Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makunduchi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuweza kuniona leo hii katika kuchangia Bajeti ya Wizara ya Ardhi. Pili, niseme kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kutuchagulia mtu wetu huyu Mheshimiwa Jerry Silaa kwa namna ambavyo alivyomwona katika hali ya utendaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutamzungumzia Mheshimiwa Jerry Silaa ambaye ni kiongozi wangu nimetoka naye kule akiwa kama Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, mwanzo kabla ya kuteuliwa nilimwambia maneno, mara ya pili baada ya kuteuliwa nayo pia nikamwambia maneno sijui kama anayakumbuka. Nilizungumza neno la Kiarabu nilimwambia al-mujtahidu-l-wajada. Sasa kama al-mujtahidu-l-wajada maana yake kwamba kwa kila mwenye kujitahidi Mwenyezi Mungu humpa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa ndugu yangu Mheshimiwa Jerry haikuwa bahati mbaya kwa kuchaguliwa kuwa Mheshimiwa Waziri katika Wizara ya Ardhi, amechaguliwa kwa sababu ya jitihada zake na hilo maana yake aliweke kila anapokwenda na Mwenyezi Mungu ampe hekima hiyo ya kuweza kuwaongoza watu kwa hekima na maarifa.
Mheshimiwa Spika, labda pengine nimwambie tu Mheshimiwa Waziri kwamba tunampa pongezi nyingi sana lakini hizi pongezi ambazo tunampa na hizi sifa ambazo tunampa kwake yeye iwe ni changamoto. Asije akafanya hizi sifa tunazompa zikaja zikamfanya kwamba akaja akatoka nje ya reli. Hayo kwake yeye maana yake yawe kama ni changamoto na aone wazi kwamba wanaonisifia ni binadamu wenzangu kama kawaida, kwa maana hiyo maana yake kwamba nifanye kazi kwa mujibu wa hali ambayo Mwenyezi Mungu atakayonijalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije katika mchango wangu wa Wizara ya Ardhi. Ukweli katika hali ya kisomi kuna wengine wamechukulia suala la ardhi wakachukulia ule msemo wa chama chetu kwamba ardhi, watu na kadhalika kwamba ndiyo vitu vya msingi lakini katika masuala ya uchumi ardhi maana yake ni moja ya jifya ya uchumi namba tatu. Katika suala la uchumi tuna vitu vitatu, tuna suala la ardhi, tuna suala la wafanyakazi (labour) na suala na mtaji.
Mheshimiwa Spika, lakini suala ambalo ni kubwa sana ni suala la ardhi, ardhi maana yake ni uchumi katika nchi yetu. Sasa nitazungumzia kwamba ardhi ni uchumi katika nchi yetu kwa sababu ardhi ina mambo mengi. Katika ardhi maana yake ndani yake ndimo mnamofanywa shughuli za kilimo, katika ardhi ndimo tunapopata maji ya kunywa, katika ardhi ndimo tunapofanya viwanda vyetu, katika ardhi ndimo tunamofanya kila kitu chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie suala moja tu ambalo limezungumzwa na watu wengi sana hapa katika michango yao Waheshimiwa Wabunge na kila mmoja anazungumza kwamba kwenye matumizi ya ardhi maana yake hakupo vizuri lakini mimi nione kwamba katika matumizi ya ardhi kitu ambacho kinakosekana; bahati nzuri kwamba katika Wizara yetu tuna Tume ile ya Mipango inayoshughulika na masuala ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, tusitosheke na ile Tume, nimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba, lazima tuwe na National Land Use Integration Planning ambayo ni ya Kitaifa ambayo michoro yetu ya ardhi maana yake tufanye suala la mapping, kui-map nchi yetu na shughuli za kiuchumi. Kwa mfano Tanzania mpaka hii leo tunavyokwenda maana yake tunajaribu kuwashauri Waheshimiwa Mawaziri.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano juzi Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, kila mmoja alishauri katika mkoa wake maana yake kuwe na viwanda. Kitu ambacho maana yake hakujafanywa ile mapping na suala la planning ya ile ardhi nini kitakachofanyika katika sehemu zile maana yake hicho kinakosekana. Sasa ushauri wangu mimi labda pengine tuige kule Zanzibar maana yake Zanzibar wao wameandaa na wamekifanya kitu wanachokiita Integration Land Use Plan and Strengthen Land Management and Administration in Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ile maana yake itasaidia nini? Inasaidia katika ku-map zile sehemu zote za ardhi kwa mujibu wa nchi yetu nzima ambayo ilivyo kwa kuangalia matumizi ya makazi ya watu, kuangalia matumizi ya kilimo, kuangalia matumizi ya utalii, kuangalia na matumizi ya shughuli za kibinadamu. Vilevile maana yake katika utaratibu huo tunatakiwa pia tuwe na yale maeneo ya wazi, kitu ambacho hata Waheshimiwa Wabunge hapa walizungumza sana kuhusu kuweka marufuku sana kwa sehemu za wazi hata katika hotuba ya Waziri amesema katika jambo ambalo atalikemea moja, watu kuchukua sehemu za wazi kwa sababu kuna umuhimu wake kubakisha sehemu za wazi.
Mheshimiwa Spika, umuhimu wake kwanza kwa watu kucheza, kama Waziri alivyozungumza katika hotuba yake ya bajeti, lakini kitu muhimu kikubwa zaidi kuliko yote ni suala la kiusalama. Suala la kiusalama maana yake linaangaliwa katika hali ya upana mkubwa sana, haiwezekani kwamba kwamba tumejenga makazi mahali fulani, lakini yanatoa maafa hatuna hata mahali pa kuwakusanya watu zaidi ya kuangalia maeneo ya shule na maeneo mengineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani nimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba ajaribu katika kufanya shughuli zake kupanga mipango miji ya Kitaifa na tuwe na mpango maalum wa matumizi ya ardhi. Vilevile, maana yake ni vizuri zaidi tukawa tuna kitu cha integration kwa kuzishirikisha kwanza watu wa ardhi maana yake wawepo, tunataka Tume ya Mipango ya Taifa washirikiane nayo, tunataka kwamba Wizara inayoshughulika na masuala ya Mazingira maana yake iwepo pamoja na Wizara hii ambayo tunayosema ya hakimiliki ambayo inashughulika na mambo ya miliki iwepo ili kui-map nchi yetu katika shughuli za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ardhi ni uchumi, ardhi ni faida kwa nchi yetu. Kwangu mimi kubwa nadhani ni hilo nililolizungumza na kumpa ushauri Mheshimiwa Waziri kwa suala hilo, lakini mwisho maana yake nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyofanya shughuli zake na alipoanza. Wachina wana msemo wanasema; ‘Heko’, mimi nitampa heko kwa shughuli zake na kwa namna anavyofanya shughuli zake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)