Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijaalia afya.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwatumikia Watanzania. Pia naomba niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake wote.

Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono hoja. Baada ya kuunga mkono hoja naomba nitoe mchango wangu katika baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuhusu kubadilishwa mpaka kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga. Mpaka huu umebadilishwa kinyemela na kwa bahati mbaya bila kuwashirikisha wananchi wa pande mbili wanaofahamu vizuri mpaka pamoja na historia ya mpaka huu.

Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza zaidi ni pale ambapo serikali ya mkoa imefikia uamuzi huo bila kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge husika. Jambo hili halileti afya hata kidogo na huku ni kukuza mgogoro bila sababu kwani umekuzwa na uongozi wa Manispaa ya Sumbawanga kwa matazamio ya kuja kujenga uwanja mpya katika eneo la Kijiji cha Kisumba ambalo mimi binafsi nilikuwepo likiwekwa jiwe na msingi na aliyekuwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Gharib Bilal. Ninaiomba Wizara iingilie kati baada ya uongozi wa mkoa kushindwa kutenda haki.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upimaji na upangaji wa vijiji na miji midogo inayokua kwa kasi kubwa kuliko upimaji wa viwanja, haina tija kwa dunia ya leo kuendelea kujenga bila kupima (squatters) hali ambayo inapunguza hata thamani ya majengo.

Mheshimiwa Spika, Mji Mdogo wa Matai ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo kwa miaka ya nyuma uliwahi kusifiwa kuwa kati ya maeneo yaliyopangwa na kupangika vizuri, lakini kutokana na uchache wa rasilimali fedha kazi ya upimaji imepungua sana. Tuombe; kati ya halmashauri zinazotakiwa kusaidiwa kifedha basi na halmashauri yetu iwe miongoni kwani kasi ya kuendelea kujenga ni kubwa. Kasi hiyo itaongezeka zaidi pale barabara yenye kiwango cha lami kutoka Matai hadi Kasesya Border itakapokamilika.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo mawili, naomba kuwasilisha.