Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa fursa hii ya kuchangia Wizara nyeti sana ya Ardhi. Pia ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ya kutupatia uhai leo hii tena.
Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya, Naibu Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Geophrey Pinda, Katibu Mkuu ndugu yangu Sanga na Naibu Katibu Mkuu na watalaamu wote wa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia mchango wangu baada ya kuwa nimepitia ukurasa namba 15 unaozungumzia usimamizi wa masharti ya umiliki. Kama kuna mahali kuna migogoro mingi nchi hii ipo katika sehemu hii ya ardhi. Wizara wameendelea kujitahidi kila wakati kuhakikisha kwamba inapungua, lakini kadiri wanapopunguza ndivyo inavyoanza tena.
Mheshimiwa Spika, hapa kwenye usimamizi wa masharti ya umiliki bado kuna changamoto, ndipo mahali ambapo watu wanakwenda kuangalia zile hati lakini wanagundua kwamba kuna watu wengi tu hawana hati. Nimesikia wachangiaji wengi wakionesha kwamba 30% tu ya ardhi ndiyo iliyopimwa. Tuna kitu cha kufanya kwenye upimaji, na kama hatukifanyi sasa maana yake migogoro itazalishwa kila baada ya muda mfupi unaokuja.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo nilikuwa napitia Taarifa ya Mheshimiwa Waziri hapa ukurasa namba 28 nikaona ameweka mazingira yanaonesha wazi kwamba, ifahamike kuwa jukumu la Wizara ni kuratibu uthamini na wajibu wa kulipa fidia ni wajibu wa atakayenufaika na ardhi atakayokuwa amechukua, na kwa nini nimekimbilia kwenye uthamini huu, ni kwa sababu kuna uthamini na fidia. Jimboni ninakotoka kuna uchimbaji wa madini ya dhahabu na madini mengine, kama kuna changamoto ambayo inatafutiwa majibu na bado majibu yake hayajapatikana vizuri ni pale tunapozungumzia habari ya umiliki wa juu wa ardhi na umiliki wa chini wa ardhi (surface right na mineral right).
Mheshimiwa Spika, mwananchi ambaye ameishi mahali fulani kwenye ardhi yake kwa zaidi ya miaka 40 au 50, kwa bahati nzuri imetokea dhahabu eneo la chini anaambiwa sasa anatakiwa afanyiwe tathmini afanye uthamini na apewe fidia. Sasa anatokaje pale? Bahati nzuri mchimbaji anayekuja anakuja kuchimba open cast, maana yake anakwenda kubomoa ile ardhi ya juu, kwa hiyo hawezi kuishi mahali pale. Kwa hiyo kumekuwa na changamoto kubwa ya hizi sheria mbili. Wananchi wengi wanalalamika kwa sababu kuna wakati wanaondolewa wanaambiwa pale ulipotoka unatakiwa ulipwe labda shilingi milioni mbili. Mwananchi huyo ameishi miaka 12, sasa akilipwa milioni mbili huko anakohamia milioni mbili itafanya kazi gani?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana na niishauri Serikali, watu wa ardhi na watu wa madini wakae chini, wamekwishafanya kazi nzuri sana, lakini waendelee kuboresha eneo hili kwa sababu migogoro yake bado inafukuta kwenye maeneo tuliyopo. Wananchi wengi wanaohama, kwa sababu inawezekana malipo yao ni kidogo, badala ya kuendelea wanapata taarifa kwamba yule aliyeingia kuchimba pale kwao amepata labda bilioni tano lakini yeye alichukua milioni tano ama milioni sita. Kwa hiyo anaendelea kuumia ndani ya moyo wake na kwa hiyo migogoro hii inashindwa kwisha.
Mheshimiwa Spika, tujue kabisa surface right itafanya nini kama mtu huya amekuja kuchimba eneo hilo. Ikiwezekana huyo anayekuja kuchimba ampe basi ubia kidogo hata wa percent wakati huyu mtu anaondoka kwenye eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hili ambalo nimelisema la surface rights kuna suala wanasema kwenye sheria, kwamba tunapokwenda kulipa hiyo fidia, fidia lazima iwe kamilifu, iwe ya haki na ilipwe kwa wakati. Kwa lugha ya Kisukuma wanasema it should be fair full and prompt compensation. Hoja yetu hapa ni kwamba je, hawa wanaokwenda kulipwa hizi fidia, je, ni fidia kamilifu? Ni fidia zinazolipwa kwa wakati? Nimesikia watu wengi wanasema kwamba mtu anakwenda kulipwa fidia baada ya miaka sita lakini sheria inasema baada ya miezi sita; na wanaonesha kwamba baada ya miezi sita inabidi iwekewe riba. Sasa je, riba hizo zinalipwa? Niombe tu Wizara iangalie namna ya kuwasaidia hawa ambao tunawazungumzia. Yako maeneo mengi ambayo ukienda sasa hivi utakuta migogoro mikubwa tuliyonayo ni ya hiyo surface rights na mining rights.
Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nilitaka kuchangia eneo hili ni ukurasa namba 30 unaozungumzia Sheria ya Mipango Miji. Tumekuwa tunasema humu ndani kila siku kwamba sasa kuna maeneo ambayo inaonekana vijiji vimeiva kwa ajili ya kupandishwa, lakini havipandishi. Hapa kwenye ukurasa huu wa 30 ambao ameandika Mheshimiwa Waziri hapa anaonesha wanashughulikia kuona maeneo yaliyoiva. Tunayo maeneo mengi yaliyoiva, lakini hayapandishwi. Nina maeneo kule kwangu Katoro, nimekuwa nikisema kila siku, yana jumla ya watu laki tatu kama na thelathini na moja. Sasa watu 331,000 unahisi eneo hili bado halijaiva? Limekwishaiva tayari, hivyo twende kwenye upandishaji.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita, tulikopeshwa fedha kwa ajili ya kupanga miji, zaidi ya milioni 600 ambazo zimekwisharudishwa. Sasa niwaombe watu wa ardhi, tukopesheni tena ili tuendelee kupanga miji yetu kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, yako maeneo katika eneo ambalo mimi natoka; Katoro nimekwishaitaja, Nyarugusu, Bukoli, Nyakagwe Rwamgasa, Chigunga na Chikobe na mengine mengi yamekwishaiva kwa ajili ya kupandishwa. Niwaombe sana watu wa ardhi hasa wale wanaoshughulika na upangaji wa miji waende wakalifanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, suala la tatu ambalo ninataka kulizungumzia ni kuhusu Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi. Tume hii imezungumziwa sana hapa. Hoja ni kwamba, tumekwishapima 30%, moja ya tatu, vijiji 4,000, lakini, kati ya hivyo vijiji 4,000 ni matumizi mangapi ya ardhi yanayoheshimiwa, kwa sababu tunaweza kuona kwamba tumepima eneo kubwa lakini wanaoheshimu wako tu ni vijiji 500.
Mheshimiwa Spika, ninafahamu matumizi bora ya ardhi sehemu nyingi tumeweka; kwamba hapa ni sehemu watu wataishi, sehemu fulani itakuwa ni kwa ajili ya ufugaji, sehemu fulani kwa ajili ya kilimo na maeneo ya wazi; lakini utashangaa hakuna anayemheshimu mwenzie. Sehemu ambayo tulisema ni kilimo utashangaa wafugaji wamekwenda kulisha ng’ombe; sehemu ambayo tumesema ni mifugo wakulima wamekwenda kulima huko; kwa hiyo unaweza ukashangaa. Shida tuliyonayo hapa ni usimamizi. Matumizi bora ya ardhi tuliyoyaweka yanasimamiwaje? Je, wananchi wanayo elimu ya kutosha ya kuhakikisha kwamba matumizi bora ya ardhi ambayo tumeyaweka yanaweza kufanyiwa kazi vizuri? Kama hawana tutaendelea kuona migogoro inaendelea.
Mheshimiwa Spika, katika hili la migogoro tumeunda mabaraza ya ardhi. Mabaraza mengi katika wilaya nyingi ambazo tunazo hayana Wenyeviti wa Mabaraza. Sasa kama haina Mwenyekiti wa Baraza, na labda Mwenyekiti wa Baraza Geita inabidi asafiri kutoka Mwanza. Mwanza kuna migogoro lakini anakwenda kushughulika na Baraza la Ardhi la Geita. Huyu anakwenda kila baada ya miezi mitatu au minne, migogoro kule inazidi kukua na inazidi kuwa mingi. Kwa hiyo niombe sana hawa wenyeviti nao waongezwe kwenye mabaraza haya. Pamoja na kuyaunda lakini yawe na wenyeviti ambao ni wakazi, hivyo wanaweza kutatua migogoro hii kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, tusipofanya hili migogoro hii baadaye inahama inakwenda mpaka kwenye jinai; watu wanaanza kufika mahali wanauana, wanaumizana kwa sababu uamuzi wa migogoro hiyo umechelewa. Inatakiwa mgogoro wowote uamuliwe kwenye infant stage, kwenye stage ile ya kwanza, lakini kwa bahati mbaya tunachelewa sana mpaka migogoro inakuwa mikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na matumizi bora ya ardhi niseme tu wazi kwamba vijiji hivi ambavyo tumevipanga je, wananchi wamehusishwa? Kama hawajahusishwa vizuri matokeo yake ni kwamba yale tuliyoyaamua hayawezi kutekelezwa, na ndicho kinachotokea mara nyingi. Nimeona watu wengi wakishughulika na matumizi bora ya ardhi wanaanza hatua ya kwanza, hatua ya pili, hatua ya tatu, hatua ya mwisho inaonekana kuna wananchi wengine wanapinga. Sasa haya maeneo mengi ya namna hii tunashindwa kuvuka vizuri kwa sababu ya utaratibu uliotumika.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nimwombe Mheshimiwa Waziri; kwenye hoja ambayo niliisema mwanzo, ya surface right na mining right watu wake na wataalamu wake waende kule kutoa elimu kwa wananchi ili wananchi hao wajue utaratibu huu ukoje, ili tunapokwenda kwenye maamuzi ya mtu mmoja amekuja kuzalisha amechukua amenufaika na eneo fulani wananchi wawe na elimu. Bila hivyo tutakuwa na resistance kila wakati kumbe Wizara hizi mbili wanaweza kutengeneza timu nzuri ya kutoa elimu kwenye maeneo yetu hayo na watu wakaishi kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)