Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa uteuzi makini ambao ametuletea, kijana wetu Mheshimiwa Jerry Silaa. Huyu kijana amekuwa faraja kwa Watanzania wote kwa kusema kweli, kwa hiyo, tunamshukuru sana Rais kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Rais na kumshukuru kwa kuongeza bajeti ya Wizara hii kwani imeongezeka kutoka shilingi bilioni 163.17 mpaka shilingi bilioni 171.37. Kwa hiyo tunamshukuru sana Rais, hii itamsaidia Waziri na wenzake wote kufanya kazi kwa umakini wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaona mageuzi makubwa sana yanafanyika kwenye wizara na kuna utendaji, kuna mambo mazuri yanaendelea. Nimpongeze Waziri na wasaidizi wake wote, hongera kwa kliniki za ardhi ambazo zimekuwa zinaendelea nchi nzima. Tunampa moyo, amekuwa faraja kwa Watanzania wengi, aendelee hivyo hivyo tusikukatishe tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme huyu Waziri wetu amekuwa mfano wa kuigwa kwa sababu wakitaka kumpa rushwa anatangaza anasema; “Sitaki mimi nina pesa yangu.” Kwa hiyo, hongera sana, ashikili hapo hapo na Mwalimu Nyerere alikuwa anapenda viongozi kama Mheshimiwa Waziri, aendelee hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye hizi kliniki hata tukienda hapo kwenye meza yake anatusikiliza, siyo zile tu. Nimshukuru yeye binafsi, nilimletea hoja za watu wangu kule Moshi, kwa mfano Mabogini wameitatua. Nilimletea hoja ya wapiga kura wangu wa Kibosho Mashariki na Uru, ameniahidi atakuja kutatua kule kule kwa hiyo tunakushukuru sana. Ila, kama walivyosema wenzangu wachache, kuna watu bado wanakukwamisha na naomba awe makini kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilivyokuwa naingia hapa Bungeni nimekutana na Mama mmoja anaitwa Elizabeth Donald Mbozu ni mpigakura wa Mheshimiwa Mavunde, anakutafuta, ni mama kilema lakini alikuwa anamtafuta yeye. Alishasema kwamba apewe ardhi yake na watendaji wake wanampiga danadana hawajampa hiyo ardhi. Sasa yule mama ni kilema…
SPIKA: Mheshimiwa Profesa ngoja kwanza, hilo ni jina la mtu hiyo kilema au ni mlemavu?
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, mwenye shida.
SPIKA: Ni mlemavu?
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, mwenye ulemavu.
SPIKA: Basi anaitwa mwenye ulemavu siyo kilema.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, anadai haki yake huyu mlemavu.
SPIKA: Ndiyo nakutengenezea lugha vizuri, anaitwa mtu mwenye…
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, anaitwa Elizabeth Donald Mbozu. (Makofi/Kicheko)
SPIKA: Sijui jina lake, ila anaitwa mtu mwenye ulemavu, haitwi kilema, ahsante sana. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ndiyo ni mwenye ulemavu. Kwa hiyo, nimwombe tumsaidie huyu kusema kweli. Hao wanaompiga danadana sijui nia yao ni nini na wewe ulishasema apewe eneo lake. Sasa kama kuna mtu mkubwa kuliko wewe tunataka tujue.
Mheshimiwa Spika, basi mchango wangu utajikita kwenye ardhi. Nianze kwa kusema kwamba Tanzania imejaaliwa kuwa na ardhi yenye utajiri mkubwa; kuna watu, madini, gesi, misitu, mazao na vitu vingine vingi. Mwenyezi Mungu alitupa rasilimali hizi ili tuzitawale na zitusaidie, lakini cha kusikitisha utajiri huu ambao tumepewa na Mungu, kwa bahati mbaya haujioneshi kwenye maisha ya kawaida ya Watanzania. Bado watu wetu ni maskini na ni kwa sababu mahali fulani masuala ya umiliki wa ardhi yameleta matatizo kwa Watanzania wetu. Kwa hiyo niombe kwamba kuna vitu vya kuangalia kwa umakini wa hali ya juu ili watu waweze kunufaika na hii rasilimali ardhi ambayo tumepewa.
Mheshimiwa Spika, kikubwa, wakoloni walivyokuja walitunga sheria za kutunyang’anya ardhi yetu na wakawakabidhi watu wachache. Walijitwalia zile ardhi zetu wakajimilikisha miaka 33, 66 mpaka 99. Nitatoa mfano kule Kilimanjaro, Eneo la Uchagani karibu lote, Arusha na Manyara eneo kubwa lilichukuliwa na hawa wakoloni na wakajimilikisha, lakini tunamshukuru sana Baba wa Taifa tulipopata uhuru alikuja akataifisha hizi mali akazirudisha mikononi mwa umma, ikiwa ni pamoja na mashamba na zile nyumba ambazo walikuwa wametunyonya wakajitwalia. Sasa pamoja na kumilikishwa hivi vitu na Baba wa Taifa bado tumekuwa na changamoto kwenye hizi rasilimali zetu za ardhi ambazo zipo.
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, narudia tena kule Kilimanjaro maeneo ya Siha Wilaya ya Siha, Wilaya ya Hai na Wilaya ya Moshi, sehemu kubwa ilikuwa imemilikiwa na wanalima kahawa, kwa hiyo wazawa wa kule wengi hawana ardhi ya kulima na wazee wengi ambao wametokea maeneo haya, wamekuwa manamba wanakwenda kufanya kazi kwenye haya mashamba, kwa hiyo kuna tatizo hapo.
Mheshimiwa Spika, yale mashamba ambayo yalibinafsishwa wakapewa Vyama vya Ushirika, hayatumiki vizuri vilevile. Wale viongozi wa ushirika kwa namna moja hawajayaendeleza na kwa wale ambao wameyaendeleza, bado kuna chengachenga ambazo wanafanya kuyauza kinyemela na kuyatoa kwa watu kinyemela, watu wamekuwa na shida ya ardhi lakini hawapati huduma. Kwa hiyo namwomba kitu kimoja, suala la umiliki wa ardhi ambapo watu wachache wanapewa na kuacha kuwamilikisha watu wengi ni la kuangalia kwa umakini wa hali ya juu katika nchi yetu ili tuhakikishe watu wote wanapata haki yao ya kuimiliki na kuitumia ardhi, hasa wazawa wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kitu kimoja ambacho nimekigundua, kuna watu hawajamwelewa Mheshimiwa Bashe kwenye lile suala lake la BBT. Mheshimiwa Bashe ile programu ambayo ameianzisha ni programu muhimu sana ambapo anataka awamilikishe vijana wazawa, wananchi wazawa wa Kitanzania ardhi. Tunakuwa na wawekezaji wa Kitanzania ambao watakuwa wanazalisha mazao hapahapa badala ya kuwapa watu wachache. Nitatoa mfano, badala ya kumpa mtu mmoja hekta 500, Mheshimiwa Bashe hapa anawapa vijana 50 wanazalisha, huyu mtu mmoja akifa, ule mradi wake unakuwa umekwisha, umekwenda vibaya, lakini ukiwamilikisha watu 49 ardhi hiyohiyo, ekari 500, akifa yule mmoja, wale 49 wataendeleza ule mradi na watakuwa ni wazawa na wanatoa huduma kwa nchi yao. Kwa hiyo naomba tuishauri Serikali kwenye suala la umilikishaji wa ardhi, wawe waangalifu na tuwamilikishe. Ushauri wangu sasa ni kwamba tuwamilikishe vijana wazawa ardhi ili waweze kuzalisha na kuliendeleza Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa pili kwenye umiliki wa ardhi, Wizara ya Ardhi kwa namna yoyote ile ilinde haki kwa nguvu zote, haki za kumiliki ardhi kwa wazawa. Pale ambapo tunaona ardhi imetumika vibaya, mamlaka za juu, Mheshimiwa Waziri umshauri Mheshimiwa Rais vizuri, hata kama ni kule Kilimanjaro kwamba watu hawajayatumia yale mashamba vizuri, a-revoke zile ownership, wafute zile hati wapewe watu ambao wanastahili, watakaotumia hiii ardhi sawasawa, tuwape wazawa ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule kwetu watu wengi hawana mashamba, huwa tunaomba hata twende mahali kotekote watu wameshajiandikisha, lakini pale tuna mashamba ambayo yanatumika vibaya, watu hawajapewa zile ardhi. Tunaomba, wale ambao wameshajiridhisha, wakifanya utafiti wakiona hayatumiki vizuri, m-revoke zile hati zao tuwape wananchi ardhi.
Mheshimiwa Spika, naomba, huko mbele ya safari, suala la kuwamilikisha ardhi watu wachache liangaliwe kwa umakini wa hali ya juu. Kabla hatujampa mtu ardhi, tutafakari sana kwa sababu watu huwa wanatumia wale viongozi wa vijiji kwa kuwa wanazo pesa, anakwenda, anawapa pesa, hajawashirikisha wananchi, wanapitisha muhtasari wanachukua mashamba makubwa ambayo watu wetu wanaumia.
Mheshimiwa Spika, vile Vyama vya Ushirika, zile Bodi za yale mashamba, wakishahongwa pesa kidogo, wanapitisha ownership ya mashamba inakwenda kwa watu ambao siyo sahihi. Kwa hiyo, tujitahidi tuhakikishe tumeshirikisha wananchi wote kwenye masuala yoyote yale yanayohusiana na ardhi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, tunaendelea kumwombea Mungu aendelee kumbariki Mheshimiwa Silaa Jerry, anapotoa maamuzi magumu hasa yanayohusiana na haki ya kumiliki ardhi kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja na tunakutakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yako. Ahsante sana. (Makofi)