Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kusema kwamba, naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kutoa mchango wangu nitoe pole kwa wananchi wa Jimbo la Kavuu, kata moja huko ambako ni wakulima maarufu wa zao la mpunga wakati wanafanya juhudi za kuondoa mpunga ule kwenye maji, ule mtumbwi waliokuwa wanautumia ulibeba wananchi kama 14, tumepoteza wananchi saba. Ilikuwa ni siku ya Ijumaa na leo ndiyo tumefunga hilo zoezi la kusaka miili mingine; lakini tumefanikiwa kupata miili minne.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo natoa pole sana kwa wananchi wangu hapo. Mungu akaziweke mahali pema peponi roho za marehemu wetu. Vilevile wale majeruhi waliopata msukosuko basi warejeshewe afya njema ili waweze kuendelea na shughuli zao.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ningeanza nalo ni kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini katika kusidia Wizara hii, kumsaidia Mheshimiwa Jerry katika kazi zake za Wizara hii. Vilevile kwa Mheshimiwa Rais kutuongezea uwezo Wizara katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru vilevile Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa jinsi wanavyoendelea kutupa miongozo ya kutekeleza majukumu yetu katika sekta hii ambayo katika mazingira ya kawaida ni sekta muhimu sana katika nchi yetu. Kwa kweli kutokana na umuhimu wake; kitu chochote kilicho na umuhimu mara nyingi kinagubikwa na mambo mengi ambayo migogoro ni sehemu ya mambo yanayojitokeza katika jambo lililo jema.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe mwenyewe, Naibu Spika, pamoja na uongozi wa Bunge kwa miongozo mbalimbali ambayo mmeendelea kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, nitajibu maeneo machache na mtoa hoja atakuja kujumuisha mambo yote. Nianze na Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi. Waheshimiwa Wabunge mbalimbali walichangia, ambao ni Mheshimiwa Edward Olelekaita, Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mheshimiwa Agnes Hokororo, Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga na Mheshimiwa Munira Mustapha, ambao kwa pamoja walizungumzia mambo mbalimbali yanayohusiana na tume, hasa kwenye suala la kuongezewa uwezo ili tume, iweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi na kwa muda mfupi katika kupambania mazingira ya kuiweka nchi katika utambuzi wa matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa vijiji ambavyo vimepimwa ni 10,000. Nataka kuweka tofauti kati ya kupimwa na kuboresha matumizi bora ya ardhi ya vijiji, isije ikawaletea confusion. Vijiji kati ya 12,318 sawa na 88% ya vijiji vyote hapa nchini. Kati ya vijiji hivyo vilivyoandaliwa matumizi bora ya ardhi ni vijiji 4,126 sawa na 33.5% ya vijiji vyote.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kukamilisha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji vilivyobaki, Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya tume kwa ajili ya kazi hiyo. Katika mwaka wa fedha huu wa 2024/2025 bajeti imeongezeka kutoka bilioni 3.41 hadi bilioni 5.04. Wizara katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 kupitia Mradi wa LTIP kiasi cha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kupanga vijiji 1,000 zimetengwa.

Mheshimiwa Spika, kuendelea kuhamasisha wadau ni njia nyingine ambayo tunaendelea kuitumia kwa ajili ya kupata fedha ambazo zinaweza zikasaidia, na hivyo katika mwaka 2024/2025 shilingi bilioni moja zitachangiwa na wadau. Hayo ni matarajio yetu makubwa kabisa. Wizara itaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuijengea uwezo tume

Mheshimiwa Spika, nataka niwape comfort Waheshimiwa Wabunge; jambo hili ni kubwa sana na hata Serikali imeliwekea umuhimu wa pekee. Kwa sasa tunaendelea na mazungumzo kati ya Wizara ya Fedha na Wizara yetu kuona kama tunaweza tukapata kile kiasi cha shilingi bilioni 120 ambalo ndilo kadirio la mwisho ambalo fedha hizi zikipatikana zitakamilisha nchi nzima kupimwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, tayari mawasiliano ya kiofisi yanaendelea; tumwombe Mwenyezi Mungu awajalie watu wa Wizara ya Fedha wawezeshwe na Mwenyezi Mungu, tushushiwe hizo fedha ambazo katika mazingira ya kawaida tume inaweza ikafanya kazi katika muda mfupi sana. Kwa sababu ni ukweli usiopingika kwamba zoezi hili la kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi limetoa matokeo makubwa sana katika kutatua migogoro mbalimbali katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, once wanapopima wakimaliza hata ile migogoro iliyokuwepo inakuwa ndiyo mwisho wa safari ya mgogoro ule. Hayo tumeyabainisha katika maeneo mbalimbali na ambayo katika mazingira ya kawaida yameonesha mafanikio makubwa sana. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inapambania kupata fedha, ili ziweze kwenda kutuletea matokeo ambayo ni matarajio ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, sambamba na eneo hili Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu elimu inayotolewa wakati wa zoezi zima la kwenda kufanya maboresho kwenye maeneo ya vijiji. Kuna hatua kama saba ambazo tunazipitia. Kwanza, ni kuhakikisha tu kwamba tunapofika kwenye vijiji wale wanavijiji wanakuwa ni watu wanaotangulizwa mbele katika kuandaliwa kupokea ule mradi. Kwa hiyo elimu inatolewa na kamati zinazokwenda kusimamia utambuzi wa yale maeneo ni kamati za wanakijiji wenyewe, tunaunda timu maalum ambayo kwa wale ambao bahati mbaya sana siyo rahisi kuwabeba Waheshimiwa Wabunge wote kwenda kwenye maeneo haya, lakini tumeipeleka Kamati maeneo mbalimbali, wameshuhudia kwamba tafsiri ya kutambua matumizi ya ardhi katika vile vijiji haitolewi na afisa ardhi.

Wale wameshibishwa kuelewa jinsi tutakavyokwenda kutumia lile eneo lao na wao ndiyo wana-own, wanabeba ule uzito wa kutambua matumizi bora ili waweze kuwa ni sehemu ya walinzi wa ile miradi. Kwa hiyo, ikitokea kuna maeneo ambayo Maafisa Ardhi wanaenda kulazimisha, ninaomba sana Waheshimiwa Wabunge tupewe taarifa haraka kwa sababu ownership ya usimamizi wa mradi ule inafanywa na wananchi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tunakuwa tu kama wataalamu na hata ukienda kule wao ndiyo wanaojua kabisa kijiji chao kinapakana na hiki, mtaa huu nani anapakana na nani na kule tuna Kamati ambayo haiishii tu kwenye kipindi kile cha zoezi, inaendelea na shughuli hizo katika muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, maeneo yale kwenye vijiji, nimemsikia Mheshimiwa Getere, ninadhani hata Mheshimiwa Olelekaita; masuala ya kulazimisha WMA kwenye maeneo ambayo tunakwenda kutambua, itambuliwe kwamba, Sheria ya WMA iko chini ya vijiji vyenyewe. Wala ile siyo ardhi inayosimamiwa na Maliasili wala siyo ardhi inayosimamiwa na mamlaka nyingine yoyote.

Mheshimiwa Spika, uamuzi wa kulinda msitu ule ulioachwa kwenye eneo lile la kijiji kile ni wa wananchi wenyewe na unapitia kwenye vikao vyao vya wazi na hata hiyo WMA kwa sababu inaweza ikawa inaleta matokeo, hata uongozi wa WMA ni wa wananchi wenyewe. Wala hakuna kiongozi mwingine wa Serikali anayeweza kusimamia lile eneo.

Mheshimiwa Spika, niwape tu mfano, kwangu kuna WMA ambayo inasimamiwa na wananchi wenyewe kwa kuchaguana wao wenyewe. Kwa hiyo, kama haya yako kwenye maeneo yetu huko tunakotoka, ninaomba tu wananchi waelewe kwamba mpango wa matumizi bora ya ardhi na mkaacha na eneo la reserve, maamuzi juu ya mnalitumiaje lile eneo kawaida linafanyiwa maamuzi yake na wananchi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba tu, kama kuna mashinikizo yanatolewa, basi hayo mashinikizo siyo sahihi, wanatakiwa viongozi wote ambao wanasimamia zoezi hili cha kwanza waanzie kwenye elimu. Waweze kutoa elimu ya kutosha juu ya wanachokifikiria wananchi wale kukitenga kwa ajili ya matumizi yao ya baadaye na maeneo mengine wanagongana kwa sababu wanataka kutenga eneo la kufugia, lakini at a same time wanajikuta wana maeneo ambayo wangetaka kuhifadhi. Kwa hiyo, haya ni maamuzi ambayo kijiji kinaweza kikaamua kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, urejeshwaji wa fedha za miradi ya kupanga, kupima na kumilikisha; Waheshimiwa Wabunge, Wizara itaendelea kushirikiana na TAMISEMI zile fedha ambazo zimeenda kule kwa ajili ya mikopo na kwa kweli ninatumia Bunge lako Tukufu kuwahamasisha Wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali nchini kurejesha fedha hizi ambazo kimkakati Serikali ililenga kutuwezesha sisi watu wa Wizara ya Ardhi kupima maeneo ya nchi yetu, hasa kwenye miji inayochipukia kama halmashauri hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halmashauri zingine usimamizi wa zile fedha umekuwa ni hafifu sana na wanashindwa kurejesha kwa wakati ili na wenzao waweze kuzipata. Ninaamini wazi wananchi wamesikia kilio cha Wabunge ambao hawajafikiwa na miradi hii lakini sisi kama Wizara tunaendela kujipanga kuona namna nzuri ya kuendelea kuhamasisha halmashauri kurejesha zile fedha.

Mheshimiwa Spika, hata kwenye miradi mingine sasa hivi tumebaini, ni lazima sisi wenyewe tuzisimamie zile fedha kwa sababu tumeshapima uaminifu wa halmashauri una kasoro kasoro, basi hata kama halmashauri itapata, usimamizi wa matumizi ya ile fedha katika miradi wanayopanga halmashauri itasimamiwa na Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Waheshimiwa kwa namna mbalimbali wameweza kulizungumzia ni suala la utatuzi wa migogoro ya ardhi katika vijiji 975. Baraza chini ya ile Kamati ya Mawaziri Nane ilishatoa ufafanuzi wa majibu mbalimbali katika namna ya kutekeleza maeneo mbalimbali yanayopitiwa na mradi huu.

Mheshimiwa Spika, tumechukua lile la Mheshimiwa Kawawa ambalo alisema kwenye kijiji chake kuna watu wana uasili, lakini mazingatio makubwa kwa sababu hata haya maamuzi ya Kamati ya Mawaziri Nane ilipita huko na kujiridhisha juu ya maelezo ya msingi ambayo yalisababisha maamuzi hayo yakatokea. Bado milango iko wazi, Wizara hii ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ile ya Mawaziri Nane, kama kuna hoja zingine za msingi ambazo tunaweza tukazipokea na tukakaa kwenye kiti kimoja tukazungumza, then tuone, lakini maamuzi ya Baraza la Mawaziri lile ambalo lilitumwa na Mheshimiwa Rais, kimsingi tumetumia lile kama mwongozo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchakato wa kupitia Sera ya Ardhi, Mheshimiwa Waziri atalieleza vizuri na sababu za msingi kwa nini tumeleta sera mpya. Mheshimiwa Waziri ana maelezo ya ndani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Ardhi; ninampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa mchango wake kuhusu Mabaraza haya ya Kata. Tuliyaondolea uwezo wa kuwa wanatoa hukumu kwa sababu hawana Vyombo vya Kisheria. Mwenyekiti ni mwananchi mwenzao, hana elimu ya sheria ambayo inaweza ikamsaidia kutoa uamuzi wenye haki kwa sababu, vigezo vya sheria vinampeleka mtu darasani. Lazima asome ajue miiko, hapa mmeamua nini na hapa mmeamua nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninadhani Serikali ilipoyapitia yale maamuzi mbalimbali yaliyofanywa na Mabaraza ya Kata, iliona ni muhimu waishie kwenye usuluhishi, upatanishi ili kujenga misingi mizuri ya mahusiano katika kile kijiji au katika ile migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye Mabaraza ya Wilaya, haya ni kweli Wabunge wamesema wanabaini yana changamoto. Siyo kwamba wamebaini wao tu, toka tumeingia na Mheshimiwa Waziri hapa, jambo la kwanza tunaendelea kuangalia uwezekano wa kufanya maboresho. Hapa hapa nina sauti mbili katika Mabaraza haya, moja ni ile process ya Serikali kuyahamisha Mabaraza haya kurudi Mahakamani, lakini yale hata yakichelewa hayajatuzuia sisi kuendelea kutengeneza mpango mzuri wa kuhakikisha Mabaraza haya yanatoa haki iliyo sawa. Kwenye Mabaraza huko hakuna prosecution hakuna nini, nako kuna vitu ambavyo kama Wizara tumeanza kuviangalia ili tuviweke vizuri ili baadaye huko tuweze kuona namna ambavyo tunaweza, wale Wenyeviti wakatoa haki zinazolingana na uhalisia wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili la Mabaraza, vilevile, hatujafungua Mabaraza nchi nzima kwa maana kwamba hatujateua wale Wenyeviti. Process yake ni kwamba tumebakiza Wenyeviti kama 35 katika halmashauri zote na hili limeshafikia kwenye mchakato. Tuliona hatuwezi kumleta mtu ambaye hana hata experience ya kufanya kazi. Kwa hiyo, Serikali tulikubaliana kwamba tuchukue wanasheria ambao tayari wako kazini tuwahamishie kwetu ili hata wanapokwenda kukalia meza za maamuzi angalau wawe na reference mbalimbali. Maana sheria inataka vilevile uwe na uwezo wa utangulizi, experience na vitu vingine katika kuamua jambo ambalo linahusisha haki za watu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili tunaendelea na mchakato na niwape comfort tu Waheshimiwa Wabunge, tunakwenda kukamilisha zoezi hili la kuwaletea Wenyeviti wa Mabaraza haya. Nia yetu ni kwa wilaya zote hapa nchini ziweze kuwa na uwakilishi wa hawa Wenyeviti ili kuwapunguzia adha wale wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Kiteto, Mwenyekiti wa Baraza anatoka Dodoma, mbali sana na hapa pana mrundikano wa kesi nyingi sana. Kwa hiyo, ile jam haimpi nafasi ya kuhudumu kwenye maeneo mengine kwa uhuru wa kutosha. Kwa hiyo, haya yote haya tumeyaona na kuna maeneo mengine ni mbali sana. Ni mbali mno kutoka wilaya moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba nimalizie, la kumalizia ni kwamba yale yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa kwetu ni maelekezo, ushauri, kwa kweli leo ninapata nguvu ya kutosha kabisa. Wabunge watakumbuka ndiyo nilikuwa ninaingia kwenye Bajeti ya mwaka jana, ile presha ilisababisha maradhi ya kutumia vidonge, lakini ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu, kwa kweli kwa mwenendo huu wa kuendelea kutuamini tunakwenda kufanya kazi ambayo wataiona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wangu toka ameingia, katika mazingira ya kawaida lazima ujifunze kutoka kwa aliye juu yako. Ninajifunza vitu vingi sana kutoka kwa kaka yangu hapa Mheshimiwa Jerry, ni mtu ambaye anasimama kwenye sheria na Wabunge wameona wote hapa nchini shughuli tunayokwenda kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi kukaa ofisini wakati Waziri wangu yuko kazini, kwa hiyo kwa mwendo wake ule ule na bahati nzuri mimi msaidizi wake ni mwanajeshi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninamsaidia kwenda mahali popote ambapo kiatu chake hakifiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema nitaendelea kumpa ushirikiano Mheshimiwa Waziri, nitamshauri kwa hekima na kwa wakati wote, anitumie kadiri atakavyoweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)