Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ya Ardhi. Kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ambapo amenipa afya njema nimeweza kusimama kwenye Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Mwenyezi Mungu alimpa macho ya rohoni kumteua Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, kaka yangu hapa na aunt yangu hapa Silaa, ambaye kwa kweli anaitendea haki sana hii Wizara ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Silaa kwa namna ambavyo anafanya vizuri. Anawatetea wananchi na amesimama kwenye haki. Nami namtia moyo kwa namna anavyofanya Mwenyezi Mungu asimpungukie, amsimamie kwenye majukumu yake, asiwe na hofu wala wasiwasi Watanzania wote wanamfurahia kwa kazi nzuri hii anayoifanya kwa sababu anawasaidia hata wale wanyonge ambao hawana uwezo kabisa. Maana mara nyingi inaonekana kama haki haipo; haki inapatikana kwenye fedha, lakini wewe hilo kwako halipo. Ninampongeza sana pamoja na Wizara yake yote ya Ardhi, Mwenyezi Mungu aendelee kuwa pamoja nao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naishukuru sana Serikali kwa kuleta fedha kupitia Mradi wa World Bank katika Mkoa wa Mbeya ambapo fedha hizo zimewezesha kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Chunya ambapo kwa ujumla wa vijiji 21 vimeandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi na pia migogoro ambayo ilikuwepo kati ya mipaka ya Songwe na Mbeya imeweza kutatuliwa na migogoro 18 ya mipaka na vijiji pamoja na Mbeya yenyewe Chunya na Songwe imekwenda kutatuliwa.

Mheshimiwa Spika, hivyo naipongeza sana Serikali na naishukuru kwa kufuatilia haya na kutuletea fedha hizo ambazo zinakwenda kufanya na kutenda haki. Pia, naishukuru sana Wizara kwa kutuletea mradi katika Halmashauri za Rungwe, Kyela na Busokelo ambapo zaidi ya vijiji 250 vinaenda kuandaliwa ambapo inakwenda kumaliza migogoro yote katika halmashauri hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa shukrani hizi; unajua Mkoani Mbeya kesi zinakuwa nyingi sana kwa ajili ya kung’ang’ania ardhi wakati fulani hata ikizidi futi moja mtu anaweza asikubaliane na ile futi moja anakwenda Mahakamani kesi zinaenda kurundikana. Sasa kwa kutuleta fedha hizi tunaamini kwamba tunakwenda kupona kwa kesi hizi ambazo zinakuwa zinajitokeza.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango kabambe wa Jiji la Mbeya kwa maana ya masterplan, Jiji la Mbeya ndiyo jiji pekee nchini ambayo sehemu yake kubwa katika kitovu cha jiji ina makazi yaliyo chakaa sana yenye ujenzi holela. Kutokana na hali hiyo masterplan ya jiji ambayo imeanza kutekelezwa mwaka 2022 ilikuja na mwongozo wa utekelezaji upya wa makazi yaliyochakaa ya Kata ya Maanga, Sinde, Ruanda na Mabatini.
Mheshimiwa Spika, Jiji la Mbeya kama nilivyoeleza hapa awali, Jiji la Mbeya ni jiji kongwe, ni jiji ambalo jina lake ni kubwa sana lakini jiji lile huwezi kusema sasa hivi unaingia hapa, kwamba hapa ndiyo mjini. Mji upo wapi? Mji ni Manga? Haiwezekani, Mji ni Sinde? Haiwezekani, Mji ni Mabatini? Pamejengwa kiholela hakuna mpango wa masterplan. Hivyo naiomba sana Wizara ya Ardhi iliangalie hili kwa macho yote kwenye Mkoa wa Mbeya katika mpango huu ambao unaendelea pale Mkoani Mbeya uliyoandaliwa tangu mwaka 2022 ili kuweka sura ya mji pale Mbeya iwe sawa sawa na majiji mengine.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mkoa wa Mbeya kiu yao kubwa ni kuona jiji lile la Mkoa wa Mbeya linafanana na majiji mengine. Sawa kuna nyumba zipo pale lakini ni chakavu sana, nyumba zimechakaa lakini pia popote unapopita unaangalia hivi nakwenda mjini, ni wapi? Mjini ni Posta, Mafiati, Mwanjelwa ama mjini ni wapi? Kwa hiyo naomba sana Serikali tuangalieni sana wananchi wa Mkoa wa Mbeya ili na sisi pale pawe na sura nzuri inayofanana na majiji mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali kwa Wizara, Wizara ina mkakati gani wa kusaidia utekelezaji wa uendeshaji upya wa makazi yaliyochakaa na yenye ujenzi holela katika kitovu cha Jiji la Mbeya? Kama kuna jambo Wananchi wa Jiji la Mbeya wanatamani ni uendelezaji mpya wa maeneo yaliyochakaa katika Jiji la Mbeya pamoja na centre inayokuwa na hadhi ya jiji kama yalivyo kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, upangaji na upimaji kwenye maeneo yote ambayo barabara ya mzunguko wa ring road na barabara ya mchepuko by pass maeneo hayo yanakwenda kutengenezwa ama yanakwenda kujengwa, hizo barabara ni mpango kwa sababu barabara hizo zinapita kwenye ardhi. Wakati Wizara inaendelea kujipanga kwenye ujenzi wa hiyo barabara tulitamani sana fedha ziende kwenye Wizara hiyo kwa maana ziende Jiji la Mbeya ili wakati wa mpango wa zile barabara ambazo zinakwenda kujengwa sasa kuwe tayari kumeshapimwa.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ambavyo Mbeya ilivyokaa tunaomba sana ionekane ni jiji la kisasa. Ni jiji ambalo limeonekana na kwamba hilo jiji linakwenda kuonekana kama majiji mengine. Jiji kama jiji kwa maana Halmashauri ya Mbeya Mjini haiwezi kuwa na fedha ambazo zitaweza kutengeneza ama kuweka majengo ambayo yanatakiwa kwenye Jiji hilo la Mbeya. Tunaitegemea sana Wizara iangalie macho yote pale kwenye Jiji la Mbeya na mkiangalia jiji lenyewe hilo mnaona kabisa na mnajua kabisa mwenye jiji lake ni Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na bado ni Rais wa Mabunge ya Dunia - IPU linatakiwa lifanane pamoja na yeye mwenyewe kwa nafasi zake alizokuwa nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ikifanya hivyo itakuwa imetuheshimisha sana wananchi wa Mkoa wa Mbeya, lakini pia imekupa heshima kubwa sana kulingana na nafasi zako ulizonazo. Kwa kusema haya nishukuru sana kwa kunipa nafasi nami kuongea juu ya hili jambo. Mwisho Mheshimiwa Waziri Jerry Silaa Mwenyezi Mungu aendelee kumsimamia na kumwongoza kwenye majukumu yake kila anapopita anaombewa kwa Mwenyezi Mungu kulingana na unyenyekevu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasisitiza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tunamshukuru kwa sababu sisi wazalendo tunaomwombea mema kwenye Taifa hili la Tanzania Mwenyezi Mungu anakubali na anampa macho ya rohoni anakwenda kuwateua watu muhimu kama hawa akina Mheshimiwa Jerry Silaa. Mwenyezi Mungu aendelee kusimama na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake yote, tunaikabidhi mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa jina la Yesu Kristo, Amina. (Makofi)