Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ametujalia afya na leo nimeweza kusimama, pia tunamshukuru Mwenyezi Mungu amekurudisha salama na umefika umeingia kazini, tunaendelea kukuombea katika majukumu ya hapa na huko kwa wenzetu ambako umeendelea kuwaongoza vema, Mwenyezi Mungu aendelee kukubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ningependa kumpongeza Waziri kwa kazi kubwa ambayo anafanya, lakini Waziri ana wasaidizi, hongera sana kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akishirikiana na Waziri wake kuifanya, wamekuwa wasikivu, wamekuwa wakitusikiliza pale ambapo tumekuwa tuna changamoto.
Mheshimiwa Spika, kama sitampongeza Kamshina wangu wa Mkoa wa Tabora kwa kweli nitakuwa sijamtendea haki, Kaka yangu Hussein amekuwa ni Kamshina mzuri, amekuwa ni msikivu na wakati wote wananchi wa Tabora wamekuwa wakinipa changamoto nikizipeleka amekuwa akiwasaidia na kuwashughulikia kwa karibu kweli kweli, pia amekuwa akisimamia migogoro mbalimbali ambayo tunashukuru angalau kwa sasa wananchi wa Tabora kidogo tunapumua tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nijikite kwenye hii Tume ya Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi. Nimesema hivi kwa sababu mara nyingi sana kila ninaposimama nimekuwa nachangia kwenye hii Tume, kwa sababu ya kujua na kuona umuhimu wa Tume hii. Nilikuwa sifahamu sana changamoto hizi za ardhi lakini kwa bahati nzuri alinipa nafasi ya kuwa kwenye Kamati ya Ardhi na Maliasili, kwa hiyo nilijua na kufahamu kwamba migogoro hii na changamoto hizi nini kifanyike ili tuweze kusaidia kutatua changamoto hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumemwona Mheshimiwa Waziri na timu yake wakienda maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutatua migogoro, lakini kama Wizara ama Serikali haitatenga fedha ya kutosha kwa Tume hii ndugu yangu Waziri Jerry Silaa utasaga visigino, unamaliza mgogoro upande huu upande wa mashariki mgogoro umezuka kama jana, kama hatutafanya maamuzi thabiti ya kuiwezesha Tume hii iweze kufanya kazi yake na kumaliza kupima na kupanga kwa wananchi ili kila mmoja aweze kujua ni wapi anastahili kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama mtakumbuka ule mgogoro wa Loliondo, ni hii Tume imekwenda kusaidia sasa hivi pamekuwa patulivu kwa sababu wamekwenda kuonesha kila mwanakijiji na eneo lake, hapa utafuga hapa utalima, hapa utaishi na ndicho hicho ambacho Tume inakwenda kufanya kwenye maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, leo ninavyozungumza hapa, watu wamekuwa wakinunua maeneo kiholela, hizi fedha ambazo tunaziomba na kuzipitisha zikajenge hospitali, zikajenge shule, zikajenge vituo vya afya badala ya kufika na kufanya ujenzi wanaanza kwanza kulipa fidia kwa wale walionunua ardhi tena kwa fedha wanayoitaka wao, wakati maeneo hayo yalikuwa ni maeneo ya Serikali kiasi kwamba kama yangekuwa tayari yameshatengwa ina maana pale tukiambiwa kijiji hiki shule inakwenda, shule inakwenda kujengwa bila matatizo yoyote ya kulipana fidia ambazo ni fedha nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeona na nilikuwa najaribu kupitia maeneo mbalimbali, nimeona nguvu kubwa na ya kutosha kwa kazi ambayo Tume hii wanaifanya. Safari hii 2023/2024, kwanza tulipunguza bajeti hata ile bilioni nne ambayo walisema watawapa 2022/2023 haikukamilika, lakini 2023/2024 wamepewa bilioni 3.4 na wamefanya kazi kwa asilimia mia moja, uone ni kwa namna gani Tume hii ina uwezo mkubwa wa kufanya kazi kama tutawasaidia kuwapa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakuhakikishia kama kweli tunataka migogoro ya ardhi nchini ipungue siyo kwa Mheshimiwa Jerry Silaa kupita na kuangalia matatizo ya watu. Ni lazima tukubali kama Taifa kutenga walau kwa mwaka hata bilioni 20 ili ziweze kwenda kufanya kazi ya kupima vijiji vyetu kule. Hili linawezekana, nilikuwa napitia bajeti ya mwaka huu, Tume wametengewa eti bilioni tano! Hivi kweli tuko serious?
Mheshimiwa Spika, nakwambia kama bilioni tano hii itatoka yote Mungu shahidi, wamekuwa wakija hapa tunawapitishia fedha. Kama utakumbuka bajeti ya mwaka jana ilikuwa ya moto kweli kweli, kila Mbunge aliyesimama hapa alizungumzia kuhusu suala la Tume, Serikali ikaji-commit ikasema katika ule mradi wa LTIP Serikali itatoa bilioni 20 ili kuweza kupeleka Tume ikapime. Mpaka sasa hivi tunavyozungumza hakuna fedha iliyokwenda na wanafanya hivyo, wanatudanganya Wabunge ili tusishike shilingi zao ili tusiweze kusema sana humu ndani, wanatudanganya, wanatuambia lakini hayatekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa watuambie huu Mradi wa LTIP si umeshaanza, sasa kama umeanza kwa nini hizi fedha hazitoki zikapelekwa Tume ikafanya kazi yake? Kama Tume inahitaji shilingi bilioni 20 kwa mwaka angalau katika vijiji 8,500 kupima vijiji 1,400 kila mwaka, tutakuwa wapi, lakini bado tukumbuke Wana-CCM wenzangu…(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, unapoingia kwenye Bunge, naona nakaribishwa vizuri na makofi, nimepokea makofi jamani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, unapoingia Bungeni moja kati ya package ambayo tunapewa katika lile furushi la mabegi huwa tunapewa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ili kuangalia utekelezaji wa yale ambayo wanataka kuyafanya kwa kipindi cha miaka mitano. Moja katika vitu ambavyo wanataka kuvifanya ni kupima zaidi ya vijiji 2500 mpaka mwaka 2025, lakini mpaka sasa kama kwa trend hii ambayo tunakwenda nayo ya kupeana bilioni tatu, kupeana bilioni moja, ya kupeana shilingi bilioni tano ambazo tunaambiwa kwenye makaratasi lakini hazitoki, tutafanikisha upimaji huu?
Mheshimiwa Spika, hii ni Ibara ya 74 ambayo ilikuwa inazungumzia hilo, lakini Takwimu za Wizara zinaonesha vijiji 8,500 vinatakiwa vikapimwe, vinapimwaje kama fedha hakuna?
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie tena Tume hii ambapo na niwaambie ukweli kama tunataka kuingia kwenye uchaguzi tukiwa salama bila kelele za migogoro iliyopo ya ardhi, hii Tume nadhani ndiyo strategic point ya ninyi kuingia kwenye uchaguzi huu na kupata ushindi 2024/2025, 2025/2026. Namwambia Mheshimiwa Waziri leo kama hajaja na majibu ya maana kuhusiana na Tume hii na fedha hizi namuahidi Mheshimiwa Jerry shilingi yake nitaishika na nitaishika mpaka mwisho. Lazima wafike mahali waone umuhimu wa hii Tume, waweze kuipatia pesa ili wananchi wetu waweze kupata ahueni, lakini hata Waziri na timu yake pia wapumzike! Kwa sababu hii kwenda kila siku huko, atakutana na mambo mengine mabaya! Namwonea huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni bora tenga fedha watu wako wakafanye kazi, una watu wazuri, Tume yako ni nzuri, ina kiongozi mzuri na watendaji wake wazuri, wanao uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Waende wakafanye kazi kwa kuipa Tume na kama hawaitaki basi walete sheria, hii Tume ipo kwa mujibu wa Sheria, Sura 116, kwa hiyo kama ni Sura 116 walete hapa tuibadilishe, tuipeleke kwa Mheshimiwa Profesa Kitila kwenye Tume ya Mipango ili akiwa na Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi na kule, pengine kule wataweza kutenga fedha nyingi na hii kazi ikaenda kwisha na mwisho wa siku hii migogoro ikaweza kupungua.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)