Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Ardhi. Wizara hii kwa sasa ina Waziri mpya na tunaona anafanya kazi nzuri sana, namshukuru sana na nampongeza sana. Nampongeza Naibu Waziri, nampongeza Katibu Mkuu Wizara, Kamishna na Watendaji wote wa Wizara ya Ardhi, wanafanya kazi nzuri tunaona wanahangaika huku na kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo nataka nizungumze mambo kama matatu hivi. Jambo la kwanza ni migogoro ya ardhi. Nashauri Wizara pale ambapo kuna mgogoro wa ardhi na Wizara imepeleka vifaa vyake vyote na watendaji wake wote wamesuluhisha huo mgogoro, Wizara itoe vibali au barua kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuonyesha kwamba sisi tumefika kwenye mgogoro fulani tumefanya usuluhishi na sasa kwa Wizara ya Ardhi tumemaliza, kwa sababu tumekuwa na mambo mawili ambayo yanajitenganisha.
Mheshimiwa Spika, kuna wakati fulani kuna mgogoro wa mpaka, wanasema mpaka uko sawa, lakini ndani kuna watu wanakaa wanataka kuhama kwenye eneo hilo kwa mujibu wa Sheria za Kijiji, lakini hawahami. Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanakuwa bado wana shida na jambo hilo. Kwa hiyo, kunapotokea migogoro ya mipaka, nimwombe Waziri mhusika, kama mpaka huo wenyewe wameusuluhisha watoe barua ya kuonyesha kwamba huo mpaka umesuluhishwa na sasa kama mtu amebaki kuhama na kama siyo wao wanaomhamisha ni Wizara ya TAMISEMI basi viongozi wanaohusika waende TAMISEMI kuwaambia wahamishe mtu anayehusika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe kwenye jambo hilo kwamba kwenye eneo langu limetokea Mekomariro na tumezungumza na nyie nawashukuru sana. Kwenye kliniki ya ardhi mnafanya vizuri, mimi nawapongeza kwa hilo, mtatekeleza yale ambayo tunawashauri ili twende vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa nataka nilizungumze hapa ni upimaji wa matumizi bora ya ardhi. Sasa matumizi bora ya ardhi mnaenda kupima kwenye vijiji, mnapima vizuri. Bahati mbaya kwenye Jimbo la Bunda nawashukuru sana wamepima karibu vijiji vyote, lakini kuna Vijiji vya Hunyari, Kihumbu, Mariwanda na Sarakwa. Watu wao wa Mashirika sijui NGOs wanakuja wanalazimisha wale watu waweke WMA. Sasa nashindwa kuelewa, wananchi ndiyo wenye ardhi wanaendaje kuwalazimisha waweke WMA kwenye maeneo ambayo wao hawataki?
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri anayehusika kwenye matumizi bora ya ardhi Mkurugenzi wake ameniambia hili jambo atalikataza na ameandika barua kwa Mkuu wa Wilaya kuzuia kulazimisha wananchi kupanga matumizi bora ya ardhi kwa maana ya WMA. Kwa hiyo, nawashukuru sana hilo nalo limetoka, lakini niombe wawaelimishe wananchi. Wanapokwenda kupima matumizi bora ya ardhi wanapanga makaburi, maeneo ya malisho na maeneo mengine. Maeneo hayo wanakuta yamekaliwa na wananchi na wanashauri kwamba either mtu anayepangwa kwenye eneo la makuburi ili ahame anatakiwa apewe fidia au apewe eneo lingine la kuishi.
Mheshimiwa Spika, je kama fidia haipo? Je, kwenye maeneo ya kuishi kama hayapo? Je, kama hakuna makubaliano na kijiji anahamishwaje? Kwa hiyo waelimishe wanakijiji katika matumizi bora ya ardhi wawe wanajua tunahamaje? Maana yake unakwenda kupima halafu wale wa Serikali za vijiji wanawaambia sasa nyie tunaweka vibao tokeni hapa. Anatoka anaenda wapi? Anaendaje kwenye eneo gani kuishi na alikuwa anaishi maeneo hayo?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuwaelimishe wananchi na sheria inasema nini kwa ambaye amekuja hapa? Watueleze inasema nini kwa mtu aliyehamishwa kutoka eneo alilokuwa anakaa kwa matumizi bora ya ardhi ahamie sehemu nyingine kwa sababu hapa tumeweka makaburi, mashamba au jambo lingine? Kwa hiyo, tunaomba tupate hiyo sheria ili wananchi wawe wanaelimishwa wanajue pa kwenda.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo liko hapa naliona ni suala la malisho. Kuna vijiji sasa hivi huwezi kutenga eneo la malisho kama hawajatenga. Kama wametenga ni sawa ila kama hawajatenga maana yake ni kwamba kila mtu anaishi kutokana na anavyokaa kwenye maeneo yake. Wakienda kulazimisha watu kutenga maeneo ya malisho ambayo tayari kila mtu ana-block yake ndiyo inatusababishia tunazalisha mgogoro mwingine ambao haupo. Kwa hiyo twende pale tukubaliane kama watu wametengeneza block, ukienda kwenye maeneo kama ya Hanang, kwenye maeneo mengine kama kule kijijini kwangu kunaitwa Sarakwa na maeneo mengine kila mtu ana-block yake ya kuchungia.
Mheshimiwa Spika, sasa ukianza kumwambia toka tuchunge wote na eneo lenyewe halitoshi, wanachunga akina nani? Kwa hiyo, tukubaliane na matumizi bora ya ardhi pale wananchi wanapokuwa wanapanga ili tusiishi kwa kukariri kwamba lazima kuwe na maeneo ya malisho, lazima kuwe na maeneo fulani hapana, tuangalie hali halisi. Kama mtu ana-block yake ni block yake aendelee nayo kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hii Wizara, huwa najiuliza mambo mengi sana. Huwa nasema hivi kila siku kuna mgogoro Dar es Salaam, kila siku kuna migogoro ya Ardhi Dodoma na kila siku kuna mgogoro sijui Mbeya. Kwa nini tusitengeneze mikoa ya Majiji kama matano tukamaliza migogoro ya ardhi? Tukasema hii ni pilot area kwamba leo Dar es Salaam ni labda 90% tumefaulu na Dodoma 90% tumefaulu. Kwa nini miaka nenda rudi maeneo fulani hayaishi mgogoro? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo ukiitisha mgogoro wa ardhi hapa Dodoma ni balaa. Ukienda hata Bunda ukiitisha ni balaa? Kwa nini tusimalize migogoro ya ardhi? Kuna shida gani? Kuna shida gani ambayo hatumalizi wakati tuna vifaa vyote ikiwemo GPS na kila kitu? Kwa hiyo, niombe tujue hili jambo tukilitengeneza litakuwa zuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna vijiji vingapi vimepimwa, tuviwahi basi. Leo tunazungumza squatter ndani ya Dodoma, leo tunazungumza squatter ndani ya Bunda, kila maeneo unaweza kukuta yako hivyohivyo. Tuwahi maeneo ambayo hayajapimwa yapimwe ili tuweze kuleta vipimo vya kutosha ili maeneo haya yawe safi tupunguze migogoro ya ardhi. Migogoro ya ardhi ni shida.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo nataka kuchangia, huwa najiuliza, kuweka gharama kubwa ya ardhi mtu kununua kiwanja, mtu kupimiwa kiwanja hivi ni ubora? Hivi ni ufanisi? Hivi hakuna mikopo? Hivi si tuanze kwenye mikopo ya kukopesha watu basi? Mpime eneo, mkopeshe mwambie alipe pole pole kuna shida gani? Kuna shida gani mtu atoe hela nyingi kupima na hana? Kwa nini tusikopeshe watu sasa? Wewe bwana una eneo gani? Hili hapa, ok tunakupa eneo tunapima tunakwambia bwana lipa polepole utamaliza. Hivi kukaa na maeneo mengi ambayo hayajapimwa ni kupata hela? Hivi kuna nini? Hivi kwa nini tusitumie akili zetu za kawaida tukopeshe watu ardhi kama mtu anapima apime halafu alipe pole pole? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ya kwangu yalikuwa hayo. (Makofi)