Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ninachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa kijamii, kisiasa, kiuchumi, kidiplomasia na mshikamano wakati wote; kwa kweli ametuepusha na majanga mengi sana.

Mheshimiwa Spika, pia ninachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa Jimbo langu la Mbulu Mjini kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali nzima ya Awamu ya Sita, kwa jinsi wanavyoiongoza na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025. Hongereni sana na Mwenyezi Mungu awajaalie mshikamano wenu udumu.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Jerry William Silaa, Waziri wa Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya Sekta ya Ardhi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara kwa jinsi walivyotekeleza majukumu yao ipasavyo kupitia taarifa ya Wizara iliyowasilishwa mbele ya Bunge letu hili, hongereni sana na Mwenyezi Mungu awabariki. Aidha, ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi pamoja na wajumbe wake wote kupitia taarifa yao ambayo imefafanua vyema mafanikio na changamoto.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo Sekta ya Ardhi. Kwanza tunaiomba Serikali iangalie upya utaratibu wa Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK). Kwa kweli huu ni mradi mzuri sana kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Ardhi nchini.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo mradi huu unakabiliwa na changamoto nyingi sana zikiwemo ukosefu wa wataalamu wa ardhi, vitendea kazi na mkanganyiko wa mfumo wa ukusanyaji wa malipo ya viwanja katika halmashauri zote nchini ambazo tayari zimepokea fedha za mradi huu, hali inayosababisha fedha nyingi kutokusanywa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo itakuwa vyema wakati wa Bunge la mwezi Septemba kuziita halmashauri zote zilizopokea fedha za K.K.K. mbele ya Kamati ya Ardhi na Kamati ya TAMISEMI ili kufanya tathmini ya maendeleo ya mradi pamoja na marejesho.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali ijitahidi sana kutoa fedha za bajeti ya maendeleo ya Wizara hii muhimu sana katika mwaka huu wa bajeti. Pia tunaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuajiri wataalam wa ardhi katika halmashauri zote nchini ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa katika kila mwaka wa bajeti kwa kuwa tunashindwa kufanikisha malengo ya K.K.K.

Mheshimiwa Spika, Wizara iangalie utaratibu wa kuweka mfumo wa sms ili kumkumbusha mlipakodi ya pango la ardhi kila inapofika muda wa malipo, ujumbe ambao utakuwa na control number ili kurahisisha malipo badala ya kutafuta namba ya malipo hadi ofisini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.