Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Waziri, yeye na timu yake yote kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kufanya. Nataka kumwambia Mheshimiwa Waziri, ana Katibu Mkuu mzuri sana, ni mnyenyekevu na ni mtu ambaye nimepata bahati ya kumfahamu tangu akiwa Mwanza, lakini anasikiliza. Sasa naamini na wengine wataiga mfano wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye vipaumbele vya Wizara, Mheshimiwa Waziri amesema anaongeza kasi ya upangaji na upimaji na umilikishaji wa ardhi. Pia, akasema kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi na mengine yaliyoko huko chini. Tukienda pia kwenye Sera ya Ardhi, Toleo la mwaka 2023 na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alipitisha mwenyewe juzi, amesema hata kwenye mpangilio, suala la kuimarisha Mfumo wa Umiliki wa Ardhi na kuwezesha raia wote kuwa na haki sawa na kupata ardhi na kulinda ardhi ya Serikali limewekwa kwenye vipaumbele namba moja. Pia kuwepo na uwazi na haki katika utoaji wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kwenye eneo hilo, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kuimarisha utawala bora. Nimeona nianze kusema maneno haya ambayo Mheshimiwa Waziri mwenyewe ameyaweka kwenye vipaumbele, lakini pia yametajwa vizuri kwenye Sera ya Ardhi. Niweke kumbukumbu vizuri kwamba nimesema naunga mkono hatuba yako Mheshimiwa Waziri na haya nitakayosema hayamaanishi kwamba siungi mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza, sisi tuna mgogoro mkubwa sana wa ardhi pale Geita Mjini. Ni mgogoro ambao tumeishirikisha sana ofisi yako, Wizara ya Madini imeshiriki sana, mgogoro huu unatokana na sheria mbili ambazo zote zinatoa haki za kumiliki ardhi ile, lakini hazimpi haki mmiliki wa asili wa ardhi ile kupata haki yake.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini inampa mtu mwenye leseni Mining Right (haki ya madini) yaliyopo chini ya ardhi. Pia, inampa haki ya kuzuia maendelezo mengine mpaka atakapotaka kuitumia. Matumizi ya Sheria hii yamesababisha kwa miaka 25 wananchi wa takriban wa mitaa saba, ardhi yao kupokwa na kunyimwa haki ya kumiliki ardhi kwa sababu ya matumizi ya sheria hii. Tumemshirikisha Chief Valuer amekuja, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Madini, tumekaa naye wiki nzima Geita, amepekua vipengele vyote vya sheria, amekosa sheria ambayo inawalazimisha wale wenye leseni kutoa hata shake hand hata ex gratia hata kulipa fidia, lakini wanaendelea kuwa na haki ya kuzuia matumizi ya ardhi ya eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kuweka hapa kumbukumbu vizuri kwamba sera ya Waziri haiwatendei haki wananchi hawa, yeye mwenyewe ameweka ya kwanza. Pili, sheria ambazo zipo haziwatendei haki, vipaumbele ambavyo vipo kwenye Wizara yako, haviwatendei haki. Mheshimiwa Waziri naomba, nilifikiria kukamata shilingi mpaka nijue hatma ya wananchi hawa ikoje, lakini sitakamata shilingi yako. Namwomba jambo hili tunataka tupate suluhu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumemwambia Waziri wa Madini maeneo yote ambayo yana migogoro hawa watu wana-renew license kwa nini yasiondolewe kwenye leseni yao? Ni kwa sababu vile vijiji sasa vinakua, watu wanaongezeka na ardhi haiongezeki. Kwenye taarifa ya Waziri amesema by 2050 kwa Tanzania ardhi itakuwa haipo, almost itakuwa haipo kwa sababu Watanzania wanaongezeka kwa kasi. Sasa hii ni haki yao ambayo ofisi ya Waziri inayo. nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba, wananchi wa Nyakabale na Nyamalembo wanamsubiri kwa hamu aende akawape hatima ya miaka 25 ya Serikali kushindwa kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi ambao upo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ardhi ilikuja na Kamati ya Mawaziri Nane, wakatoa maelekezo, wakamwelekeza Afisa Ardhi kwamba jambo hili walishughulikie na kamishna alikuwepo. Kila wakisoma sheria wanashindwa kwenda kupima, hawawezi kupima kwa sababu coordinates zinaingiliana na kusomana. Sasa tunaishi kama tunaishi mjini na nimeangalia kwenye vipaumbele vya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi. Nilidhani kwenye moja ya vipaumbele angesema kuifanya Wizara hii kuwa chanzo kikuu cha mapato cha nchi. Sasa kwa sababu haipo hata kwenye vipaumbele, ndiyo maana mitaa saba haijapimwa, ipo mjini hiyo, mitaa saba haijapimwa. Eneo takriban kilometa 154 halijapimwa, linakaliwa na watu na hakuna kodi ya ardhi inayokusanywa. Wananchi hawalipi chochote na mwekezaji hawalipi watu fidia, ni kwa sababu kitu hiki siyo kipaumbele kwenye Wizara yako Mheshimiwa Waziri. Kama kingekuwa kipaumbele kwamba kuifanya ardhi ya Tanzania kwanza imilikiwe kwa haki lakini pili iwe chanzo cha mapato, hii ardhi ingepimwa na mgogoro huu ungeisha. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hilo lishughulikiwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, amesema kwenye kuimarisha utatuzi wa migogoro ya ardhi. Kwanza nampongeza kwa kliniki yako aliyoianzisha, nampongeza sana. Ilianza mwaka jana alianzisha Mheshimiwa Mama Mabula, nampongeza sana na Waziri amekuja ameiimarisha. Nataka nimshauri na namshauri tu kwa nia njema, amesema hapa Mheshimiwa Ighondo, atakwenda kwenye wilaya ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shida ninayoiona kwenye eneo hili, hebu twende mbali zaidi Mheshimiwa Waziri, kama anaweza kwenda kwenye kliniki ya siku moja akatatua mgogoro wa miaka 20 na hakuna extra force aliyoleta, yaani hakuna nyongeza yaani hujaleta Wizara tofauti, yaani Wizara yako ileile, hapo watu wako wale wale, lakini yeye akafika siku moja akatatua mgogoro basi tatizo liko ndani ya Wizara yako. Ingekuwa akifika, analeta watu wa Mahakama, analeta watu sijui wa nani, halafu wanasaidia kwenye kutatua migogoro, tungesema hizi kliniki uwepo wake una sababu za msingi kuendelea kwa mfumo huu uliopo. Kwa sababu mimi ni muumini sana wa operesheni, naamini siku atakaposema amechoka, migogoro itazaliana maradufu kwa sababu watengenezaji wa migogoro wako ndani ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, I am so much worried kwamba Mheshimiwa Waziri ni Mwanasheria, leo ana bahati hiyo, anaenda pale anatatua mgogoro. Mgogoro wowote unaoutatua kwa siku moja nina uhakika unaacha grievance kwa watu wengine kwa sababu yuko mtu pengine amekuwa na mategemeo kwamba anayo hiyo haki. Sasa kwa bahati mbaya sana ikatokea siku hiyo mtu akagundua haki yake haikutendeka vizuri kesho yake akaenda Mahakamani akakupinga Mheshimiwa Waziri na yeye alishatoa haki hiyo pale, huko baadaye watu watasema Waziri alitumia madaraka yake vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nikataka nishauri, hebu tengeneza mfumo ndani, uwepo wako kama haupo migogoro hii iweze kutatuliwa bila wasiwasi. Yaani hata unavyozungumza hapa, mtu aliyeko Kigoma, akutane na One Stop Center ileile ambayo wewe ukifika pale unapata majibu na unatoa suluhu ya jambo lile pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe mfano, watu wa PCCB Wilayani kwangu Geita walifanya uchunguzi wakagundua kwamba kuna mwananchi ambaye Baraza la Ardhi mpaka na Mahakama Kuu iliamua anyang’anywe ardhi, lakini kumbe watu wake walipeleka ramani fake kutoa ushahidi ikasababisha yule mwananchi ashinde. Sasa kuirudisha Mahakamani anahitaji kibali tena huku. Najua akienda Waziri akisoma zile document ataamuru apewe sasa hapo, nitaona kuna vitu viwili, moja, yule wa zamani anaweza kuendelea na hukumu yake aliyoipata Mahakama Kuu, lakini huyu ana vielelezo vya kutosha kwamba ile hukumu ilikuwa induced na ramani feki ambayo ilisababisha yule mtu apate haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa jambo hili nadhani tutengeneze one stop center, iwe na wataalamu, kwa sababu ni wale wale hakuna externals wanaokuja pale ndani, waimarishwe, watengenezewe mfumo ambao haki inaweza ikatendeka in your absence. Otherwise nadhani Mheshimiwa Waziri anafanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu, Mheshimiwa Waziri tuna shida kwenye maeneo ya wakulima na wafugaji na juzi nilisema kwenye semina ya Waziri. Katika nchi hii wamezungumza Wabunge wengine kuhusu Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi, kwanza hauheshimiwi, pili haufuatwi, tatu, speed yake ni ndogo sana, lakini ongezeko la mifugo na wakulima ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie, katika nchi hii popote alipo mfugaji analima, popote alipo mkulima anafuga. Matokeo yake vijiji vya wafugaji ni wakulima na vijiji vya wakulima ni wafugaji. Sasa kinachotokea ni nini? Kadiri wanavyolima, wanawafukuza wafugaji kusogea kwenye hifadhi na kadiri wanavyoenda kwenye hifadhi wanaanzisha vijiji vipya. Maeneo yote 33% ni hifadhi yataisha na hakuna siku yatatosha. Lazima tuje na sheria kali ya kumtaka mkulima abaki kwenye maeneo ya wakulima na mfugaji akae kwenye maeneo ya wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)