Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Jerry Silaa na Naibu Waziri Mheshimiwa Geophrey Pinda, Katibu Mkuu Ndugu Anthony Damian Sanga pamoja na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazozifanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu hatimiliki za mashamba ya ushirika Mkoani Kilimanjaro na mikoa mingine ambayo yalirithiwa baada ya kutaifishwa mwaka wa 1967 kutoka kwa wamiliki waliokuwa wana hatimiliki za miaka 33, 66 au 99.
Mheshimiwa Spika, mashamba niliyoyataja hapo juu yalikuwa na hatimiliki. Kifungu cha 32 cha Sheria ya Ardhi kinasema kuwa mtu anaweza kupewa hati bila kupewa chaguo la kupewa tena. Hii ina maana unapewa hati kwa muda maalum na muda huo ukiisha basi ardhi hiyo inakuwa si mali yako tena. Inapokuwa si mali yako tena ardhi hurudi mikononi mwa mamlaka za ardhi ambapo Waziri mwenye dhamana na Kamishna Mkuu wa Ardhi wanaweza kumpatia mtu mwingine ardhi hiyo akiwa kama mmiliki mpya.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ifanye utafiti wa kina ili kubainisha uhai wa hatimiliki za mashamba ya ushirika mkoani Kilimanjaro (penye mashamba mengi ya ushirika na uhaba mkubwa wa ardhi) na mikoa mingine. Maeneo haya yana migogoro kutokana na uwezo mdogo wa kuzilinda rasilimali ardhi hizi.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tumeshuhudia matumizi mabaya sana yanayofanywa na wawekezaji katika mashamba hayo, na pia baadhi ya viongozi wa mashamba haya wameshindwa kuyaendeleza kabisa kwenye baadhi ya miradi ya uwekezaji mashambani, hata zile Corporate Social Responsibility hupatikana kwa shida. Ukweli ni kwamba wananchi hawaoni kabisa manufaa ya kiuchumi kutoka katika ardhi hizi za umma.
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali kuwa sasa ni wakati wa kupitia hati za umiliki wa mashamba haya na kubaini uhai wa hatimiliki za mashamba yote. Kwa zile zilizomaliza muda, ni wakati muafaka wa kubadilisha umiliki wa mashamba hayo na kuwapatia wazawa wa maeneo husika (hasa vijana wasio na ardhi) ili wasaidiwe na kuwa wawekezaji na kuondokana na mawazo ya kuwapatia ardhi yetu wawekezaji wa nje ya Tanzania. Kwa wale wanaotumia ardhi vibaya, mamlaka ya Rais ifute umiliki kisheria na kuwamilikisha vijana wa hayo maeneo ili washiriki kikamilifu kwenye miradi ya kitaifa ya uzalishaji kama BBT.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.