Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili nichangie katika Wizara yetu hii ya Ardhi ambayo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Kwa muktadha huo naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jerry Silaa pamoja na Naibu wake kwa utendaji mzuri. Kimsingi tumemwona Mheshimiwa Waziri akipambana sana kuhakikisha ana-over whole na kuleta mabadiliko na maendeleo katika sekta hii ikiwa ni pamoja na kuondoa migogoro, kutenda haki na niendelee kumpa moyo kwamba aendelee kuchapa kazi. Kikubwa tu ni kwamba watendaji walioko chini yake hasa kule kwenye maeneo ya wilaya ndiyo kunakotakiwa kuboresha na kumulikwa hasa.
Mheshimiwa Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tunaona kazi yake kwenye maeneo mengi: kwenye ardhi, kwenye utendaji haki na utoaji haki anapambana kuhakikisha Watanzania wanaishi katika maisha ya haki katika kutendeana haki.
Mheshimiwa Spika, leo nina mambo machache na kubwa katika uchangiaji wangu nataka nizungumzie kwenye upande wa kupata hati miliki za ardhi na hasa hasa ule uaminifu wa watumishi wetu, hasa katika Jiji la Dodoma. Natoa ushauri sana hapa kwa watendaji wa ardhi. Nampa Mheshimiwa Waziri aangalie Idara ya Ardhi katika Jiji la Dodoma kuna matatizo makubwa, ndiyo chanzo cha migogoro ambayo wananchi wanakosa haki zao na wananyang’anywa ardhi yaani ni usimamizi wa watendaji wale wa ardhi (wataalamu) wanashiriki moja kwa moja kuwanyang’anya wananchi maeneo. Wao wanajigeuza kuwa wanasheria na wanajigeuza kuwa ni madalali; sasa hili jambo linakera. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi wanakwenda na genuine cases lakini haziendi mpaka mwisho ni danadana tupu. Ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri amulike sana eneo hili, linamchafua na linachafua kabisa hata taswira ya Mheshimiwa Rais ambaye amesimama kuhakikisha wananchi wanatendewa haki. Wananchi wengi wanakuwa ni wanyonge na mnafahamu mambo haya ya ardhi yanahusisha hata pia kutoa fedha kwa maana ya kulipia na nini, hasa kwenye maeneo ya kumilikishwa.
Mheshimiwa Spika, sasa mwananchi mnyonge anapokuwa hana uwezo aangaliwe, lakini hawa watu wetu wa ardhi wanapoona mwananchi hana uwezo wanampiga danadana mwisho wanammilikisha mtu mwingine au ananyang’anywa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninazo cases zaidi ya tatu, sitaki kutaja watu majina hapa, Mheshimiwa Waziri nitakuletea hayo majina; kwa ridhaa yako nitampa Mheshimiwa Waziri hizi cases ili azifanyie kazi aangalie, yaani mwananchi anakuwa kama digidigi kwenye nchi yake, hili siyo sawa. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri alitazame kwa karibu eneo hili, alijaribu kuna wakati hapa Jiji la Dodoma zaidi ya watumishi 90 waliondolewa, lakini vile vimelea bado vipo havijaisha. Namwomba sana asogelee hili eneo asilitazame juu juu tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu haya Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya pamoja na yale ya kata; mengi hayana Wenyeviti; unakuta mwenyekiti mmoja anahudumia wilaya tatu au mbili. Sasa ule mzigo ni mkubwa na wanafahamu maeneo haya ya ardhi migogoro inaanzia kwenye vijiji uende kwenye kata. Sasa ukichanganya wilaya tatu mwenyekiti mmoja inakuwa ni mzigo mkubwa. Kwa hiyo, naomba sana eneo hili Wenyeviti wa Ardhi waajiriwe ili waweze kufanya kazi ya kutoa haki kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, hapo hapo kwenye mabaraza ya kata, tumeyang’oa meno kwa kusema wawe washauri tu. Sasa wanabaki kushauri mambo ambayo wakati mwingine yangehitajika kufanyiwa maamuzi ili mwananchi apate haki, lakini wanaambiwa wanashauri na wanaposhauri huku juu tunasema hakuna wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya; maamuzi yanakuwa hayafanyiki wananchi wanabaki na malalamiko bila kutatuliwa kero zao na kupatiwa haki zao. Kwa hiyo, hili nalo nashauri Mheshimiwa Waziri alitazame kwa karibu ili kuhakikisha Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi kila Wilaya wanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu kupima maeneo kwenye miji yetu midogo, Mji wetu wa Ilongero ndiyo tunasema ni makao makuu ya halmashauri lakini nimeona juhudi nzuri zinafanyika pale kupima maeneo, lakini ni eneo dogo sana. Maeneo mengi ya wananchi hayajapimwa na tusipopima ina maana tunaandaa squatters, tunaandaa maeneo yasiyokuwa rasmi; yaani unakuwa ni mji mchafu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri naomba sana ututazame kwenye maeneo yetu haya ya miji midogo hasa hasa Mji wa Ilongero ambayo ndiyo makao makuu ya wilaya, upimwe wote ili maeneo haya yaweze kupangika vizuri na pia tukipima yanapanda thamani. Kwa hiyo, wananchi wetu nao waweze kupata angalau nini kwenye maeneo yao haya.
Mheshimiwa Spika, hiyo iende sambamba na miji midogo iliyoko kwenye wilaya yangu ikiwemo Mji wa Mtinko upimwe, Mji wa Ngamu upimwe wote, Itaja nayo ni mji unaokuwa na wenyewe unatakiwa upimwe na pale Msange papimwe ili sasa twende kwenye maeneo yetu huko tunakoenda tuhakikishe kwamba tunakuwa na miji iliyopangika na ambayo inakaa vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa leo nilikuwa na mchango huu mdogo, lakini ninasisitiza sana pale kwenye eneo la migogoro katika Jiji la Dodoma, Maafisa Ardhi wa Jiji letu la Dodoma walio wengi siyo waaminifu; wapo wachache ambao ni wazuri, lakini walio wengi cases za Wabunge na wananchi wa kawaida malalamiko ni mengi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, ninaomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja. (Makofi)