Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na Mwenyezi Mungu atubariki wote kabisa humu ndani ya Bunge ili tuweze kutoa mawazo ambayo yatasaidia katika kuboresha sekta yetu ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naanza na pongezi. Nampongeza Mheshimiwa Rais, kwanza kwa kutuletea Mheshimiwa Jerry Silaa. Bahati nzuri namfahamu toka akiwa Mwenyekiti wa UVCCM, lakini na mimi nikifanya kazi pale Ilala Boma, enzi zile pale kwa Mzee Makamba tulikuwa tunaita Ilala Boma kwa Mzee Makamba, yeye alikuwa Meya, kwa hiyo najua utendaji wake na ninavyokumbuka, alikuwa Meya mdogo kuliko wote. Kwa hiyo, napongeza sana uteuzi hii na sisi tunaendelea kumwombea utendaji mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi ziende mpaka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mheshimiwa Geophrey Pinda, pengine wasiofahamu Mheshimiwa Pinda alinipokea mimi Wizara ya Mambo ya Nje na mimi nimekuja kumpokea hapa Mjengoni, nilikuwa namwonesha korido za hapa Bungeni kama yeye alivyokuwa ananionesha pale Foreign Affairs na alinifundisha kazi, lazima nikiri. Kwa hiyo nafahamu utendaji wake na moyo wake wa kujitoa katika utendaji wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Katibu Mkuu Engineer Sanga, Naibu Katibu Mkuu, Kamishna Mathew, Makamishna wote, Watendaji na wataalam wa ardhi kwa ujumla kwa sababu mara nyingi binadamu tumezoea kulaumu, lakini kuna wakati pia tupongeze kwa sababu pia wanafanya kazi katika mazingira ambayo ni delicate na tete.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili napongeza kuhusu hizi clinic za ardhi. Ni kweli Waheshimiwa wengi wamesema kwamba Mheshimiwa Waziri huwezi kwenda kila sehemu, lakini nataka kusema kwamba, hizi clinic kwa kiasi fulani, zimeleta amshaamsha fulani ambayo pia imeleta woga kwa matapeli wa ardhi. Kwa kweli hilo lazima tuseme, kama mtu sasa hivi alikuwa ni mjanja mjanja wa mambo ya ardhi, akienda kule YouTube akaona ile mikutano ya Waziri anavyowabana wale watu, mmh! Anapata moyo wa kurudi nyuma?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo pamoja na kwamba hawezi kufika kila sehemu, lakini kuna amsha amsha fulani ameleta, kwa kweli imesaidia sana. Nilimwambia kama shemeji yake, anatakiwa aanze kunichangia bando kwa sababu usiku nachelewa kulala, naangalia zile YouTube mwanzo mpaka mwisho. In fact, zinasaidia sana naangalia siyo kujifurahisha, najifunza pia namna ya ku-solve migogoro na namna ya kusikiliza kila upande na namna ya kufikia hitimisho, kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napongeza pia mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi ambao unatekelezwa pia katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, lakini Mheshimiwa Waziri namwomba, Mafinga bado hatujaanza utekelezaji wa ule mradi, baadhi ya maeneo wameanza lakini kuna baadhi ya maeneo nimeambiwa kuna changamoto, wamesimama kwa sababu ya taratibu fulani fulani, hebu atukwamue katika jambo hilo ili mambo yaweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya pongezi hizi, nakuja kwenye hoja zangu. Nitakuwa na hoja zangu kama mbili. Kwanza, wananchi wa Wilaya ya Mufindi, nadhani hili jambo nitakuwa nasema sasa ni mwaka wa nane toka nimekuwa Mbunge hapa 2015, tunaomba tuwe na Baraza letu la Ardhi kwa sababu wananchi wanatoka Mgololo, wanatoka Malangali, wanatoka Mtula, wanatoka Bumilahinga, ni gharama kwenda kupata huduma Iringa Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza mwananchi atoke asafiri afike Mafinga, alale, atoke Mafinga aende Iringa akapate huduma, saa nyingine tena alale Iringa Mjini, arudi tena alale Mafinga aanze kutawanyika kwenda huko maeneo ya vijijini, kwa kweli gharama inakuwa ni kubwa kwa wananchi. Nimelisema na naomba Mheshimiwa Waziri, watu wengi hapa jinsi walivyoongea, ameonesha kwamba yeye ni tumaini, tumaini la watu wengi, tumaini hata la watu ambao walipoteza haki zao miaka 20, 30, wamepata ardhi zao, wamepata haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Mufindi, tupate Baraza la Ardhi, liwe pale Mafinga. Mara ya mwisho nilipouliza, niliambiwa kwamba, tayari kila kitu kiko vizuri, kiko hatua za mwisho, sijui wamepata Wenyeviti kama wangapi, wanasubiri sijui vibali utumishi, something like that, lakini kwa wananchi kwa kweli itoshe jamani kusema Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri sana, sasa ile kazi nzuri iguse kila maeneo.

Mheshimiwa Spika, mahali ambako naomba iguse, ni Baraza la Ardhi Wilaya ya Mufindi ili wananchi wapate huduma, wasogezewe huduma karibu. Kwa kweli nitaomba katika hitimisho, mimi sina kawaida ya kushika shilingi, niliwahi kushika shilingi zamani wakati wa mambo ya vinyungu, kwa hiyo mimi sitashika shilingi ila namwomba tu Mheshimiwa Waziri anisaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, Mafinga tumetenga ekari 750 na tuliomba pale tupime kwa ajili ya Industrial Park. Ninavyozungumza hapa, Wilaya ya Mufindi ina viwanda kama 35 vya mazao ya misitu, vimetawanyika tawanyika. Tulisema tutenge eneo, tuwe na eneo kwa ajili ya viwanda, wakati walipokuwa wanatupa semina ya Mradi huu wa LTIP, niliomba kwamba, tuingize pia lile eneo, lakini Kamishna Mathew akashauri kwamba hapana huu mradi uende peke yake tutawapa Revolving Fund.

Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba kuna maeneo ambako kuna Halmashauri zilipewa hizi fedha, zikatumia ndivyo sivyo, sasa dhambi za halmashauri nyingine, tusiumie sisi wananchi wa Mafinga! Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri tuone uwezekano na sisi kupewa hizo fedha za revolving fund, tuweze kupima eneo la industrial park. Sisi kwa sababu tuko eneo ambalo ni ukanda wa kuelekea SADC, naamini litakuwa na tija siyo tu kwa wananchi wa Mafinga na kwa Taifa zima kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wengi wamezungumza hapa kuhusu migogoro Dodoma. Kwa sababu ya kazi yangu ya Mwakilishi wa wananchi na vikao vinafanyika Dodoma, kwa kiasi fulani maisha yangu yanakuwa pia Dodoma. Kwa hiyo natoa ushauri, migogoro hapa Dodoma imetajwa sana, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri, arejee kwanza mapungufu gani yalitokana na ile Sheria iliyokuwa imeunda CDA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ile sheria kwa namna moja au nyingine imekuwa ni chanzo cha migogoro hii iliyopo kwa sababu, ile Sheria jinsi ilivyokuwa, ilikuwa inatoa eneo, linapimwa, viwanja anagawiwa Mheshimiwa Chumi, viwanja anagawiwa Mheshimiwa Lucy, viwanja anagawiwa Mheshimiwa Silaa, kesho mtu anakuja anasema hili eneo lilikuwa la kwetu, lakini tayari ile ardhi ameshapewa mtu. Kwa hiyo, namwomba Waziri, naweza nikawa tofauti na watu wengine, hebu kaangalieni ile sheria ilikuwa na mapungufu gani na imeacha makovu gani kwenye Jiji la Dodoma, vinginevyo Mheshimiwa Waziri, sitetei watumishi wala sitetei wataalam, lakini mta-victimize watumishi, mta-victimize wataalam, mwisho wa siku kumbe ni makovu yaliyoachwa kutokana na ile sheria iliyokuwa imeunda CDA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili Mheshimiwa Waziri akilifanyia kazi kwa utulivu, namwambia, hata akija Malaika hapa Jiji la Dodoma, migogoro haiwezi kwisha kwa sababu kuna makovu yameachwa kutokana na ile Sheria iliyokuwa ya CDA, kwa hiyo namwomba sana.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, namwomba, kwa hapa Dodoma, kuna migogoro Mheshimiwa Waziri ndiyo maana Dodoma inaonekana kama ni migogoro, ni migogoro, ni migogoro. Kuna ile migogoro ya makundi, kwa mfano kuna hawa watu 562 maarufu kama Nala Sheli Mbili. Toka mwaka 2019 walikuwa wanapimiwa na watu wa Global, lakini mpaka leo unakuta hadi Mheshimiwa Lukuvi alikuwepo alishughulikia hili jambo, amekuja Mama Mabula ameshughulikia hili jambo, sasa kwa sababu hatukamilishi mpaka hitimisho la hii migogoro ndiyo maana Dodoma inaonekana kama ni Dodoma ya migogoro.

Mheshimiwa Spika, ukienda pale Ndachi, kuna mgogoro wa makundi yaani wa watu wengi, ukienda pale Kizota Mbuyuni ambapo kuna mgogoro kati ya wananchi na wawekezaji, kwa hiyo hii migogoro ya makundi makundi, naomba Mheshimiwa Waziri, ajipe wiki mbili aamue kwamba kama alivyoweza kufanya masuluhisho kwenye maeneo mengine, basi ajipe muda kwamba hii migogoro ya makundi ya watu wengi hapa Dodoma, nataka nihitimishe na ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mara nyingi migogoro hii inaenda inafikia 90% inaishia njiani, anakuja kiongozi mwingine anaanza sifuri, inafikia 90%, inaishia njiani, kwa hiyo namwomba aangalie hili jambo.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naendelea kusisitiza na kushauri, hizi kliniki Mheshimiwa Waziri nimeona anafanya maeneo ya mijini, hebu pia ajipe nafasi hata wiki mbili zingine, aende level ya vijiji nako wananchi tunaweza tukajikuta wana changamoto mbalimbali ambazo pia akawa amesaidia kuzipatia suluhisho.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru, namwomba mambo makubwa mawili, Baraza la Ardhi Wilaya ya Mufindi na kupewa fedha Revolving Fund Industrial Park.

Mheshimiwa Spika, namshukuru kwa kunipa nafasi, Mungu atubariki wote na nawapongeza Yanga kwa lile gwaride zuri, hata kama mimi ni Simba, Mungu awabariki sana. (Makofi)