Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Ardhi. Kwa kuanza tu niseme, mimi ni mzaliwa wa Mkoa wa Mara na desturi za Mkoa wa Mara, mara nyingi sisi huwa ni wasema kweli daima, nyeupe kama ni nyeupe itasemwa nyeupe na nyeusi kama ni nyeusi itasemwa nyeusi, pale inapolazimika nyeusi kusemwa nyeupe basi huwa tunaisema kwa sauti ya mnong’ono huwezi kuisema kwa sauti kubwa kwa sababu unakuwa umesema kinyume na matakwa yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeanza kwa kusema hivyo, niseme ukweli nimesoma taarifa ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri, nimesoma randama, wikendi yote hizi siku mbili nimejipa muda wa kusoma kipengele kwa kipengele kwa kutambua ni mdau wa Sekta ya Ardhi.
Mheshimiwa Spika, nikwambie na niwaambie Wabunge, Mheshimiwa Waziri kupitia hotuba yake na kazi kubwa aliyoifanya amefanya kazi kubwa sana, nasema hayo kwa kuwa nimekuwa mtumishi kwa miaka nane ndani ya Wizara hii na hata nilipoacha utumishi bado nilirudi mtaani kufanya kazi ya sekta ya ardhi. Kwa hiyo, kwa maana moja ama nyingine ni mdau wa sekta ya ardhi kwa zaidi ya miaka 14. Najua mfumo wa ndani wa Wizara unavyofanya kazi, lakini ukirudi kama kimtaani mtaani namna ya uendeshaji changamoto zinazowakumba wadau wa sekta ya ardhi, kule mtaani napo nazijua kwa sababu nimefanya kazi kama dalali na kwa bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge wengi humu nimewauzia ardhi. Kwa hiyo, najua changamoto za sekta ya ardhi in and out. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaposema kwamba Mheshimiwa Waziri ametutendea haki sisi wadau ni pale ambapo tumeona ameyagusa maeneo mengi ambayo ndiyo vilio vya sekta ya ardhi na wadau wa ardhi kwa miaka nenda rudi. Amegusa maboresho ya kanuni ambayo sisi kama wadau tumekuwa tukizungumza namna kanuni zinavyotukwamisha kwenye utendaji wa kazi zetu. Amekwenda kuzungumzia maboresho ya sera ikiwemo na sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, amezungumzia namna ya kutambua Wathamini (Valuers) ambao kimsingi kazi yao kubwa baada ya kufanya uthamini wale wamekuwa wakirushiwa mzigo. Ndiyo wameonekana wezi, wamekuwa wakionekana matapeli, lakini amekwenda kutengeneza mwongozo ambao unawanusuru wathamini na naamini kwa kutumia ule mwongozo hawa wathamini wataenda kuheshimika maeneo yote ndani ya nchi hii.
Mheshimiwa Spika, amekwenda kugusa maboresho mbalimbali ya sheria kwenye taarifa hii. Kubwa ambalo amelifanya ni kutambua na kuthamini private sector ambazo wanafanya shughuli za ardhi na amezirudisha na kufanya nao kazi. Mheshimiwa Waziri Mungu akurehemu umefanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu tu, kwenye hii transformation unayokwenda nayo ya mabadiliko ya sera, mabadiliko ya kanuni na mabadiliko ya miongozo kwenye sekta ya ardhi, nimwombe Mheshimiwa Waziri ajitahidi sana kuhusisha Chuo Kikuu cha Ardhi. Atambue wadau na watu ambao wamesomea kozi mbalimbali pale ili aweze kuwa-accommodate na hii transformation anayokwenda nayo asije akafika mbele akarudi nyuma, akajikuta yuko peke yake na wale akawa amewaacha.
Mheshimiwa Spika, nitaje mambo matatu ambayo Mheshimiwa Rais ametukumbuka wadau wa sekta ya ardhi na ameyagusa kwa kiwango kikubwa na tumekuwa tukiyasema ndani ya Bunge hili. Kwanza, ndani ya Bunge hili tumekuwa tukizungumzia Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi wa Taifa. Mfuko huu ulianzishwa mwaka 1991 kwenda 1992. Mwaka 2016 wakati Mifuko mbalimbali ya maendeleo ya sekta nyingi inafutwa na Mfuko huu ulifutwa. Sisi wadau wa sekta ya ardhi tuliona kama halijakaa sawasawa kwa sababu maelezo yake hayakuwa sawia.
Mheshimiwa Spika, leo ninavyozungumza na wewe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia, baada ya kulisema ndani ya Bunge amerudisha Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi wa Taifa na unakwenda kufanya kazi na kwa kuanza amewapa bilioni 15.1 ili kuunufaisha na kuunenepesha ule Mfuko na ametoa maelekezo mengine. Mheshimiwa Waziri amesema hapa bilioni 50 ambayo ipo kwenye KKK (Kupanga, Kupima na Kumilikisha) kwenye Halmashauri mbalimbali, marejesho ya fedha zile ziende zikanufaishe Mfuko huu. Tumekuwa tukisema ndani ya Bunge, ndiyo ushauri wa Bunge na umekuwa ndiyo mchango wangu kwa miaka yote mitatu. Mheshimiwa Waziri atupelekee salamu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kulifanya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo tumelisema ndani ya michango yetu ya Wabunge, tumekuwa tukisema juu ya mradi wa uboreshaji wa usalama wa miliki, fedha zimekuja kwa ajili ya mkopo bilioni 345. Tulisema hapa fedha zile hatukuona kama ni sawia kwenda kupanga matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 250 peke yake. Bilioni 300 ya mkopo kupanga matumizi bora kwa vijiji 250 ilikuwa inatumika zaidi ya bilioni tatu peke yake, bilioni mia tatu na ngapi ilikuwa inaenda wapi. Tukatoa ushauri hapa ndani ya Bunge tukamwomba Waziri aliyekuwepo Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula na Serikali kwa ujumla wake waka-review fedha ya mkopo iende ikafanye kazi ya kupanga matumizi bora ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo ninavyozungumza na wewe vijiji 1667 vimepangwa matumizi bora ya ardhi ndani ya mwaka mmoja na wametoka 2,400, leo tunazungumza vijiji 4100 vimepangiwa matumizi bora ya ardhi. Mheshimiwa Waziri, atupelekee salamu tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili na wewe mwenyewe kwa utashi wa kisiasa kuamua kuridhia kuwapa fedha hawa watu kwa ajili ya kuboresha.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho la kumshukuru Mheshimiwa Rais ni pale ambapo tumepata taarifa nzuri kwamba Sera ya Ardhi ya Taifa imekwishaidhinishwa, sasa kilichobaki ni Wizara hii na sekta hii kwenda kutoa elimu kwa wadau, wananchi ili angalau sera hii iweze kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukisema hapa, moja ya changamoto kubwa ya migogoro inasababishwa na Sera ya Ardhi ya Taifa. Sera ya Ardhi ya Taifa ina miaka zaidi ya 20 back toka 1995, watu wanakua, changamoto zimekuwa kubwa na matumizi ya ardhi yanaongezeka kila leo. Sera ile haiendani na kasi ya ukuaji wa matumizi bora ya ardhi nchi hii, tukashauri maboresho yafanyike. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri sana kupata taarifa kwamba sera ile sasa imekamilika na inakwenda kufanya kazi. Namwomba sasa kwa kuwa tayari imeidhinishwa aende akafanyie kazi sera hii, nenda akatoe elimu kwa haraka kwa sababu kuna baadhi ya maeneo yamekwama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo mojawapo ni hadhi maalum kwa watu wa diaspora. Leo Waziri wa Mambo ya Nje ameanzisha mchakato kutoa hadhi maalum kwa wenzetu ambao ni wana asili ya Tanzania lakini wako nje ya nchi ili kwa ajili ya kupewa kumiliki ardhi. Wameshindwa kuendelea kwa sababu sera haiwatambui kama wahusika halisi wa kumiliki ardhi, wamekwama. Kwa hiyo, kutoa elimu kwako ku-initiate sera hii kutakwenda kumsaidia Waziri wa Mambo ya Nje ili kazi iweze kwenda kufanyika.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo mazuri ambayo yamefanyika kwenye sekta hii ya ardhi. Ninayo mambo kadhaa kama maoni na ushauri wangu. Jambo la kwanza, nimeona hapa umetoa taarifa ya kutokulipwa kwa kodi ya ardhi kwa baadhi ya wananchi na mashirika ya umma. Hili lazima tuwe serious sana, Mheshimiwa Rais aliridhia na akafuta madeni yaliyokuwa ya muda mrefu ambayo ni ya kodi ya ardhi ambayo yalikuwa hayajalipwa na wananchi na taasisi mbalimbali, akaridhia akafuta ili watu wapate mwamko wa namna ya kuanza kulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huzuni yangu na wasiwasi wangu ni pale ninapoona kwenye taarifa ya Waziri, pamoja na mazuri aliyofanya Mheshimiwa Rais maoni yake ya kufanya hivi bado mashirika ya umma yamelimbikiza zaidi ya bilioni 136, hayataki kulipa kodi ya ardhi. Sasa wanaturudisha kule kule nyuma, Mheshimiwa Rais anafuta madeni, wanaanza kulimbikiza madeni ambayo hayana msingi wowote. Nichukue nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa ametoa mwezi mmoja kwa wananchi kulipa kodi ya ardhi na namuunga mkono, akianza utekelezaji wa agizo lake aanze na haya mashirika ya umma haya ambayo yanamwangusha Mheshimiwa Rais, haya ambayo hayataki kulipa kodi ya ardhi na wakati wamepanga kwenye bajeti.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ashughulike kwanza na haya mashirika ya umma, ndiyo aje kwa mwananchi mnyonge ambaye anatakiwa kulipa shilingi 2,000 wakati kuna bilioni 136 zimekaliwa na haya mashirika ya umma ambao ni wateule na wateuzi wa Mheshimiwa Rais. Hawafanyi vizuri na wanamwangusha Mheshimiwa Rais. Naomba uanze na haya mashirika walipe hii fedha kwa sababu hii fedha inakuangusha wewe, inaonekana unashindwa kutimiza lengo lako la makusanyo la kila mwaka kwa sababu kuna fedha kama default wameshikilia hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili kama ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kuhusu kuchelewa kulipwa kwa uthamini (valuation report). Hili nimeona Mheshimiwa Waziri ametoa mwongozo, naomba asimamie mwongozo huu.
Mheshimiwa Spika, mwananchi anapopisha eneo kwa maslahi mapana ya umma, likafanyiwa uthamini na likatakiwa lilipwe aidha na Serikali au taasisi fulani, Sheria ya Uthamini inasema eneo hili linatakiwa lilipwe na thamani ile inatakiwa ilipwe ndani ya miezi sita peke yake. Leo tunaona wananchi wanapisha maeneo baada ya kufanyika uthamini inachukua miaka sita, kumi na miaka nenda rudi kinyume kabisa na Sheria. Mheshimiwa Waziri kwa sababu ametoa mwongozo aende akakatae hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili jambo kwanza linatengeneza mgogoro kwenye maeneo hayo. Pia, linazalisha na kuonekana wale wathamini (maskini ya Mungu) hawafai na wakati siyo kazi yao. Yule amekwishafanya uthamini, amekabidhi uthamini kwa mtu husika, asipolipa kiasi kinachotakiwa wanarudisha lawama na wanatengeneza mgogoro ambao hauna msingi. Niombe sana kama ni Serikali wakifanya uthamini walipe kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo ni ushauri wangu ni usimamizi wa masharti ya uendelezaji wa miliki. Mheshimiwa Waziri, ametoa siku 90 kwenye maeneo ambayo hayajaendelezwa yaweze kuendelezwa na yasipoendelezwa atagawa kwenye maeneo mengine. Sina shaka na namuunga mkono kwenye hili. Hata hivyo, tutambue kuna baadhi ya maeneo hayajaendelezwa kwa sababu huduma za kijamii zinakosekana.
Mheshimiwa Spika, mtu anashindwa kujenga nyumba au kiwanda kwa sababu hakuna barabara, hakuna maji na hakuna umeme kwenye eneo lile. Pia, kwa kuwa kwenye umiliki wa hati, mtu analipa hati analipa kitu kinaitwa premium (malipo ya mbele). Premium kazi yake ni kuhakikisha huduma hizi ninazosema zinapelekwa kwenye maeneo yale. Mheshimiwa Waziri, sasa utakapoanza utekelezaji wa kuwanyang’anya wale watu maeneo kwanza tazama hili linasababishwa na nini? Inawezekana anataka kujenga hakuna barabara, maji au umeme. Mheshimiwa Waziri akimnyang’anya na kwenda kwa mtu mwingine tutakuwa hatuwafanyii kazi watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namalizia dakika moja. la mwisho ambalo nimwombe Mheshimiwa Waziri ni namna ambavyo Mabaraza ya Ardhi ya wilaya yanavyokuwa yakilalamikiwa kwa kuchukua rushwa na kutokutenda haki. Kesi ya Mabaraza ya Ardhi ndani ya vijiji kwenye haya maeneo, yanachukua zaidi ya miaka miwili kwenye kesi ndogo tu. Leo unakwenda unapigwa kalenda kwamba njoo miezi sita, njoo mwaka mmoja. Hawa wananchi ni wanyonge na wanaumia. Niombe Mheshimiwa Waziri aweze kulitazama hili kwa maboresho mazuri.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naomba nimalizie kwa kusema kazi nzuri imefanyika. Tunamshukuru sana Waziri, akaze moyo na naamini anafanya haya kwa kufuata mikono na miguu ya watangulizi wake Mheshimiwa Lukuvi na Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula. Mungu ambariki sana hongera sana na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)