Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kwanza kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara hii ya Ardhi siku hii ya leo ili niweze kufikisha masuala mbalimbali ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyoisimamia Wizara yake akisaidiana na Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kweli wameleta chachu kubwa kwenye usimamizi wa masuala ya ardhi najua mfupa huu ni mfupa mgumu, lakini sina wasiwasi Mheshimiwa Waziri alikuwa Diwani, lakini ameshawahi kuwa Meya, kwa hiyo, anajua kule chini ambako hasa ndio kunakotengenezewa haya matatizo namna ambavyo kupo, kwa hiyo, nimtie moyo na nimwambie tu, tuna imani kwamba atatufikisha mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze moja kwa moja kupongeza baadhi ya maeneo ambayo amefanya vizuri mpaka sasa. Majengo ya National Housing Tanzania nzima yapo maeneo ambayo ni prime, maeneo muhimu ambayo ndiyo yanabeba taswira. Majengo haya kwa muda mrefu yalikuwa hayafanyiwi ukarabati, yanakuwa yamebaki yamechakaachakaa, yana sura mbaya na kusababisha maeneo kama Mji wa Moshi kuonekana na sura chakavu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri lakini na Mkurugenzi wa National Housing kwa kuleta zaidi ya shilingi milioni 300 kwenye mkoa wetu wa Kilimanjaro na kurekebisha au kufanya ukarabati kwenye majengo yale ya National Housing ambayo yapo katikati ya mji hasa barabara ya Double Road. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze kazi ya Kliniki za Ardhi ambazo anazifanya Mheshimiwa Waziri ambazo zinaleta majibu ya moja kwa moja na kumuonesha uhalisia kwenye maeneo yale ambayo anafanyia kazi. Pia nimpongeze kwenye hati hizi za kielektroniki, unakuta sehemu moja watu watatu wana hati na zote zinafanana. Kwa kuleta hati hizi za kielektroniki ambazo zina serial number ina zina tarehe ina maana itapunguza kwa kiasi kikubwa sana migogoro, lakini italeta urahisi katika utatuzi kwa sababu itajulikana ni nani mwenye hati zile za mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale kwenye ukarabati nilete ombi Mheshimiwa Waziri, pamoja na kukarabati zile nyumba hasa kwenye maeneo ya biashara ninaomba waangalie namna ya kurekebisha maeneo ya pedestrian, maeneo ya watembea kwa miguu yawekwe angalau pavement ili sasa uzuri huo ambao umeonekana katika ukarabati wa majengo u-reflect kwenye maeneo ya watembea kwa miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa muhimu sana leo unakwenda kwenye ukurasa wa nane wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini naangalia tena kwenye ukurasa wa 47 alipoorodhesha vile vipaumbele vya Wizara katika bajeti hii alisema ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishwaji wa ardhi mijini na vijijini, sasa hapa ndio ninapotaka kuweka point yangu ya muhimu.

Mheshimiwa Spika, miji inakua, wakati Dar es Salaam inaanza enzi hizo pale Manzese palikuwa panaonekana ni nje ya mji, kwa hiyo, wakati inakua pale pakaachwa, pakajengwa kiholela, slum, hivyo hivyo pakaja Kimara. Sasa maeneo mengi ya miji yanayokua, watu wamekuwa na tendency ya kununua maeneo ya pembezoni, moja ni kwa sababu ya kasi ya ukuaji, lakini pili ni kwa sababu ya gharama kwenye yale maeneo yanayohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili linasababisha maeneo ya pembezoni ya maeneo yale ambayo yameshatambulika kama ni maeneo ya miji kununuliwa kwa kasi na kujengwa kiholela maana yake ni nini? Kwa mfano, natolea mfano halisi wa Moshi Mjini, Moshi Mjini ndio mji mdogo zaidi Tanzania, una kilometa za mraba 58, ulipokuwa unapanuka, maeneo ambayo yalitambulika kuanzia na Baraza la Madiwani, yameshapita kwenye DCC, yamekwishapita kwenye RCC na yakaletwa Wizarani kwa ajili ya kupanua mji mwaka 2016. Mpaka leo tangu hayajapata baraka hiyo, yalishakwenda mbali sana mpaka tukapata GN Na. 219 ya terehe 15 Julai, 2016, lakini tangazo hilo lilitiwa saini na Mheshimiwa Lukuvi akiwa Waziri wa Ardhi tarehe 26 Juni, 2016.

Mheshimiwa Spika, ombi la msingi ni kupanua maeneo yale ya kiutawala kwa sababu eneo lile limeshajaa kabisa, hatuna maeneo ya makaburi, makaburi yamejaa, eneo la dampo tumenunua Moshi Vijijini na ni umbali mrefu, lakini adha kubwa zaidi ni kwamba barabara ya kwenda pale kwenye dampo hatuwezi kukarabati na maeneo mengine ya kiutawala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu eneo la Moshi Mjini linapakana na eneo la Hai, linapakana na Moshi Vijijini ilikuwa ni vigumu kulifanyia maamuzi mara moja, lakini vikao vyote vimeshafanyika na wakati huo mimi nilikuwa Diwani nilishiriki, tukapitisha hayo, lakini mpaka leo tumeshindwa kuongezewa eneo hilo ili tuweze kupanga eneo hilo vizuri na kwa bahati mbaya waliokuwa wanapinga mwanzo walionesha eneo hilo ni eneo la kulima, lakini Mheshimiwa Waziri ninaomba ufanye ziara, uje nikutembeze, maeneo hayo yanauzwa kiholela, yanapangika kiholela na yanajengeka kiholela, nyumba kubwa na za kifahari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Mnavyochelewa kuja kulifanyia maamuzi maana yake tutakuwa kila mara miji yetu badala ya kuipanga vizuri kazi yetu itakuwa ni kuirasimisha tu ambayo imeshapangika vibaya, barabara haziwezi kupelekwa, huduma za jamii haziwezi kupelekwa. Kwa hiyo, ninamwomba sana Waziri, sina nia ya kuja kukamata shilingi, nilikuwa ninaweza hapa na ndio ningekamatia, lakini ninaomba nimwelezee, naomba walifikishe mwisho suala la upanuzi na ninaelewa kuna matatizo ya kibajeti tunaposema liwe jiji, tuachane na jiji kwanza, turuhusuni yale maeneo ambayo tayari yameshapita kwenye vikao ya upanuzi yaingie, tupanue mji wetu ili suala la jiji lije baadaye, hilo ndio suala langu la kwanza ambalo nimeona ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni eneo la urasimishaji makazi, limekuwa na phases mbalimbali, kuna mwanzo ilikuwa inafanyika na Serikali, baadaye wakaleta sekta binafsi ifanye, watu wakachanga hela, likaishia njiani. Tuna maeneo mengi kwenye baadhi ya kata hasa pale Moshi Mjini ambazo watu walishatoa hela kwenye makampuni ya urasimishaji, idadi haikufika ile inayotakiwa, makampuni mengine yakawa yameshaondoka na hela watu wameshatoa, urasimishaji haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha alete hoja ambayo itaonesha namna ya kufunga suala la urasimishaji hasa kwenye maeneo ya miji ambayo tayari yanahitaji sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna eneo linahitaji sana kuangaliwa na Wizara, kwa mfano Wizara ya Ardhi haina wataalamu kabisa, Mkoa wa Kilimanjaro nafikiri mkoa mzima surveyor ni mmoja, Moshi Mjini tulikuwa na surveyor tena msomi mwenye PhD wakamchukua, wakampeleka UDOM, hawajatuletea surveyor mpaka leo, ma-QS hali kadhalika.

Mheshimiwa Spika, sasa unajitahidi sana kutatua migogoro, lakini moja ya maeneo yanayokusababishia migogoro ni kutokuwa na wataalamu kule chini ambao watasimamia na kuhakikisha wanakupa taarifa za uhakika za kila siku kwenye maeneo yake, lakini pamoja na wataalam hata kwenye ofisi, sisi Moshi Mjini tulitoa eneo la ofisi kwa ajili ya Wizara ya Ardhi nimeona pale umeandika kwamba unaweka mkazo katika kujenga ofisi, lakini mpaka sasa hivi hamna kilichoendelea, eneo lipo pale kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Wizara yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine la muhimu sana ni eneo la maeneo ya wazi na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri alikuwa Diwani, anafahamu jinsi maeneo ya wazi yanauzwa, yanauzwa kwa kasi sana na yanauzwa kwa watu binafsi, hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi Manispaa ya Moshi katika baadhi ya maeneo ya Kata ya Rau, Ng’ambo na Mji Mpya yalipata mafuriko, tumechukua watu tukawapeleka kwenye hizi shule mpya wakae pale kwa sababu gani? Hatuna maeneo ya wazi, yameuzwa, watu wanamilikishwa pamoja na mazuri yote ambayo yanaendelea kwenye Wizara yako naomba tutafute namna ya kuweka sheria kali kwenye maeneo ya wazi hata ikibidi hati yake iwe tofauti, lakini tuhakikishe kwamba inakuwa ni kosa la jinai mtu kununua eneo la wazi hata akiwa na hati shida hii ya kusema lazima afute Rais kwenye eneo la wazi hata kama ni miaka 20 mtu analo, tuweze kulirudisha kwa wananchi kwa sababu tunayahitaji sana maeneo ya wazi na maeneo ya wazi yanauzwa sana... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)