Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi, lakini karibu tena tuliku-miss sana. Wakati Baba wa Taifa anapigania sisi tuweze kupata uhuru na baada ya kupata uhuru alitangaza maadui watatu: maradhi, ujinga na umaskini; kwa muktadha huo kwenye janga hilo moja la ujinga zaidi ya Watanzania 95 walikuwa hawawezi kusoma na kuandika. Pia, tulikuwa hatuna lugha moja ambayo inaweza ikatuunganisha kama Watanganyika hata na Wazanzibar ili tuweze kuwasiliana.
Mheshimiwa Spika, bado viongozi hawa wawili waliendelea kuwa wazalendo pamoja na kujua Watanganyika hawajui kusoma na kuandika, hawawezi kuwasiliana na hakuna document yoyote ambayo wangeweza kuidadavua lakini kiongozi huyu na wenzake waliendelea kuwa waaminifu na wazalendo kuendelea kutulindia sisi vizazi ambao tupo mpaka leo akina Condester kwamba tukizaliwa ardhi ya Watanzania iwe ni mali yetu.
Mheshimiwa Spika, tunaona nchi nyingine viongozi ambao walipigania kupata uhuru waliweza kujimegea maeneo makubwa. Tunavyoongea sasa inawezekana Baba wa Taifa angeamua kusema Nyanda za juu Kusini yote ni eneo lake, tungesema nini? Sasa hivi ingekuwa ni ardhi ya kina Makongoro au angeweza kusema Mbuga za Wanyama zote ni zake. Kwa hiyo, sasa hivi kila mtalii ambaye angekuwa akiingia nchini kwetu hela zote zingekuwa zinaenda kwenye familia ya Baba wa Taifa, lakini sisi tumekiri na tumekuwa ni mashahidi kuona sisi na kina Makongoro tunaishi sote kama Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Baba wa Taifa huyo huyo alishawahi kusema kwamba hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo Mheshimiwa Waziri naomba niungane na maneno haya ya Baba wa Taifa. Tunakiri na kukubali kwamba bado ipo changamoto ndani ya Wizara ya Ardhi kwenye migogoro. Wakati siku mlipokuwa mnazindua Clinic ya Ardhi hapa Bungeni tarehe 23 Mei, 2024, ninanukuu; “Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anazitaka taasisi zinazoshughulika na masuala ya jinai kuhakikisha zinawashughulikia wavamizi wa ardhi kama wanavyoshughulikia wahalifu wa jinai nyingine.”
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo tarehe 23 Mei, 2024, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama. Hata Waziri Mkuu anakiri kwamba bado kuna watu ambao wana changamoto kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kunukuu tena maneno ya Baba wa Taifa; mwaka 1958 wakati anaendelea kupigania uhuru wa Watanganyika aliyasema maneno haya; “Katika hii nchi kama yetu ambamo Waafrika ni maskini na wageni ni matajjiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Waafrika wakiruhusiwa kuuza ardhi yao katika miaka 80 au 100 ijayo ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri na wenyeji watakuwa watwana, lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka la Watanganyika matajiri na wajanja, tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu katika muda mchache tutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kurudia hapa ambapo Baba wa Taifa anasema kwamba; litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri na wajanja, as we are speaking now Watanzania. Nachelea kusema kwamba viongozi hawa ni wazalendo; tunamwona hata Rais wa kwanza wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Rais Karume, baada ya Mapinduzi Matukufu kila wilaya iliyoko Zanzibar aliweza kujenga nyumba za Wazanzibari wenzake na kuwapatia waweze kuishi bure, ni uzalendo wa pekee, angeamua kuwaacha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nije ndani ya Wizara yako, ninakiri na kukubali kwamba migogoro ya ardhi ipo ile ambayo ni ya kiasili kama ambavyo ni desturi wanadamu kugombana tu; mnaweza mkagombana na kwenye ardhi hivyo hivyo, lakini migogoro hii ya ardhi inapoibuka tulitegemea Wizara ya Ardhi wao wawe kama Mahakama kuzuia hiyo migogoro au ikiwezekana kuisitisha isiwepo kabisa, lakini ndani ya Wizara yako wapo baadhi ya watumishi, hapa nieleweke siyo wote, wapo ambao ni wazalendo; wapo baadhi ya watumishi ambao siyo waaminifu kwa uchu wao wa madaraka na kutaka kujipatia pesa haraka haraka wameendelea kuwa chanzo cha kuchochea migogoro kwa wenzao hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya Watanzania wanauana na wanagombana na wanakufa kwa presha, lakini ni kwa sababu ya watumishi hawa wasiokuwa waaminifu. Katika hili naomba nitume salamu zangu za kipekee kwa Kamishna wetu Msaidizi wa Mkoa wa Songwe amejitahidi kuwa mzalendo katika hili, iko scenario moja hapo mbele nitaeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ameanzisha hiyo Clinic yake ya Ardhi; nataka kukwambia ndege wanaofanana huruka kwa pamoja. Mheshimiwa Waziri atakuwa analima shamba wakienda kulala usiku wenzao wanaleta magugu wanarudisha tena kwenye lile shamba. Wanaamka tena wanakusanya takataka, wenzao tena wanaendelea kuleta, ndiyo hilo kundi ambalo liko ndani ya Wizara yako. Ili hiyo Clinic ya Ardhi iweze kufanya vizuri na kuleta matunda kikamilifu na kuonesha hali ya uzalendo kama viongozi wetu waliopita ni lazima aone namna ya ku-reform tena baadhi ya watumishi ambao wako ndani ya Wizara ya Ardhi. Wameshakubuhu na wameshaota mizizi na wameshaona kwamba wao wako hawapaswi hata kuguswa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa Dodoma ni mfano dhahiri Wabunge wengine wataungana na mimi kwamba nini kinachoendelea hapa Dodoma. Mheshimiwa Waziri yupo mwananchi mmoja anatokea kule Kijiji cha Kamsamba anaitwa Mzee Kauzeni toka mimi naomba kura mwaka 2020 kila kiongozi anayemwona anaenda kulia shida yake kwa ajili ya ardhi, lakini kwa sababu wapo Watanzania wachache wajanja na matajiri ambao wameshirikiana na baadhi ya watu wa ardhi kumpora maskini huyu ardhi na kuendelea kumfanya aendelee kuwa mtwana. Wazo la Mheshimiwa Waziri litafanya vizuri kama atachagua ndege ambao wataweza kuruka nao kwa pamoja, atatafuta kundi la watu ambao lazima watambue wanaowarudisha nyuma na watu sahihi ambao watawafanya waweze kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naendelea kumnukuu Baba wa Taifa, anasema kwamba; “Ardhi ni msingi wa maisha ya mwanadamu na Watanzania wote waitumie wa ajili ya kuwekeza kwa maendeleo yao ya baadaye kwa sababu ardhi ni mali ya Taifa, Serikali ione kwamba inatumia ardhi kwa manufaa ya Taifa lote kwa ujumla na si kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu wachache.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa nchini kuna kikundi cha watu wachache, watu wachache au mtu mmoja mmoja ambao wameinuka wamekuwa ndiyo hawa Watanganyika waliosemwa zamani hawa, ambao wao wamekuwa ni wajanja na ni matajiri, lengo lao ni kuwafanya wenzao kuwa watwana.
Mheshimiwa Spika, kule kwenye Jimbo la Momba, sisi wote ni Watanzania na ni haki ya kila Mtanzania kumiliki ardhi mahali popote maadamu anafuata utaratibu, lakini wapo Watanzania wenzetu ambao, sisi tumezaliwa kwenye ardhi hiyo, tukaitunza na kuilinda toka vizazi vya babu zetu na babu zetu. Wao kwa ajili ya ujanja wao na utajiri wao, wamefika ndani ya jimbo letu na kutaka kutugeuza sisi kuwa watumwa ndani ya ardhi yetu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri aitishe hati zote ambazo ziko ndani ya Jimbo la Momba, hati zote, ziwe ni za kimila aweze kuzihakiki. Nimeshawahi kuchangia hapa nikamwambia Mheshimiwa Waziri, kuhusu scenario moja, Mtanzania mmoja ambaye amefika Kijiji cha Msungwe alipofika hapo akajifanya kuwa Tajiri na huyo ni mmojawapo tu. Wako wengi zaidi ya 30 na wengine hawawezi hata kuguswa wanasema wametumwa huko juu. Huko juu ni wapi kama Baba wa Taifa yeye mwenyewe aliamua kuipigania nchi hii akawaachia, huko juu ni wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili wasiwachafue viongozi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, wasimchafue hata Mheshimiwa Rais, wametumwa huko juu wapi? Amehodhi ardhi yote yeye kwa makusudi mazima na kijiji kizima kiendelee kunyanyasika. Mheshimiwa Waziri, kwa kuona yeye ni mjanja kaenda kujipatia hati kutoka kwenye kijiji kingine kwa sababu alijua kijiji hiki hakiwezi kumpatia hati. Aliyetusaidia kutambua hilo ni Kamishna wa Mkoa wa Songwe, nampongeza sana kwa moyo wake wa kizalendo. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Condester kengele ya pili imeshagonga.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, lakini tunaomba hawa matajiri na wajanja ambao Baba wa Taifa aliwakataa tuone Mheshimiwa Waziri akiwashughulikia hadharani bila kuwaogopa. Ahsante. (Makofi)