Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bagamoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara yetu hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Ardhi kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Kwa kweli ni jambo lisilopingika kwamba Mheshimiwa Waziri tangu ameteuliwa katika Wizara hii anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba masuala ya ardhi yanapatiwa ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tarehe 23/09/2023 Mheshimiwa Waziri alitembelea jimboni kwangu Bagamoyo kwenye kliniki ya ardhi ambayo iliandaliwa na Mkuu wetu wa Wilaya ya Bagamoyo. Kwa kweli nimshukuru sana na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri. Siku hiyo aliyokuja amefanya kazi kubwa sana na nzuri ambayo leo hii inaleta matunda katika mji wetu wa Bagamoyo.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Bagamoyo lina migogoro mikubwa sana ya ardhi; bado ipo na inaendelea mpaka sasa haijamalizika. Katika Jimbo la Bagamoyo kuna kata mbili ambazo zinakuwa na migogoro mikubwa sana ya ardhi, Kata ya Mapinga pamoja na Kata ya Makurunge. Haya ni maeneo sugu kabisa kabisa kwa migogoro ya ardhi katika Jimbo la Bagamoyo.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mkuu wetu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge; anafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba maombi mengi ya migogoro ya ardhi anayatatua. Hata hivyo bado kuna changamoto ambazo zinajitokeza. Changamoto kubwa ambayo iko Bagamoyo ni uvamizi wa maeneo ya ardhi. Watu wengi wanavamia mashamba ya watu, wanavamia maeneo ya watu pasipo kujua na hatimaye migogoro hii ya ardhi inakwenda Mahakamani na kusababisha mahakama zinapotoa maamuzi yake watu wengi kuvunjiwa nyumba zao.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumepata changamoto kubwa sana katika Kitongoji cha Kimele ambapo zaidi ya nyumba 28 na 29 hivi zimevunjwa kutokana na migogoro ya ardhi baada ya mhusika mwenye ardhi yake kushinda kesi Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli nilikuwa nataka niiombe Serikali, watu wengi na wananchi wengi wanauziwa haya maeneo ya ardhi kwa kutapeliwa na walio wengi hawajui. Mtu anaokoteza fedha yake kwa miaka mingi anaamua kujenga nyumba yake; nyumba anaweza ikajengwa kwa miaka kumi ama kumi na tano, lakini leo hii mtu anaposhinda mahakamani nyumba inabomolewa kwa dakika tano. Kwa kweli jambo hili tuliangaliwe. Sasa hivi kuwe na mazungumzo kati ya watu wenye maeneo ambayo yamevamiwa pamoja na wahusika ambao wamejenga katika maeneo hayo ili kuwaondolea adha na hasara kubwa ambayo wanaipata kwenye ujenzi ambao wamejiandaa kwa miaka mingi katika kujenga nyumba hizo.
Mheshimiwa Spika, mgogoro mwingine uliopo Bagamoyo ni suala la GN ambayo imewekwa katika Kata ya Zinga pamoja na ya Kilomo kupisha Mradi wa EPZA; huu mgogoro huu ni mkubwa sana. Mheshimiwa Waziri huu mgogoro tulikuwa tunaomba, kwa sababu EPZD washa-declare kwamba kuna maeneo ambayo watayaacha hawatoendelea nayo. Kwa hiyo, ninaomba ikiwezekana muende mkaondoe GN katika yale maeneo ambayo EPZA wameyaacha ili wananchi hao waweze kuyatumia maeneo yao kwa uhuru kwa sababu leo hii mtu akitaka kwenda kuuza eneo lake anaambiwa huwezi kuuza kwa sababu eneo hili lina GN ambayo iko chini ya EPZA; wakati EPZA hawalitumii lile eneo. Kwa hiyo, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri alishughulikie suala hilo ili wananchi wengi waweze kunufaika na maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine ambalo lina mgogoro mkubwa sana, Mheshimiwa Waziri kuna mgogoro katika Shamba la Razaba, hili linafahamika. Shamba lile ni moja kwa moja 100% ni mali ya Serikali, hilo halipingiki lakini kuna wananchi pale wamehamia miaka mingi sana na wale waliohamia miaka mingi wengine wamefariki wameacha vizazi vyao pale. Wale watoto walioachwa hawajui kama hili eneo baba yetu kavamia; baba kafa kaacha watoto na watoto wanajua kwamba hili eneo ni mali yao, kwa hiyo, wana haki ya kuishi pale lakini lile eneo ni mali ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, wananchi wale wamenituma wanasema kwamba hawapingi maamuzi ya Serikali kwamba lile eneo siyo mali ya Serikali, lile eneo wazazi wao walivamia na wengine walikwenda pale miaka mingi karibuni miaka 15 au 20, lakini wanaomba pale katika eneo la Razaba, kuna hekta karibuni 12,000; walikuwa wanaomba angalau Serikali iwaonee huruma ikate japo hekta 3,000 iwapimie viwanja ili wawe na makazi ya kukaa wapate sehemu ya kuishi kuliko ambavyo wanahangaika hivi sasa, Serikali ikiwaambia waondoke hapa hili eneo siyo lao hawana pakwenda.
Mheshimiwa Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa macho ya huruma jambo hili. Yeye ni msikivu na anajua jinsi gani wananchi wanavyopata tabu katika suala zima la ardhi. Kwa hiyo, naomba sana awaonee huruma wananchi hawa wa Razaba at least eneo hili ligawanywe japo hekta hizo 3,000 waweze kugawiwa ili waweze kukatiwa viwanja na kuweza kuishi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni masuala ya mabaraza ya ardhi; kwa kweli kidogo bado utendaji kazi wao una malalamiko mengi. Wananchi wengi wanalalamika kwamba mabaraza haya bado haki haitendeki. Kwa hiyo, waangalie ni jinsi gani sasa kutafuta watu ambao ni makini ambao watakuwa wanatenda haki katika haya mabaraza ili wananchi wasipoteze haki zao.
Mheshimiwa Spika, la mwisho napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Nashukuru kwa pale Bagamoyo kufuta mashamba mawili; Shamba la Kiembeni, Mapinga pamoja na shamba la kwa Mchina, Kisutu - Bagamoyo; mashamba haya yamefutiwa hati na sasa hivi yako chini ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri hili Shamba la Mapinga 99% au 100% limejengwa nyumba za watu. Ninaomba basi Serikali ichukue nafasi kurasimisha rasmi lile eneo kwa wananchi wa Mapinga pale maeneo ya Kiembeni ili waweze kulipia kodi za ardhi waendelee kuishi katika lile eneo kwa amani zaidi kwa sababu ni wananchi wetu. Zipo zaidi ya nyumba 4,000 pale, kwa hiyo, leo hii ukisema kwamba unawavunjia au unawaondoa wale watu wanakuwa hawana pakwenda.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kukuomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu Mheshimiwa Rais ameridhia kufuta yale maeneo basi wananchi hawa wapate nafasi kuweza kuishi katika maeneo hayo; warasimishiwe. Otherwise nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na timu yenu yote kwa kazi kubwa anayoifanya. Migogoro ya ardhi Bagamoyo wataitatua; naona kwa mwendo wanaokwenda tutafika hatua tutafika pazuri.
Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)