Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Ardhi. Pia, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. Hakika wamekuwa mkifanya kazi kubwa na nzuri ndani ya Wizara hii ya Ardhi kwa muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kufanya kazi nzuri na kuongeza kasi ya upimaji ambapo zaidi ya vijiji 1,000 vimepimwa. Niendelee kuiomba Serikali iendelee kuongeza pesa kwenye Tume ya Upangaji wa Ardhi ili vijiji vingi viendelee kupimwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichangie mchango wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na migogoro mingi kwenye Mabaraza ya Ardhi. Kwanza, kwenye haya Mabaraza ya Ardhi, Wenyeviti wamekuwa hawalipwi fedha zao kwa wakati, jambo ambalo linasababisha rushwa kubwa ndani ya Mabaraza haya. Niiombe Serikali iweze kuwalipa Mabaraza ya Ardhi fedha zao kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwenye Mabaraza ya Ardhi. Katika baadhi ya Wilaya bado hakuna Mabaraza ya Ardhi. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie zile wilaya zitakazokuwa hazina Mabaraza ya Ardhi.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
TAARIFA
SPIKA: Mheshimiwa Munira kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cosato Chumi.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe Mheshimiwa Munira Taarifa kwamba, hata sisi wananchi wa Mufindi mpaka sasa bado hatuna baraza hilo na ndicho ambacho nilikuwa naandika hapa kwenye mchango wangu wa maandishi. Kwa hiyo, ni kweli kwamba kuna maeneo bado watu hawana Mabaraza ya Ardhi. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Munira, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Spika, naipokea na niiombe Serikali iweze kuangalia zile wilaya zote ambazo zilikuwa hazijapatiwa bado Mabaraza ya Ardhi waendelee kuwapatia Mabaraza haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niongelee uthamini. Wizara imekuwa ikifanya uthamini kwenye ile miradi ambayo ilikuwa inakuja kufanya miradi ya maendeleo lakini kumekuwa na changamoto kubwa ambayo imekuwa inasababisha migogoro ya ardhi. Wanafanya uthamini lakini fedha zinachelewa kutoka kwa wananchi. Wanatoa fedha baada ya miaka mitatu au minne mpaka miaka sita jambo ambalo Serikali yenyewe inapata hasara kwa sababu inabidi iende ikafanye tena uthamini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia wananchi wamefanyiwa uthamini leo wanakuja kulipwa baada ya miaka sita. Wengine wanataka kulipwa kwa fedha ileile ambayo walikuwa wamefanyiwa baada ya miaka sita jambo ambalo limekuwa linasababisha migogoro mingi kati ya Serikali na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali isifanye uthamini mpaka mradi unapokuwa upo tayari kwa ajili ya kutekeleza na ambapo Serikali tayari ina fedha za kuwalipa wale wananchi ndiyo iweze kufanya uthamini na waweze kulipa fidia kwa wakati. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri anabeba mzigo ambao ulikuwa siyo wake, lakini mathalan uthamini unafanywa ndani ya Wizara ya Ardhi huu mzigo tutaendelea kumbebesha yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna fedha za miradi ya KKK. Kuna halmashauri hadi leo hii zinadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 27 wakati kuna nyingine hazijapatiwa fedha hadi leo. Niiombe Wizara itafute namna nzuri ya kuweza kurejesha fedha hizi ambazo kuna halmashauri nyingine zinahitaji fedha kwa ajili ya kwenda kupima vijiji vyetu. Niiombe sana Wizara itafute njia nzuri ya kuweza kurejesha fedha hizi ili halmashauri nyingine ambazo zina uhitaji ziweze kupatiwa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna migogoro mikubwa ya ardhi. Migogoro hii inatokana zaidi na wawekezaji ambao walikuwa wanamiliki mashamba makubwa. Pia, kuna migogoro mingine ya hifadhi na wananchi. Niwaombe sana Serikali iangalie wawekezaji hawa ambao wanamiliki maeneo makubwa. Maeneo ambayo hayajaendelezwa wakae chini na wawekezaji hawa kuangalia namna nzuri ya kuweza kupunguza maeneo yale ili kuwapatia wananchi waweze kufanya shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, migogoro hii inasababisha wananchi na wawekezaji kugombana jambo ambalo halileti tija kwenye nchi yetu. Tuiombe sana Serikali iangalie namna nzuri. Tusishikilie wawekezaji hawa wana hati tu na ni wamiliki, lakini tuangalie wananchi wetu wanakosa maeneo ya kulima, wanakosa maeneo ya ufugaji na wanakosa maeneo ya kujenga nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu bado tunaongezeka mwekezaji yupo mmoja, haendelezi maeneo. Kwa nini tusikae na wawekezaji hawa tukaangalia namna nzuri ya kuweza kuwapunguzia wananchi maeneo haya ili wapate maeneo ya kulima? Tunaingia mgogoro ambao hauna sababu. Mwekezaji anamiliki zaidi ya hekta 25,000 maeneo hayo hajaendeleza. Tuangalie namna nzuri mwekezaji apate eneo la kuendesha miradi yake na wananchi wapate eneo la kulima na kufugia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine la migogoro ya ardhi kati ya hifadhi na wananchi. Waende wakaangalie namna nzuri ya kuweka beacon ambazo zinaonekana kati ya hifadhi na eneo la mpaka la kijiji. Jambo hili litaondoa zaidi migogoro kati ya wananchi na hifadhi. Niiombe sana Wizara ishirikiane na Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia namna nzuri ya kuweza kuondoa migogoro hii ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niiongelee Tume ya Mipango. Tume ya Mipango imekuwa ikifanya kazi nzuri kwa sababu inapima vijiji lakini bado haijapewa fedha za kutosha. Tuiombe sana Serikali iwape pesa hii Tume waende wakapime vijiji, watakapowapa pesa tutaondoa migogoro mingi kati ya wananchi na Serikali. Pia tutakapoipa Tume tutaenda kupima maeneo mengi zaidi ya vijiji 1,100 ndani ya mwaka huu vimepimwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutakapoendelea kuwapa fedha wataenda kupima vijiji vingi zaidi. Kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali, iendelee kutoa fedha kwa Tume ili waweze kwenda kupima maendeo mengi zaidi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)