Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kabla ya kuchangia naomba nitumie nafasi hii kukupongeza wewe kwa kazi nzuri ambayo unaifanya hususan ya kutuwakilisha huko duniani. Hakika Mungu akubariki na sisi tunaendelea kukuombea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuendelea na mchango wangu naomba kwanza nianze na pongezi. Pongezi zangu za kwanza ni kwa Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya hususan katika eneo hili la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukisikiliza hotuba nyingi za Mheshimiwa Rais na mara nyingi tumeona na tumesikia jinsi ambavyo amekuwa akielekeza Wizara pamoja na wateule wake kuhakikisha wanasimamia haki kuhusiana na suala zima la ardhi ili kila mwananchi au kila Mtanzania apewe haki yake ya msingi pale linapokuja suala zima la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende pia kumpongeza Waziri mpya Mheshimiwa Jerry Silaa kwa kazi nzuri, kubwa na ngumu anayoifanya. Kuthibitisha kwamba Waziri huyu anafanya kazi nzuri, nakumbuka mnamo tarehe 13, Machi, Mheshimiwa Rais akiwa anawaapisha Waheshimiwa ma-DC na baadhi ya Wakuu wa Mikoa alisema wazi wazi jinsi ambavyo anafurahishwa na utendaji kazi wa hii Wizara ya Ardhi. Tutakuwa ni watu ambao basi tunajidanganya ikiwa Mheshimiwa Rais, atatambua kazi kubwa na nzuri ya Waziri pamoja na timu yake anayoifanya halafu sisi tukasimama hapa tukasema Waziri hufanyi kazi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Jerry nakupongeza, lakini niseme kwamba unazo changamoto nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu unapoona hadi Rais wa nchi, anakupongeza ujue hiyo ni habari njema, lakini pia ni mtego. Ikiwa hutaenda kutimiza majukumu yako ipasavyo, basi ujue kuna siku ambayo atakwambia kwamba anachukizwa na hapendezwi na kazi yako njema. Sisi tunamwombea Waziri na tunamwamini. Binafsi namfahamu tangu kutokea huko, mimi natoka Jimbo la Segerea, yeye yuko Ukonga, utendaji wake wa kazi naufahamu vizuri na sina shaka naye.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda moja kwa moja katika mchango nina ombi kwa Mheshimiwa Waziri. Nakumbuka niliwahi kwenda kwenye kiti chake hapo na nilimweleza jinsi ambavyo mimi natoka Jimbo la Segerea kwa maana naishi Segerea, kuna wakazi ambao wanaishi Segerea ila asili yao ni ya kutoka kule Jimbo la Chalinze kwa maana ya eneo la Mbara. Sasa nilimshirikisha Mheshimiwa Waziri, jinsi ambavyo wananchi hawa wana changamoto kubwa sana au wana mgogoro mkubwa kati ya wafugaji pamoja na wakulima. Nilimweleza Mheshimiwa Waziri kwamba hata wao kuhamia Segerea na wengine nafikiri wapo Jimboni kwa kaka yangu Mheshimiwa Ridhiwani na maeneo mengine; wengi walihamia kule baada ya kuwa wamevutana sana kwa maana ya wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Spika, sasa walipoanza mambo ya kuvutana, kugombana na hata kutaka kutishana maisha, basi wengine wakaamua kujiepusha kutafuta maeneo mengine ili angalau maisha mengine yaendelee na ndiyo hivyo baadhi wakawa wamekuja katika Jimbo la Segerea. Nilimwambia Mheshimiwa Waziri na nilimpa vithibitisho kwamba ni zaidi ya wananchi 200 ambao wana huo mgogoro katika eneo la Mbara. Sasa nimwombe sana Mheshimiwa Jerry, tumeshuhudia jinsi ambavyo ametatua migogoro mikubwa kabisa kuzidi huo mgogoro wa Mbara. Tumemwona Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Arusha na kule Ilemela ameweza kutatua migogoro mikubwa sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kuwa nilishamshirikisha jambo hili na akaniahidi kwamba atafika sehemu ile asikilize na baadaye atende haki.

Mheshimiwa Spika, atakapokuja hapa Mheshimiwa Waziri kwa nia njema kabisa na kwa sababu Watanzania hawa na wakazi hawa wa Segerea wanamsikiliza. Hivi ninavyochangia wananisikiliza na wanasubiri kusikia Waziri atajibu nini? Nimwombe Mheshimiwa Waziri, aniambie ni lini sasa ambapo ataweza kufika eneo hilo la Mbara ili angalau basi ijulikane ni wafugaji au ni hawa wakulima ambao wana haki ya kumiliki ile ardhi? Mheshimiwa Waziri, nitashukuru ikiwa atanipa majibu hayo na Wana-Segerea kwa kuwa wanakufuatilia, basi hakika watazidi kumwombea.

Mheshimiwa Spika, sasa niende katika machache ambayo nimejipanga kuchangia. Jambo la kwanza kabisa Mheshimiwa Jerry, wakati anawasilisha Hotuba ya Bajeti yako hapa nilimsikiliza kwa umakini mkubwa sana. Pia, nilisikiliza vipaumbele vyake na namna ambavyo amejipanga kwenda kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu migogoro ya ardhi. Nimpongeze kwa maana vipaumbele vyake ni vizuri, lakini pia maelezo yake yamejitosheleza.

Mheshimiwa Spika, niseme pia kwa Mheshimiwa Jerry, Wizara hii kama ambavyo mzungumzaji ambaye amemaliza amesema ni zigo kubwa sana, lakini pia wewe ndiyo kwanza umeingia. Katika suala hili la ardhi Mheshimiwa Waziri Jerry, zipo changamoto nyingi au kuna migogoro ambayo kimsingi siyo migogoro ambayo tunapaswa kuisikia kila iitwapo leo.

Mheshimiwa Spika, nikienda katika suala zima la upimaji na umilikishwaji wa ardhi yapo mapungufu mengi sana. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na hii Wizara ya Ardhi, lakini yapo mapungufu makubwa sana katika upimaji na umilikishwaji wa ardhi. Nitataja baadhi kwa sababu ya muda.

Mheshimiwa Spika, kwanza kuna suala la Wizara kwenda kupima maeneo na kutoa viwanja katika maeneo ambayo hayana sifa ya kuwa makazi. Mheshimiwa Jerry ninachokwambia hapa, naongea kwa niaba ya Watanzania lakini pia naongea kwa niaba yangu mimi mwenyewe binafsi kwa sababu jambo hili limenitokea hapa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2019 nilinunua kiwanja kutokea Jiji. Baada ya kununua kiwanja kile na kukabidhiwa document zote niliweza kujenga nyumba pale kubwa tu yenye vyumba vitatu na nikajibana, nikaezeka kwa bati ya m-south. Baada ya kama miezi sita nikiwa Dar es Salaam, niliambiwa kwamba ile nyumba imebomolewa. Ni kwa nini imebomolewa? Nikarudi hapa Dodoma kufuatilia inakuwaje? Nimemilikishwa kihalali, nimejenga nyumba imekaa zaidi ya miezi sita halafu wanakuja wanabomoa kama hakuna chochote ambacho kilikuwa pale? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilivyofika hapa nilienda moja kwa moja Jiji. Nilipofika nilichoambiwa ni ile kwamba makosa yamefanyika ni kwamba mifumo haikusomana kwamba kwa hiyo, alipewa mtu mwingine. Nimenunua mimi eneo, nimepewa document zote amekuja mwingine amenunua halafu huyu aliyeuziwa ndiyo anakuja kubomoa nyumba yangu. Kwa hiyo, nilichoambiwa kwamba sasa tutakupatia kiwanja kingine. Unajua wakati mwingine kama hujajua hizi Sheria za Ardhi unaweza ukanyanyasika na imagine mimi napata majanga kama hayo? Mtanzania wa kawaida wa kule kijijini kabisa ambaye hajui lolote unaweza uka-imagine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, to cut the story short, nikaahidiwa kwamba ni makosa yalitokea, mifumo haikusomana. Sasa sijui haikusomana namna gani? Wizara inajua na wataalamu wanajua, nikaambiwa sasa nitapewa kiwanja kingine. Kile kiwanja kilikuwa kina square meter 1,870, nikaambiwa napewa kiwanja kingine. Mheshimiwa Waziri, nimekaa muda mrefu nafuatilia baadaye nikaambiwa njoo usaini hati, nikasaini document zote za hati bila kuoneshwa kiwanja. Nilihitaji nione kiwanja kabla ya kusaini ili niridhike kwamba je, kiwanja ninachopewa kinaendana na kile kitu ambacho nimepoteza?

Mheshimiwa Spika, sikuoneshwa kiwanja, baadaye nimekabidhiwa hati the same day ndiyo napelekwa kuoneshwa kiwanja. Ni maajabu, ni aibu hata kusema, lakini Mheshimiwa Jerry kile kiwanja kwamba pale kwanza hapapaswi kuwepo na kiwanja ni kwenye korongo ni kwenye mawe halafu kiwanja chenyewe square meter 450. Mimi nimevunjiwa nyumba, nimechukua kiwanja kikubwa halafu napewa kile kiwanja ambacho siyo kiwanja na siyo sehemu ya kukaa kiwanja ila nimeshikishwa hati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, so baada ya pale nilirudi jijini Mheshimiwa Jerry nikaambiwa nisubiri natafutiwa kiwanja kinachoendana na kiwanja cha kwangu. Kipindi kile alikuwepo Mkurugenzi mwingine ambaye ni Mafuru kama nakumbuka vizuri akaniambia nitapewa kiwanja kingine. Wakati yupo kwenye process zile akaondoka kabla hata sijapewa kile kiwanja na mpaka naongea na wewe sijapewa kiwanja ile hati ninayo siyo kiwanja ni korongo, ni mawe. Ukifika pale mwenyewe hata ukipewa bure kwamba hapa ujenge choo huwezi kukichukua kabisa.

Mheshimiwa Spika, sasa mpaka naongea hapa bado nilikuwa sijafika Ofisi ya Mkurugenzi mpya ndiyo leo sasa nakuja kuchangia. Natambua kwamba Mkurugenzi aliyepo anasikiliza watu na najua nikienda atanisikiliza. Nimeona niliseme hapa kwa sababu yaliyonikuta najua yamewakumba watu wengine wengi ambao hawana hata sehemu ya kwenda wala kusikilizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hilo lilikuwa ni pungufu moja wapo. Pungufu la pili na la mwisho kwa sababu kwenye mapungufu ni mengi na muda hautoshi. Pungufu la pili ni Wizara kwenda kupima maeneo ya wananchi bila kuwashirikisha. Mtu ana eneo lake na hapa Dodoma ndiyo business ya hali ya juu na mimi hilo limenikuta. Kwa sababu tumehamasishwa sana kuwekeza Dodoma si ndiyo? Kwa hiyo, watu tunawekeza Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilinunua ardhi kule Msalato nina document zote. Nimekuja kushangaa naenda pale nakuta kote kumepangwa mawe halafu mawe yamepangwa ya kupimwa viwanja ni vidogo square meter 340, 350 na hatujui nani alipima. Ukiuliza unaambiwa kampuni fulani. Ukienda kwenye Kampuni unaambiwa hii Kampuni iliacha kazi imekuja nyingine, nyingine iko wapi? Haijulikani, haijulikani and then we just give up, hayo ni mapungufu.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, nimemwona Mheshimiwa Jerry the way anavyoshirikisha watu anapokuwa anakwenda kutatua migogoro. Amekuwa akishirikisha kuanzia viongozi wa Kiserikali na wataalam. Pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Jerry, naomba nimwibie siri moja, anapokuwa anakwenda kutatua hii migogoro, sehemu nyingi viongozi wa Kiserikali ni sehemu ya hii migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unakuta ma-DC, wakuu wa mikoa, nimesema baadhi, si wote, ni sehemu ya migogoro ambayo unakwenda kuitatua. Sasa, kama ni sehemu ya migogoro unayokwenda kuitatua unapokuwa nao tayari wanakuwa wameshakueleza wanayojua wao kwa sababu ya kuwa-favour wao, unapokwenda kwa wananchi ni ngumu sana kujua ukweli na kutambua ni nani hasa ambaye ni mhusika anapaswa kupewa haki kama hii. Hatimaye unakuta, kwa mfano maeneo ambayo kuna wawekezaji kama vile sheli na kadhalika, always viongozi wa kiserikali wana-base upande wa huyu ambaye anaonekana ameshiba sana kuliko kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, ninafahamu na ninatambua kwamba zipo kanuni na taratibu za kutatua hii migogoro ya ardhi. Kwa hiyo ushauri wangu, hizo hatua pamoja na hawa viongozi wa kiserikali ambao tunawaheshimu na kutambua mchango wao, lakini kwa sababu maeneo mengi yamekuwa ni sehemu ya migogoro, basi utumie ule utaratibu na kanuni za utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, ninayasema haya kwa sababu, unakuta kuna mwekezaji amekuja kuwekeza kwenye eneo kubwa kabisa. Anachukua eneo la wananchi kwa hela ndogo au bila hata na fedha kabisa. Kiongozi wa mtaa au kijiji anapindisha pindisha mambo, hili eneo la Serikali, sijui lilikuwa eneo la wazi, ghafla unakuta amekuja mwekezaji. Anapokuja DC au mkuu wa mkoa ambao wamekaa kisiasa wanatoa matamko ya kuvunja moyo, na wote tunatambua. Naomba Mheshimiwa Jerry atambue kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anategemea wapigakura wengi ambao ni wanyonge na wanaolia kwa ajili ya ardhi. Hatutaki mwaka 2025 Mama Samia anakwenda kuomba kura, wameshika mabango wakiwa wanadai ardhi.

Mheshimiwa Spika, ninamwomba sana asimamie kanuni. Wakuu wa mikoa, ma-DC awasikilize kama watawala wa eneo hilo, lakini wasiwe ni final say ya kumweleza ni nani yupo sahihi, nani ambaye hayupo sahihi. Aende chini kabisa kule awasikilize wananchi na hatimaye naomba akatende haki. Tumemwona akiwa anatenda haki, amesimama katika maeneo magumu ambako changamoto na migogoro ilishindikana kwa miaka mingi, lakini amesimama na ametatua. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais anasema kwamba anafurahishwa na utendajikazi wake na Wizara yake. Kwa hiyo ninamwomba asimwangushe na asituangushe Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kusema kwamba nipo chini ya miguu yake, Wana-Segerea wanamsikiliza na wananisikiliza mimi pia, atuambie ni lini atakwenda pale Mbara kutatua ule mgogoro? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)