Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ili niweze kuchangia hoja ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya ya kuliongoza Taifa letu, na pia kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuhakikisha kwamba Wizara ya Ardhi inaendelea kutenda haki kwa Watanzania, ili Watanzania wamiliki ardhi bila kuwa na migogoro ya aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nikupongeze sana wewe mwenyewe kwa kazi kubwa na nzuri iliyotukuka unayoifanya ya kuliongoza Bunge letu Tukufu. Sisi Wabunge tumekuwa mashuhuda kwamba unafanya kazi kubwa sana. Hongera sana na sisi tutaendelea kukuombea ili uendelee kufanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi inatokea katika maeneo ya vijiji, mitaa, kata na maeneo yote ambayo yapo chini ya Menejimenti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi mara kwa mara tumekuwa tukifanya vikao vya pamoja ili kushauriana na kuona njia nzuri zaidi za kwenda kutatua migogoro hii katika maeneo ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ili kuhakikisha wananchi katika maeneo hayo wanaendelea kupata huduma bora za ardhi, kuendelea kupunguza migogoro na ikiwezekana kumaliza kabisa migogoro katika baadhi ya maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halmashauri ndiyo mamlaka za kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa wananchi katika maeneo yao. Kwa hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeendelea kusimamia hilo, kusisitiza wakurugenzi, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuhakikisha kwamba wanasimamia kwa karibu kazi zote zinazohusiana na masuala ya ardhi, ili kupunguza na kuondoa migogoro hii na kuwezesha wananchi kustawi katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi kuna taratibu zake za kuitatua; na utaratibu rasmi zaidi ni wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya. Sasa, kwa sababu mabaraza haya yapo mbali na wananchi walio wengi, Serikali kwa mapenzi yaliyo mema iliona ni vyema tuanzishe utaratibu wa vyombo ambavyo vitatatua migogoro ya kawaida katika maeneo ya vijiji, mitaa na kata husika. Kwanza, kuwapunguzia umbali wananchi kwenda kutafuta suluhu ya migogoro hiyo katika mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya migogoro ni migogoro ambayo kwa kweli inaweza ikatatuliwa katika ngazi za kata. Hii inawezesha pia kupunguza msongamano wa migogoro ya kawaida sana kwenda kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya. Kwa kuzingatia hilo Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Kata. Kwa mujibu wa sheria Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Kata yanateuliwa na Ward C (Kamati za Maendeleo za Kata husika) na wajumbe wanakuwa ni wakazi wa eneo katika kata husika na wanawajibika kusikiliza migogoro yote inayotoka katika kata hiyo katika vijiji au mitaa ndani ya kata yao.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa tuna jumla ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata 3,956 kote nchini. Mabaraza haya yanafanya kazi kwa mujibu wa sheria; lakini bado pamoja na kazi kubwa ambayo mabaraza haya yamekuwa yakifanya kumekuwa na changamoto za aina mbalimbali. Hapa Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja na ushauri kwamba, bado ufanisi na kazi za mabaraza haujawa wa kutosha. Sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunakubaliana na Waheshimiwa Wabunge, ni kweli tuna Mabaraza ya Ardhi ya Kata, na yana majukumu yao ambayo yameelezwa, yanakuwa specified wanatakiwa kufanya nini kwa hatua ipi, lakini bado tunakubaliana kwamba kuna changamoto.

Mheshimiwa Spika, changamoto hizi zimetokana na sababu kadhaa. Sababu ya kwanza inatokana na wajumbe walio wengi kwa sababu wanapatikana katika vijiji na mitaa husika ndani ya kata husika, hawana utaalamu rasmi wa masuala ya kisheria na masuala ya ardhi. Kwa maana hiyo kumekuwa kuna maeneo baadhi ufanisi unakuwa si wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, pili, kumekuwa na changamoto za kibajeti na ndiyo maana ili kutatua changamoto hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tulitoa maelekezo mahsusi kwenda kwa Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri, kwamba kwanza wahakikishe mara wanapoteua wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi ya Kata wapate mafunzo maalum katika maeneo yale, ili wajue taratibu na sheria za ardhi zinavyowataka namna ya kwenda kutatua migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shughuli hizo zimekuwa zikifanyika mara kwa mara katika Mabaraza ya Ardhi ya Kata kwa kuwafanyia mafunzo na kuhakikisha kwamba angalau wanajua a,b,c,d za kutatua migogoro katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo tumesisitiza ni kwamba, halmashauri zote zihakikishe zinatenga fedha kwa ajili ya kuwezesha mabaraza ya kata kufanya majukumu yao ipasavyo. Ikiwemo kufanya vikao mara hoja zinapotakiwa kufanyika na pia kuhakikisha kwamba wanatenda haki kwa kuzingatia kukaa vikao vile kwa muda na kuwa na maamuzi ambayo yanazingatia taratibu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni kuzuia migogoro na pale ambapo inakuwa haijazuiwa, basi tunakwenda na hatua za kutatua migogoro. Kwa kiasi kikubwa migogoro mingi ambayo inatokea katika maeneo ya vijiji mitaa na kata zetu, haya Mabaraza ya Ardhi ya Kata yamesaidia sana kutatua migogoro hiyo. Tumekuwa mashahidi kwamba mara nyingi migogoro mingi sana inakwisha ndani ya mabaraza ya kata. Hata hivyo kuna migogoro ambayo inakuwa ni migumu inahitaji hatua za kisheria za juu zaidi. Migogoro hiyo inakuwa referred kwenda kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inatambua sana umuhimu wa mabaraza ya ardhi katika ngazi za kata, na inaendelea kuyaimarisha mabaraza hayo ili yaweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na yaweze kutatua migogoro ya wananchi kwa ufanisi mkubwa zaidi na kuweza kutenda haki pale ambapo kunakuwa na migongano ya hapa na pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na taratibu hizi ambazo zimwekwa na hatua ambayo Serikali imechukua moja kubwa ni kuendelea kuwasisitiza Viongozi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Sekretarieti za Mikoa, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuzingatia sheria za ardhi katika maeneo hayo na pia jinsi ya kuzingatia kanuni na taratibu za ardhi, ili kuepusha migogoro. Kwa sababu tunaamini njia pekee ya uhakika ni kutoa elimu kwa wananchi ili…

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): …waweze kujua sheria, taratibu na kanuni za kuzuia migogoro ya ardhi katika vijiji na matawi pamoja na kata hizo.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Timotheo Mnzava.

TAARIFA

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ninaomba nimpe taarifa mzungumzaji (mchangiaji) Mheshimiwa Naibu Waziri. Ni kweli Sheria ya Mabaraza ya Kata ipo, lakini ni vizuri TAMISEMI wakajua kwamba, kwa mujibu wa sheria ile mabaraza ya kata hayapo kwa ajili ya kesi za ardhi peke yake. Kwa hiyo, hata ile composition yake inavyokaa ni kwa sababu yanashughulika na mambo mengine nje ya mambo ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mabaraza yamekuwa na changamoto na ni muda sahihi sasa wa TAMISEMI kwamba, pamoja composition na sheria ile kuwepo, kuitafakari upya sheria ili iweze kutusaidia kutatua changamoto tulizonazo hasa mahususi kwenye eneo la upande wa sekta ya ardhi yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Dugange unaipokea taarifa hiyo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninaipokea taarifa hii ya Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli, nimetangulia kusema kwamba tunatambua kuwa tuna mabaraza ya kata, kimsingi, mabaraza ya kata yanafanya shughuli nyingi zikiwemo shughuli za kusuluhisha migogoro ya ardhi, masuala ya ndoa na mambo mengine mengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo na sisi tunaona umuhimu kwa sababu kwa sasa mwamko wa kumiliki ardhi umeongezeka miongoni mwa wananchi na hivyo migogoro imeendelea kuongezeka. Tunaona umuhimu sasa wa kuwa na baraza mahsusi ambalo linaweza likatatua migogoro hii kwa ufanisi mkubwa zaidi. Kwa hiyo tu kwamba niseme tunapokea maoni hayo na sisi Serikali tutakwenda kuyafanyia tathmini na kuona namna nzuri zaidi ya kuboresha ili ufanisi wa mabaraza ya ardhi ya kata uweze kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwasisitiza viongozi, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na menejimenti za mikoa yote nchini, pia Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara; kwanza kuhakikisha wanasimamia Mabaraza ya Ardhi ya Kata ili yaweze kutoa huduma ipasayo kwa kadiri ya sheria, maelekezo na taratibu ikiwemo kusimamia kuona kwamba yanafanya vikao mara kwa mara na pia kuhakikisha yanatenda haki. Pale ambapo yatahitaji kusaidiwa tuna Wakuu wa Idara, Wanasheria na Maafisa Ardhi katika halmashauri wanaweza wakaingia na kusaidia kabla ya kufanya reference kwenda kwenye ngazi ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, pili nitumie nafasi hii kusisitiza halmashauri zetu kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwezesha kazi za mabaraza ya ardhi ya kata ili yaweze kutoa huduma vizuri zaidi na kuendelea kuondoa migogoro ya wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaendelea kuyasimamia Mabaraza ya Ardhi ya Kata, ili yaweze kutatua migogoro hii.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)