongeza mama yangu kwa jicho lake la kuona. Bunge hili ni kubwa, lakini akaona na amepatia, na muda wote hesabu za mama ni za uhakika, zinafunga magoli. Mama endelea kupiga hizi hesaby za uhakika ili wananchi wa Tanzania waendelee kufaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)