Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nami niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya yeye, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara ya Ardhi. Kazi nzuri sana wanaendelea kuifanya na hasa wanafanya kazi hiyo kwa msingi kwamba ardhi ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa letu na ndiyo eneo kubwa linalotegemewa na wananchi kimakazi lakini pia kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, ardhi kiuchumi katika wilaya yetu au katika nchi yetu haiongezeki ila wananchi tunaongezeka na matumizi yake yanaongezeka na ndiyo maana kuna migogoro ya ardhi. Kwa hiyo kazi nzuri wanayoifanya ya kuendelea kutatua migogoro ya ardhi tunaomba waendelee nayo hivyo hivyo.

Mheshimiwa Spika, sisi kwetu kule Namtumbo eneo kubwa la ardhi ni hifadhi lakini sisi ni wakulima. Kwa kuzingatia sera, Serikali iliyokuwa inahimiza matumizi bora ya ardhi na sisi tulipanga matumizi bora ya ardhi katika Wilaya ya Namtumbo. Katika matumizi hayo bora ya ardhi tulipanga katika maeneo ya kilimo, uhifadhi na makazi. Pia, tulipanga eneo la uhifadhi kwa maana ya kwamba watu wanapoongezeka, mahitaji yanapoongezeka basi ile ardhi iliyohifadhiwa ya kijiji ije kusaidia kwenye kilimo kwa ajili ya wananchi wetu kuzalisha mazao na kujiongezea kipato kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuja pia na mpango mwingine katika eneo letu la hifadhi za vijiji kwamba basi kuongeza mapato kwenye hifadhi ile tuzifanye pia kama WMA. Katika utaratibu tuliowekeana vijiji na Serikali kwamba kila baada ya miaka 10 tutafanya mapitio ili kuona kuna hitaji la ardhi kwenye kilimo baada ya watu kongezeka, lakini mpaka leo hii zaidi ya miaka 15 jambo hilo halijafanyika na kumekuwa na demand kubwa sana ya wananchi kufanyiwa mapitio ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, sasa hili nalieleza kwa sababu Wizara ndiyo wanasimamia ardhi hii. Sasa hii ni kero kubwa sana kwa wananchi, kule tuna jumuiya zinaitwa Kimbande, Kisungule na Mbarang’andu zinahitaji mapitio ya ardhi. Watu wa eneo la Mbarang’andu hususani Kata ya Mchomolo walilalamika sana kwa presha kubwa sana mpaka tukasukuma wakaenda kufanyiwa mapitio, lakini mpaka leo hakuna majawabu yanayoeleza hayo mapitio yake ya ardhi wataongezewa kiasi gani kwa ajili ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachotokea wakulima wanaonekana wanavunja sheria ya kuingilia maeneo ambayo yamehifadhiwa. Kwa hiyo sisi tunaomba Serikali itusaidie kwenye hili, haya mapitio ni makubaliano ya kisheria kwa hiyo yarudi yakamilishwe kisheria kama utaratibu ulivyofanyika wakulima waendelee kupata eneo la kulima. Watu wameongezeka wanataka kulima na uchumi wa watu wa Namtumbo unategemea kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri aliongoza safari ya Mawaziri Nane kama kawaida ya kwenda kutembelea na kuangalia migogoro au kueleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri. Walipokuja Namtumbo walienda katika Kijiji cha Lingusenguse mkaeleza maamuzi ya kutaka Kitongoji cha Semeni kiondoke pale kilipo kiende eneo lingine, wakaeleza vizuri, lakini nataka niwafahamishe kwamba kitongoji kile pale wale ndiyo asili na asili yao, hifadhi iliwakuta pale, wale hawana tofauti na Ngorongoro tofauti yao watu wa Ngorongoro wanavaa mgolole wale hawavai migolole lakini wao nao wanaishi na wanyama na wamekuwa wakiishi na wanyama miaka nenda miaka rudi, pale walipoenda ndipo asili ya babu wa babu yangu, pale ndiko asili yao na ndio walikuwa wanaishi na wanyama, sasa leo wanawaambia wanawahamisha, wanawahamisha hivi hivi tu?

Mheshimiwa Spika, dunia iko kiganjani watu wote dunia hii wanajua kila kinachoendelea siku hizi. Wanaohamishwa Ngorongoro wanawapeleka kule Msomera wanawajengea nyumba, wanawapa ardhi kwa ajili ya uchumi, wale wanaenda kuwahamisha hawakuwaambia wakiwahamisha wanawapeleka wapi na watawajengea? Kwa sababu pale Serikali ilijenga shule pale iliwatambua, wale wananchi wana mashamba yao makubwa ya chakula na ya biashara ya mikorosho, wanazo nyumba pale za kudumu, sasa wakienda kwa kauli ya wahame pale tu hivi hivi na wakaenda kusimamia wahame tu, bila kutengeneza utaratibu mzuri kama wa Msomera, watakuwa wametubagua, sisi sote ni wamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema, tofauti yetu sisi na Ngorongoro, Ngorongoro wanavaa migolole na wanatembea na sime, sisi hatuvai migolole lakini tunaishi sawa tu na wanyama, tembo, simba, fisi na wengine wote, faru tunaishi nao. Kwa hiyo, tunaomba sana uamuzi huo wauangalie nasi wasitubague.

Mheshimiwa Spika, naishia hapa, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)